Watoto 20,000 waliozaliwa na walowezi enzi ya ukoloni walisafirishwa Ubelgiji kwa lazima

Sanamu za kiafrika katika makavazi kuu ya Ubelgiji Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Sanamu za kiafrika katika makavazi kuu ya Ubelgiji

Waziri mkuu wa Ubelgiji, Charles Michel, ameziomba msamaha nchi za Burundi, DR Congo na Rwanda kwa kuhusika na maelfu ya visa vya utekaji nyara wa watoto waliozaliwa na walowezi wa nchi hiyo zama za ukoloni.

Watoto hao wanaosadikiwa kuwa karibu 20,000 walichukuliwa kwa nguvu kutoka kwa mama zao waafrika na kupelelewa na kanisa katoliki na taasisi zingine zanchini Ubelgiji.

Baadhi ya watoto hao ambao walizaliwa miaka ya 1940 na 1950, hawakuwahi kupewa uraia wa Ubelgiji hali iliowafanya kuishi kama watumwa..

Akilihutubia bunge la nchi hiyo,Bw. Michel alikiri kuwa Ubelgiji ilikiuka haki ya kimsingi ya watoto hao, kwa kuwachukulia kama tisho kwa mfumo wa ukoloni.

Ubelgiji iliwavua uraia wao, kuwabagua na kuwatenganisha na jamaa zao.

"Hatua hii itatusaidia kutambua rasmi sehemu ya historia yetu ya kitaifa,"alisema katika taarifa yake.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Charles Michel, Waziri mkuu wa Ubelgiji akihutubia bunge la nchi hiyo

Miaka miwili iliyopita kanisa katoliki iliomba msamaha kuhusu jukumu lake katika sakata hiyo.

Na mwaka jana wabunge wa Ubelgiji walitoa wito kwa serikali kuwapa usaidizi watoto waliyoathiriwa kupata wazazi wao na pia kupewa uraia wa nchi hiyo

Huku hayo yakijiri mama zao za watoto hao pia wamekuwa wakiwatafuta tangu walipochukuliwa kutoka kwao kwa lazima.

Georges Kamanayo, mmoja wa watoto waliopelekwa Ubelgiji amesema hatua ya Bw. Michel ni "Utambuzi wa hakika kuwa walidhulumiwa".

''Tumejihisi kama watu duni nchini Ubelgiji kwa muda mrefu, tulijaribu kujichangaya na jamii ya wabelgiji lakini ilikuwa vigumu kwasababu tulitengwa na jamii hiyo." aliiambia gazeti la De Standaard.

Ubelgiji inatajwa kuwa moja ya koloni katili zaidi enzi hizo na inakadiriwa kuwa waafrika kati ya milioni 10 na 15 waliuawa chini ya utawala wao katika Congo ya Ubeligiji ambayo sasa ni taifa la Jumhuri yaKidemokrasia ya Congo.

Mwezi uliyopita , jopo la wataalamu kutoka umoja wa mataifa lililopewa jukumu la kuchunguza watu wa asili ya kiafrika wanaoishi Ubelgiji liliiambia taifa hilo kuomba msamaha kwa madhila iliyofanya enzi ya ukoloni.

Ubaguzi wa rangi ulikuwa mbaya sana katika taasisi za elimu za Ubelgiji, wataalamu wa walisema katika ripoti yao.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Ubelgiji Bw. Michel hata hivyo hakuzungumzia ripoti hiyo ya Umoja wa mataifa.

Bunge limesema kuwa hatua yake ya kuomba msamaha watu wa asili ya kiafrika waliotekwa na kupelekwa nchini humo wakiwa watoto wadogo lazima isaidie kuimarisha mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini humo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii