Ripoti ya CAG yabainisha hali mbaya ya kifedha kwa mashirika ya Umma Tanzania

Ripoti ya CAG yabainisha hali mbaya ya kifedha kwa mashirika ya Umma Tanzania

Ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali nchini Tanzania (CAG) Prof Mussa Assad ya mwaka wa fedha 2017/2018 imewasilishwa leo bungeni mjini Dodoma.

Ripoti hiyo imebainisha hali mbaya ya kifedha kwa mashirika ya umma, matumizi mabaya ya fedha kwa vyama vya siasa na kudai kuwa katika ripoti iliyopita ni mapendekezo 80 pekee kati ya 350 yaliyofanyiwa kazi kikamilifu.

Mwandishi wetu Yusuph Mazimu ana taarifa zaidi:

Ripoti hiyo inayohusu taasisi 241 zilizokaguliwa pamoja na vya siasa na kati ya hizo 234 zilikua na hati safi ambazo ni sawa na asilimia 97 sita zikiwa na hati zenye mashaka.

Taasisi zenye hati chafu ni Tume ya huduma za walimu, Idara ya Deni la Taifa na Huduma za Jumla, Idara ya Uhamiaji,Chuo cha sanaa Bagamoyo, Ubalozi wa Tanzania Zambia ,Tume ya Taifa ya Matumizi Bora ya Ardhi na Hazina.

Mambo yaliyogundulika kwenye Ripoti ya CAG

Matumizi ya fedha za Umma:Matumizi ya shilingi bilioni 4.66 yalitekelezwa na Ofisi ya Mwanasheri Mkuu wa Serikali kwenda Kampuni binafsi za huduma za kisheria bila kufuata makubaliano ya mikataba.

Bima ya Afya: Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umefanya malipo hewa ya shilingi bilioni 3.

Mishahara kwa Marehemu: Mamlaka 17 za Serikali za mitaa zilifanya malipo ya mishahara ya shilingi milioni 207.37 kwa watumishi ambao walikoma kufanya kazi kati yake shilingi milioni 128.31 zililipwa kwa waliofariki na wastaafu.

Polisi: Jeshi la polisi lilishindwa kuonyesha monitor 58 za Kompyuta za shilingi milioni 159.1, pia mzabuni Lugumi alilipwa shilingi milioni 195.22 kwa ajili ya monitor 213 ambazo hazikuonekana.

Tume ya uchaguzi:Tume ya taifa ya uchaguzi ilinunua mashine za kielektroniki (BVR) 8,000 kwa ajili ya usajili wa wapigakura, kati ya hizo 5,000 hazikukidhi vigezo hivyo kusababisha Serikali kuingia hasara ya shilingi milioni 862.08.

Malipo ya posho:Ripoti imeeleza kuwepo matumizi yasiyostahili ya shilingi milioni 859.14 yaliyofanyika katika mamlaka za serikali za mitaa 36 kwa sababu hakukuwa na fedha zilizotengwa kwenye bajeti.

Sare za Polisi:Jeshi la Polisi lililipa shilingi bilioni 16.66 kwa ajili ya sare za askari bila kuwapo ushahidi wa uagizaji na upoakeaji wa sare hizo.

Miradi:Ukaguzi ulibaini miradi 10 ambayo Serikali ilitakiwa kuchangia sh bilioni 118.44, ilichangia sh bilioni 7.43 sawa na asilimia sita tu.Hii ilisababisha upungufu wa sh bilioni 111.01

CCM:Hakikuwasilisha michango ya kila mwezi NSSF ya shilingi bilioni 3.74, ilifanya pia matumizi ya shilingi 604,996,994 bila nyaraka toshelevu.

CHADEMA:Walinunua gari la shilingi milioni 147.76 na kulisajili kwa jina la mwanachama badala ya bodi ya wadhamini,walifanya pia matumizi ya sh 134,646,740 bila nyaraka toshelevu.