Marekebisho ya katiba huenda ikamwezesha rais al-Sisi kuongoza hadi mwaka 2030

Bango la picha ya Abdul Fattah al-Sisi

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Bango la picha ya Abdul Fattah al-Sisi

Bunge nchini Misri limeidhinisha marekebisho ya Katiba itakayomwezesha Rais Abdul Fattah al-Sisi kusalia madarakani hadi mwaka 2030.

Bw. Sisi anatarajiwa kuondoka madarakani mwaka 2022, wakati muhula wake wa pili wa miaka minne utakapokamilika.

Lakini marekebisho hayo, ambayo lazima yapigiwe kura ya maoni katika siku 30 zijazo, yatarefusha muhula wake wa sasa kwa miaka sita na kumruhusu kugombea tena urais mara nyingine tena.

Marekebisho hayo pia yatampatia mamlaka zaidi dhidi ya idara ya mahakama na vile vile kujumuisha majukumu ya kijeshi katika siasa.

Mwaka 2013, Bw. Sisi aliongoza mapinduzi ya kijeshi dhidi ya rais wa kwanza wa Misri aliyechaguliwa kidemokrasia, Mohammed Morsi, kufuatia maandamano ya kupinga utawala wake.

Tangu wakati huo ameongoza kile ambacho wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wanasema ni msako mkali dhidi ya wapinzani wake yaliyosababisha maelfu ya watu kuwekwa kizuizini.

Bw. Sisi alichaguliwa mara yakwanza kuwa rais mwaka 2014 na alichaguliwa tena mwaka jana baada ya kupata 97% ya kura zilizopigwa.

Hakukabiliwa na ushindani mkali kwasababu baadhi ya washindani wake walijiondoa katika kinyang'anyiro cha kugombea urais au walikamatwa.

Bunge pia limesheheni wafuasi wa Bw Sisi na limelaumiwa na upinzani kwa kutumiwa vibaya na rais kupitisha ajenda zake.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Wafuasi wa Bw. Sisi wanasema kuwa mabadiliko hayo ni muhimu na wanataka kumpatia muda zaidi ili yatekelezwe

Mohammed Abu Hamed, mmoja wa wabunge wanaounga mkono marekebisho ya katiba, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba Bw. Sisi ni rais muhimu ambaye "anatilia maanani masuala ya kisiasa, kiuchumi na usalama " na ndio maana tumemruhusi "aendelee mbile na ajenda yake ya mageuzi" tukizingatia mzozo wa kisiasa unaokumba mataifa jirani ya Libya na Sudan.

Lakini mbunge wa cham cha kiliberali cha al-Dustour,Khaled Dawoud, amepuuzilia mbali maoni hayo aliyotaja kuwa ya "kustaajabisha" na kuambia BBC kuwa mabadiliko hayo yanaashiria "unyakuzi wa madaraka" wa Bw. Sisi.

Rais atasalia vipi madarakani hadi mwaka 2030?

Kifungu cha 140 cha katiba ya sasa ya Misri ambayo iliidhinishwa kupitia kura ya maoni mwaka 2014, kinasema rais ataongoza kwa muhula wa miaka minne na anaweza kuchaguliwa tena mara moja muda huo ukikamilia.

Chini ya marekebisho yaliyoidhinishwa na bunge siku ya Jumanne, muhula wa uongozi wa rais utakuwa wa miaka sita

Makubaliano ya kipindi cha mpito kama ilivyokaririwa katika kifungu cha 241 cha katiba kitarefusha muhula wa sasa wa uongozi wake kwa miaka miwili na kuuongezea muhula mwingine mmoja wa miaka sita ifikapo mwaka 2024.

Rais pia atapewa idhini ya kumteua naibu wake wake mmoja au zaidi. Wadhifa ambao ulitolewa baada ya katba ya mwaka kuidhinishwa kwa katiba ya mwaka 2012.

Jukumu la jeshi litakua lipi?

Majukumu ya jeshi katika masuala ya kiucumi na na ya kiraia yaliongezeka tangu Bw. Sisi alipokua rais.

Jeshi linasimamia miradi yote ya miundo mbinu, na pia kushikilia nyadhifa katika idara mbali mbali za serikali.

Kifungu nambari 200 kitabadilishwa ili iongeze majukumu kama ya kulinda nchi na kulinda "katiba na demokrasia, kudumisha msingi wa taifa kwa kuhakikisha haki ya raia na uhuru wao unaheshimiwa".

Sheria nyingine itakayofanyiwa marekebisho iko katika kifungo cha 234cha katiba ambayo pia inalenga kuimarisha jukumu la jeshi.

Idara ya mahakama itaathiriwa vipi na marekebisho hayo?

Kufanyiwa marekebisho vifungo nambari 185, 189 na 193 kutampatia mamlaka rais wa Misri ya kuwateua wakuu wa mahakama muhimu nchini ikiwa ni pamoja na uteuzi wa jaji wa mahakama ya juu zaid na waendesha mashtaka wote wa umma

Shirika la kutetea haki la Amnesty International linasema hatua hiyo itahujumu uhuru wa idara ya mahakama.

Je bunge nalo litabadilika pia?

Sheria mpya zitakazobuniwa itazindua tenna bunge la juu ambalo lilifutiliwa mbali mwaka 2014.

Rais atateua thuluthi moja ya wabunge 180 katika bunge hilo jipya ambalo litafahamika kama bunge la Seneti huku wengine wakichaguliwa

Idadi ya viti katika bunge la chini na bunge la wakilishi vitapunguzwa kutoka 596 hadi 450, huku angalau 25% ya viti hivyo vikitengewa wanawake.