Magufuli amtaka waziri 'avute bangi'

Rais Maguli
Image caption Rais wa Tanzania, Dokta John Magufuli ameonyesha kutoridhishwa na utekelezwaji wa miradi ya maji

Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli amemtaka waziri wa maji na umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa kuwa mkali kusimamia miradi ambayo imekusudiwa na serikali.

Alipokua kwenye ziara ya kikazi mkoani Njombe, nyanda za juu kusini mwa Tanzania Rais Magufuli amekagua miradi mbali mbali ikiwemo kufungua barabara ya Mafinga mpaka Igawa yenye umbali wa kilometa 138.7.

Kando na hilo Magufuli ameonyesha kutoridhishwa na utekelezwaji wa baadhi ya miradi ya maji nchini Tanzania. Magufuli kwa lugha ya utani alimtaka waziri wa Maji Prof Mbarawa kuvuta bangi ili kuwa mkali.

Amesema katika uhakiki wa miradi ya maji kuanzia mwaka 2013 mpaka 2018 palikua na miradi ya maji iliyohakikiwa na wataalamu kutoka wizara ya fedha ambapo kulikua na miradi ya thamani bilioni 119 miradi ya kweli ilikua na thamani ya bilioni 17.

Rais Magufuli amesema watanzania si wajinga

Jinsi polisi walivyozuia maandamano Tanzania

Kati ya bilioni 119 madai ya kweli ya mradi uliofanyika ni bilioni 17 kwa hiyo miradi mingine yote ilikua hewa.Watu walidai fedha kuwa wamefanya kazi ya miradi ya maji lakini maji hayakuwepo hivyo ni sawa na kusema miradi hewa na hizo fedha hazikulipwa.

Amemueleza waziri wa maji: ''Nimekupeleka pale ukafanye mabadiliko Ili miradi ya maji iliyopangwa hapa makambako yenye thamani ya bilioni 45 na umesema makandarasi watakua kwenye site ikifika mwezi wa tisa, ukalisimamie hilo

Rais Magufuli ameeleza kuwa na matatizo na baadhi ya miradi ya maji nchini hali inayofanya kufanya mabadiliko kwenye miradi ya maji hata kwa mawaziri kwa kuwa haoni faida yake kwa wananchi.

''Zinazungumzwa fedha zimeenda kwenye miradi lakini hazikwenda, kuna wakati nilienda kanda ya ziwa ninauliza mradi wa maji uko wapi zimetumika milioni 400 zilikua milioni 800 lakini maji hayapo''

''Sasa nikuombe waziri na watendaji wako mkawe wakali kweli kweli kama una uwezo wa kuvuta bangi ya njombe ili uwe mkali kaivute, kaivute kisirisiri ili wasikuone ukiivuta ili ukienda kwenye mradi hawa mainjinia wa maji wakafanye kazi''.Alisema Rais Magufuli

Mada zinazohusiana