Spika Ndugai amemtaka CAG ajiuzulu kwa kuwa Bunge limekataa kufanya naye kazi

Job Ndugai Haki miliki ya picha BUNGE
Image caption Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amtaka Profesa Assad ajiuzulu

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ameonyesha wazi kukerwa kwa namna ambavyo Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali Profesa Musa Assad ambavyo hakujutia kauli yake inayodaiwa kuwa ya dharau dhidi ya Bunge la Tanzania.

''Tatizo letu ni maneno ambayo Profesa Musa Juma Assad aliyasema kule Marekani, na majuzi alipowaita waandishi wa habari Dodoma akarudia tena kwamba ataendelea kuyasema maneno hayo.Maneno yale sisi tumeyakataa kuwa si maneno ya kistaarabu hilo ndio tatizo, na sio taarifa iliyotolewa.''Alisema Ndugai

Tukampa nafasi tukamuita ndio utaratibu wetu , akahojiwa na kamati akasimamia msimamo wake.Jambo lake likaingia Bungeni Bunge likaazimia kutofanya kazi naye

Ndugai amesema kuwa Kwenye hadidu za rejea za ukaguzi za kila mwaka, haijawahi kutokea ajenda ya kulifanyia tathimini Bunge, hakuna tangu uhuru, kinachofanyika hata kama ni kwa ofisi ya Bunge.

Spika amesema Profesa Musa Assad amefanya kosa linaitwa 'contempt of Parliament' (kulidharau Bunge).Katika kutekeleza majukumu yake CAG hakupaswa na hapaswi kulitukana Bunge kwa lugha zile za 'rejereja',na kuwa Bunge linasimamia kazi na majukumu yake lenyewe na haliwezi kukaguliwa lakini linatimiza majukumu yake kwa kufuata kanuni za bunge hivyo profesa hawezi na hakuwahi kufanya kama alifanya alifanya kazi ambayo si yake.

Haki miliki ya picha BUNGE
Image caption Ndugai:CAG ametanda kosa la kulidharau Bunge

''Neno dhaifu ni neno ambalo kihasibu mkaguzi hulitumia anapoongelea Taasisi anayoifanyia ukaguzi na akimaliza uhasibu wake huwataarifu wadau wadau ripoti yake. kwa upande wa taasisi ya Umma ni serikali ndio wanakaguliwa na yeye na mdau hapa ni Bunge kwa niaba ya wananchi.''

Amemshangaa Assad akisema ameogopa kuelekeza hoja zake mahali alikokusudia na kuamua kuhusisha kundi jingine ambalo halihusiki:''Sisi ndio wasimamizi wa serikali kwa niaba ya wananchi, tunasimamia mambo mengi moja wapo ni masuala ya fedha.''

''Lakini yeye amewekwa na Ofisi yake kuwa jicho la Bunge, kuangalia na kuliambia Bunge ndio kazi yake. Hawezi tena kugeuka akafanya alichokifanya.''

''Ningependa kumwambia kuwa 'hatupendi'.. na kutokana na hilo kuonyesha kuwa hatupendi tumechukua hatua kali hata kwa wenzetu mheshimiwa Halima Mdee na Godbless Lema ambao ni wabunge wenzetu.Tunasisitiza hatupendi kitu hicho.''Kwa hiyo kuendelea kurudia na kuahidi kwamba utarudia....Haya rudia, tutakuita tena.Nadhani itakua mbaya zaidi.''

Spika Ndugai ametaka Profesa Assad aliache jambo hilo na kuwa tayari Bunge limepokea taarifa na kuahidi kufanyia kazi kama ilivyo ada na watanzania watapanya mrejesho wa kila jambo lililotajwa ndani ya ripoti.

Bunge la Tanzania lamtia 'hatiani' CAG

CAG Assad: Natekeleza majukumu yangu kikatiba

''Lakini msisitizo wetu ni mmoja, kwa kuwa Bunge lilikwishafanya uamuzi ya kwamba halifanyi kazi na 'mtu' anayeitwa Profesa Juma Assad kwa sababu ya kulidhalilisha Bunge,uamuzi huo ni uamuzi halali na haungiliwi na mtu yeyote.''

''Katika nchi za wenzetu kote, ikifika mahali Bunge limeonyesha kutokua na imani nawe unajiuzulu, hung'ang'anii lakini si kazi yangu wala wajibu wangu kumfundisha nini cha kufanya Profesa Assad.Anampa mheshimiwa Rais wakati mgumu bure tu.'' lakini tutaendelea kufanya kazi na ofisi ya ukaguzi ya taifa.Ofisi ina maafisa wengi wa kutosha kama lilivyo Bunge.''

Mvutano huu ulianzaje?

Mvutano ulianza baada ya CAG kufanya mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya redio ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York mwezi Disemba 2018 ambapo alisema kuwa Bunge la Tanzania halina meno na hivyo limeshindwa kuiwajibisha ipasavyo serikali.

"…Kama tunatoa ripoti na inaonekana kuna ubadhilifu halafu hatua hazichukuliwi huo kwangu mimi ni udhaifu kwa Bunge. Bunge linatakiwa liisimamie (serikali) na kuhakikisha kuwa pahali penye matatizo basi hatua zinachukuliwa...Sie kazi yetu ni kutoa ripoti tu na huo udhaifu nafikiri ni jambo la kusikitisha lakini ni jambo tunaamini muda si mrefu huenda likarekebishika. Lakini tatizo kubwa tunahisi kwamba bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa," Profesa Assad aliiambia radio ya UN.

Spika Job Ndugai alilieleza Bunge mwezi Januari kuwa maelezo ya Assad yalioonesha dharau kubwa dhidi ya mhimili huo na kumtaka aende mbele ya kamati kwa hiyari yake, ama apelekwe kwa pingu.

Haki miliki ya picha NAOT
Image caption Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali, Profesa Musa Assad

Kumwondoa kazini CAG

Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, CAG huondoka madarakani baada ya kufikisha umri wa kustaafu ama kujiuzulu wadhifa wake.

Ibara 144 ya katiba pia inasema CAG anaweza kuondolewa katika madaraka ya kazi yake kwa sababu ya kushindwa kutekeleza kazi zake (ama kutokana na maradhi au sababu nyingine yoyote) au kwa sababu ya tabia mbaya, au kwa kuvunja masharti ya sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Hata hivyo, kuna utaratibu maalumu wa kumwondoa ambapo ibara ya 144 (3) inabainisha kuwa iwapo rais ataona kwamba suala la kumwondoa kazini CAG lahitaji kuchunguzwa, basi atateua Tume Maalum ambayo itakuwa na Mwenyekiti na Wajumbe wengine wasiopungua wawili.

Mwenyekiti na angalau nusu ya wajumbe wengine wa tume hiyo itabidi wawe watu ambao ni Majaji au watu waliopata kuwa Majaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani katika nchi yoyote iliyomo kwenye Jumuiya ya Madola.

Iwapo Tume itamshauri rais kwamba huyo CAG aondolewe kazini kwa sababu ya kushindwa kufanya kazi kutokana na maradhi au sababu nyingine yoyote au kwa sababu ya tabia mbaya, basi rais atamwondoa kazini.

Wakati wa uchunguzi, rais anaweza kumsimamisha kazi CAG. Lakini uamuzi huo utabatilika ikiwa Tume itamshauri rais kwamba huyo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu asiondolewe kazini.