WHO: Visa vya surua vimeongezeka mara tatu duniani mwaka 2019

The World Health Organization says the latest figures paint "an alarming picture" Haki miliki ya picha PIUS UTOMI EKPEI
Image caption Shirika la afya duniani linasema takwimu za sasa zinadhihirisha "picha ya kushtusha".

Visa vya ugonjwa wa surua vilivyoripotiwa kote duniani katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka 2019 vimeongezeka mara tatu ikilinganishwa na hali ilivyokuwa wakati kama huu mwaka jana kwa mujibu wa shirika la afya duniani (WHO).

Shirika hilo la Umoja wa mataifa linasema data ya awali imeashiria 'mkondo wa wazi', wa maeneo yote duniani yanayoshuhudia mlipuko wa ugonjwa huo.

Afrika imeshuhudia viwango vya juu vya visa vya ugonjwa huu - kwa 700%.

Shirika hilo limesema huenda takwimu halisi zikawa juu zaidi kutokana na kwamba ni kisa kimoja kati ya 10 kinachoripotiwa.

Surua au ukambi ni ugonjwa ambao ni wa maambukizi ambayo kwa mara nyingine unaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiafya, ikiwemo maambukizi kwenye mapafu na ubongo.

Ukraine, Madagascar na India ndio mataifa yalioathirika pakubwa na ugonjwa huo, huku maelfu ya visa vingine vikishuhudiwa kati ya mamilioni ya watu.

Tangu Septemba, watu 800 wamefariki kutokana na surua huko Madagascar pekee.

Kumehsuhudia mlipuko wa ugonjwa huo huko Brazil, Pakistan na Yemen, "uliosababisha vifo vya watu wengi - hususan kwa watoto wadogo".

Haki miliki ya picha SEYLLOU

Kuongezeka kwa visa pia kumeshuhudia katika nchi kama Marekani na Thailand huku kukitolea chanjo ya kiasi kikubwa.

Umoja wa mataifa unasema ugonjwa huo unaweza 'kuzuilika kikamilifu' kwa kutumia chanjo sahihi, lakini chanjo iliotolewa duniani katika awamu ya kwanza imekwama katika kiwango cha 85%, "chini ya kiwango kinachotakiwa cha 95% kuzuia milipuko ya ugonjwa huo".

Katika uhariri ulioandikwa katika CNN, wakuu wa WHO, Henrietta Fore na Tedros Adhanom Ghebreyesus wamesema ulimwengu upo "katikati ya janga la surua" na kwamba "kukithiri kwa taarifa za kuchanganya na kupinga chanjo ndio sehemu ya chanzo cha kushuhudiwa hali iliopo.

Kwanini kunashuhudiwa 'janga la ghafla la surua duniani'?

Ni mojawapo ya virusi vinavyoambukiza pakubwa, hatahivyo hakuna kilichobadilika kuhusu ugonjwa wa surua. Sio kwamba umegeuka kuwa hatari zaidi, badala yake majibu yote yanatokana na hatua ya binaadamu.

Kuna hadithi mbili hapa - moja kuhusu umaskini na nyingine kuhusu kusambaa kwa taarifa za uongo. Katika mataifa ya kimaskini watu wachache wanapewa chanjo na sehemu kubwa ya watu wanaachwa katika hatari ya kuugua ugonjwa huo.

Hii hutoa nafasi ya kushuhudiwa mlipuko mkubwa kama ilivyoshuhudiwa katika Jamhuri ya Kidmeokrasi ya Congo, Kyrgyzstan na Madagascar.

Lakini mataifa yalio na viwango vikubwa vya utoaji chanjo vinashuhudia kuongezeka kwa ugonjwa huu. Na hii ni kutokana na kwamba baadhi ya watu wanaamua kutowapeleka watoto wapewe chanjo kutokana na kusambaa kwa taarifa za uongo katika mitandao ya kijamii dhidi ya chanjo hizo.

Ni muhimu kutambua kwamba takwimu hizi ni za awali, shirika la afya duniani linasema takwimu halisi zitakuwa juu zaidi. Na kwamba surua au ukambi ni tishio. Husababisha vifo vya takriban watu laki moja, wengi wao watoto kila mwaka.

Haki miliki ya picha MAMYRAEL

Wakuu hao wa WHO wameandika kwamba "inaeleweka, katika mazingira hayo wazazi wanaweza kupotea" lakini kwamba "mwisho wa kwisha faida za chanjo hiyo hazina mjadala".

Wameongeza: "Maisha ya zaidi ya watu milioni 20 yameokolewa kwa chanjo ya surua tangu mwaka 2000 pekee yake."

Dalili za surua

  • Kuhisi baridi na kupiga chafya
  • Homa kali,uchovu,kukosa hamu ya kula na misuli kuuma
  • Macho kuwa na rangi nyekundu na majimaji kama unataka kulia
  • Kuwa na rangi ya kijivu mdomoni
  • Kuwa na vipele vyenye rangi nyekundu ambavyo vinaweza kusambaa kutoka kwenye kichwa,shingoni mpaka kwenye mwili wote.

Kutokana na mlipuko wa hivi karibuni wa surua, kumetolewa wito katika mataifa tofuati duniani kuhakikisha kwamba watoto wanapewa chanjo kwa lazima.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii