Wazazi wa Chibok wakutana na TB Joshua wakiwa na matumaini ya kuwapata watoto wao

Mama Godiya Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bintu Bitrus, Mama wa Godiya, binti aliyetekwa nyara akisali na wazazi wengine

Katika mfululizo wa barua kutoka kwa waandishi wa kiafrika, Mwandishi wa Nigeria Adaobi Tricia Nwaubani anasema wazazi wa wasichana wa Chibok waliopotea, wamekosa matumaini ikiwa ni miaka mitano baada ya mabinti zao kutekwa nyara.

Wazazi wa wasichana wanahofu kuwa kuna nguvu isiyoonekana kwa macho, zaidi ya Boko Haram ambayo imekua chanzo cha masumbufu waliyoyapitia katika kipindi cha miaka mitano tangu watoto wao walipochukuliwa shuleni Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.

Zaidi ya wasichana 200 walitekwa wakiwa kwenye mabweni tarehe 14 mwezi Aprili mwaka 2014, 107 wakiwa wameokolewa au kuwekwa huru baada ya mazungumzo na Serikali ya Nigeria na wanamgambo wa kiislamu huku wengine zaidi ya 100 wakiwa hawajulikani walipo.

''Kuna kitu kinatufuata kwa namna moja au nyingine,'' anaeleza Yakubu Nkeki, Mwenyekiti wa Umoja wa wazazi wa watoto waliotekwa nyara na ambaye mpwawe alikua miongoni mwa kundi la mwisho la wasichana walioachiwa mwezi Mei mwaka 2017.

Boko Haram wameshindwa?

Mfahamu rais wa Nigeria Muhammadu Buhari

Mwezi Aprili mwaka jana, wazazi wa baadhi ya wasichana walioachiwa huru ghafla walipata ajali.Walikua wakisafiri pamoja wakielekea mkutanoni katika Chuo Kikuu mjini Yola ambako mabinti zao walidahiliwa kwenye masomo ambayo yalifadhiliwa na Serikali.Mzazi mmoja alipoteza maisha papo hapo huku wengine 17 wakipelekwa hospitali kutokana na majeraha waliyoyapata.

Mwezi Januari mwaka huu, ndugu 18 wa wasichana ambao bado hawajulikani walipo, ambao wanafadhiliwa na kituo cha msaada, walikua wakirejea shuleni wakati chombo cha moto walichokuwa wamekodi kupata ajali. Wanane kati yao walipata majeraha, pia aliyejeruhiwa vibaya Zannah Lawan, Katibu wa umoja wa wazazi, aliyekuwa akiwasindikiza wanafunzi shuleni.

Kukua kwa chuki

Majuma kadhaa baadae, mwezi Machi, watoto waliokuwa wamejeruhiwa walikua tayari kurudi kwenye masomo yao.Bwana Nkeki aliongozana nao kwenda shule, akawashusha na kuwarejesha nyumbani.Gari alilokodi ambalo alikua akisafiri nalo likapata ajali.

''Gari ilipinduka lakini sikujeruhiwa,'' alisema, lakini akaongeza, ''Mambo haya si ya kawaida.''

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rifkatu Galang, alitekwa akiwa na miaka 17, bado hajapatikana

Wanachama wa umoja wa wazazi 34 wamepoteza maisha baada ya mabinti zao kutekwa nyara na sasa, kutokana na ajali, maradhi, na zaidi mashambulizi ya Boko Haram.

Bwana Nkeki pia ana wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa chuki miongoni mwa jumuia ya wazazi.Mikutano imekua ikimalizika kwa malumbano, wazazi wakijaribu kupigana wenyewe kwa wenyewe.

Mwaka jana, baadhi ya wazazi wa watoto waliopotea walitishia kuzuia msafara wa mabasi unaowachukua watoto walioachiwa huru kupelekwa Yola, baada ya mapumziko ya majira ya joto.Walikua wakihisi kuwa kuachiwa kwa baadhi ya wasichana na kurudi kwao shuleni kumefanya umakini wa kuwafikiria wengine ambao bado wanashikiliwa umeondoka kabisa.

''Sipendi kuwaalika wote kwa wakati mmoja kwenye mikutano,'' Alisema bwana Nkeki. ''Wakati mwingine nachagua watu wachache ambao husikilizana vizuri na kupeleka ujumbe kwa wengine.''

Wakati huohuo, tishio la Boko Haram ni tukio la kweli kwa watu wa Chibok-ambapo mchanganyiko wa watu wa imani ya kikristo na kiislamu wanaishi.Pamoja na mafanikio ya jeshi kudhibiti eneo hilo kutoka mikononi mwa wanamgambo.

Majuma kadhaa yaliyopita, Boko Haram walifanya uharibifu katika vijiji saba wakiharibu makazi yakiwemo ya watu ambao watoto wao waliachiwa huru na kuendelea na masomo katika chuo kikuu cha Yola.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Baadhi ya walioachiwa wanasoma chuo kikuu cha Amerika huko Yola

''Kinachoendelea Chibok ni kibaya sana,'' alisema Nkeki.''Watu wengi hawako majumbani mwao.''

Wazazi wa Chibok wanatazama kutekwa kwa watoto wao ni moja ya mfululizo wa matukio ya bahati mbaya kukumba watu na jamii yao.

Kutafuta miujiza

Katika kumbukumbu ya miaka mitano ya vitendo vya kutekwa nyara kwa wasichana, ambavyo viliishitua dunia na kuanzisha kampeni ya #BringBackOurGirls sasa wazazi wanaomba msaada wa kiimani.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mchungaji TB Joshua

Mwanzoni mwa mwezi huu, wawakilishi wa jumuia ya wazazi walisafiri zaidi ya saa 48 kwa barabara kutoka Chibok kwenda Lagos kukutana na mchungaji maarufu TB Joshua.

Ni mwanzilishi wa kanisa la Sinagogi, Kanisa la mataifa yote (SCOAN), Muhubiri mashuhuri nchini Nigeria.

Maelfu ya watu hufika makao makuu ya kanisa hilo kutoka ulimwenguni kote kufuata miujiza na kushuhudia shuhuda mbalimbali.

''Sababu ilifanya twende kumuona tumeona nguvu ya wizara ya wanawake, serikali ya Nigeria na watu wengine wengi, mpaka sasa hakuna taarifa yeyote kuhusu wasichana,'' alisema Yana Galang, mmoja kati ya wazazi 12 waliofika katika kanisa la SCOAN na ambaye binti yake Rifkatu anashikiliwa mpaka sasa.

''Hakuna anyetuambia habari zozote kuhusu wasichana.Ndio maana tumefika kukabidhi jambo hili kwa Mungu.''

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wasichana walichukuliwa kutoka shule ya bweni ya Dapchi, jimbo la Yobe, Mwezi Februari

Miongoni mwa waliokuwa kwenye safari ni mlezi wa Leah Sharibu, binti wa miaka 14 ambaye mwezi februari mwaka 2018 alichukuliwa na wanamgambo akiwa na wasichana wengine zaidi ya 100 kutoka kwenye shule nyingine-hii Kaskazini -Mashariki mji wa Dapchi.

Baadhi ya wasichana wa Dapchi walipoteza maisha wakiwa kwenye safari na Boko Haram wengine wakirejeshwa mwezi mmoja baadae baada ya mazungumzo kati ya Boko Haram na Serikali ya Nigeria.Lakini Leah alibaki nyuma kwa kuwa alikataa kubadili dini.

Pamoja na ahadi ya Serikali kuhusu kuachiwa kwake, alitumia kumbukumbu yake ya miaka 15 ya kuzaliwa akiwa ameshikiliwa.Wazazi wake wote wako na hali mbaya kiafya, hivyo walimtuma ndugu yao wa karibu awawakilishe wanapokutana na TB Joshua.

Msemaji wa Rais Muhammadu Buhari, Garba Shehu amesema jitihada zinaendelea kuhakikisha wasichana waliobaki wanaachiwa.

Mada zinazohusiana