Wakunga wa jadi wawazalisha wanawake kwa kutumia 'mifuko ya rambo' Tanzania

mtoto mchanga

Barani Afrika matatizo ya uzazi kwa wanawake ni suala lenye changamoto kubwa hususan katika maeneo ya vijijini, ambapo umbali na vituo vya Afya husubabisha wanawake kujifungulia nyumbani.

Kwa mujibu wa shirika la Afya Duniani WHO, zaidi ya 60% ya wanawake wanaojifungua vijijini nchini Tanzania hukosa usaidizi wa wataalamu.

Huko Mkoani Tabora wanawake wanazalishwa na wakunga wa Jadi kwa kutumia mifuko ya rambo, Jambo ambalo si salama kiafya.

BBC ilitembelea wilaya ya Sikonge ambayo ni umbali wa takriban masaa mawili kutoka Tabora mjini kutathmini hali ya kinamama wanaotafuta huduma ya wakunga wa jadi.

Katika baadhi ya vijiji wilayani humo hakuna vituo vya afya hali ambayo huwalazimu wakunga wa jadi kuwazalisha kinamama nyumbani na kisha baadhi yao huenda hospitali baada ya hapo.

Chanzo cha picha, AFP

''Natumia mifuko ya rambo kufunga mikono wakati namhudumia mama mjamzito baada ya kushindikana usafiri, lakini kama kuna uwezekano wa kumpeleka hospitali basi tunampeleka'' asema Asha Ibrahim mmoja wa wakunga wa jadi.

Bi Asha ambaye ameshawasaidia wajawazito wanane anaongeza kuwa baadhi ya wanawake hao wakati mwingine huja wakiwa wamejiandaa kabisa.

''Kama hawajajiandaa basi tunafunga mikononi mifuko ya rambo na kuwasaidia''

Kiafya jambo hili linaweza kuongeza hatari ya maambukizi ya magonjwa kutoka kwa mama anaejifungua na mtu anaemsaidia.

Lakini suala hili la utumiaji mifuko ya plastiki linashughulikiwa namna gani na wahudumu wa afya?

''Kama mkunga atatumia mifiko ya rambo ambayo si misafi basi ni wazi huenda ikaleta mambukizi kwa mama'' anasema Daktari Baguma kutoka hospitali ya mkoa wa Tabora kitengo cha wazazi na magonjwa ya kinamama.

Dkt Baguma anaongeza kuwa changamoto wanazopitia kinamama wajawazito ni kuwa mji wa Tabora uko mbali na kitu chocho kinaweza kutokea hapa katikati.

Wazara ya afya nchini Tanzania ilipiga marufuku wakunga wa jadi kuwazalisha wanawake nyumbani lakini kutokana na matatizo ya usafiri na uhaba wa vituo vya afya vijijini, ni wakunga hao ndio wamekua wakombozi wa wanawake na watoto wanaozaliwa.