Madaktari wa Cuba nchini Kenya watekwa na washukiwa wa Al-Shabaab

Some 100 Cuban doctors follow proceedings during their induction programme at the Kenya School of Government, on June 11, 2018 in Nairobi. - The doctors will be posted to various hospitals in Kenya's 47 counties. Each county is expected to get at least two doctors Haki miliki ya picha SIMON MAINA
Image caption Madaktari 100 wa Cuba katika mapokezi nchini Kenya mnamo Juni 11 2018 - wanahudumu katika hospitali tofauti nchini Kenya

Taarifa tunazopokea ni kwamba madaktari wawili wa Cuba nchini Kenya wametekwa nyara na washukiwa wa kundi la Al-Shabaab katika mji wa Mandera.

Inaarifiwa kwamba mkasa huo umetokea mapema leo asubuhi wakati madaktari hao wakielekea kazini katika mji huo uliopo katika eneo la kaskazini mashariki mwa Kenya.

Mwandishi wa BBC katika eneo hilo la Mandera Bashkas Jugosdaay anasema walinzi wa madaktari hao wameuawa na washambuliaji wamefanikiwa kutoroka kwa kutumia gari aina ya Probox.

Hatma ya madaktari hao wa kigeni haijulikani kufikia sasa.

Inaarifiwa madaktari hao wanaishi karibu na makaazi ya Gavana wa eneo hilo ambayo ni kilomita takriban 4 kutoka eneo la mpaka na Somalia.

Haijulikani ni washambuliaji wangapi waliokuwa ndani ya magari aina ya Probox ambayo kwa mujibu wa duru yalikuwa yameegeshwa karibu na makaazi hayo.

Milio ya risasi imesikika katika mji wenyewe wa Mandera na kwa sasa maafisa wausalama wanawasaka watekaji hao.

Akihotubia waandishi habari msemaji wa Polisi Charles Owino amesema wahalifu hao walitoroka na gari hilo mpakani kuingia Somalia.

Kufikia sasa, Owino anasema gari hilo la serikali ya kaunti hiyo limepatikana na sereva wake anahojiwa.

Madaktari hao ni miongoni mwa kundi la madaktari zaidi ya 100 kutoka Cuba waliowasili Kenya kwa ombi la serikali kuja kupunguza uhaba wa madaktari nchini humo.

Miongoni mwa madaktari walio kwenye kundi hilo kutoka Cuba ni wataalamu watano wa figo, wataalamu wa x-ray, wataalamu wa mifupa na maungio na wataalamu wa mfumo wa neva.

Wamekuwa wakitoa huduma na kushauriana na madaktari wengine katika maeneo tofauti nchini.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii