Umoja wa Afrika watoa makataa kwa serikali ya kijeshi nchini Sudan

Jeshi lilimuondoa madarakani kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir Haki miliki ya picha Getty Images

Umoja wa bara Afrika umetishia kuipiga marufuku Sudan kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliomuondoa madarakani Omar al-Bashir baada ya takriban miongo mitatu madarakani.

Iwapo Jeshi hilo litashindwa kuwakabidhi raia uongozi katika kipindi cha siku 15 , AU itasitisha uwakilishi wa Sudan katika maswala yote ya AU hadi pale katiba itakapofuatwa, ilisema body ya amani na usalama ya umoja huo PSC katika taarifa yake.

Bashir aliiongoza Sudan kiimla kwa takriban miaka 30 kabla ya kung'atuliwa wiki iliopita kufuatia maandamano makubwa ambayo yamelikumba taifa hil tangu mwezi Disemba.

Maandamano hayo yamesalia katika barabara , huku raia wakitaka utawala wa kiraia kutoka kwa baraza la kijeshi ambalo lilimuondoa Bashir.

AU imeunga wito wa waandamanaji ikisema yaliofanyika ni mapinduzi ambayo Umoja huo unashutumu. Umoja huo ambao unashirikisha wanachama 55, uliongezea kwamba serikali ya mpito ya kijeshi ni kinyume na matakwa ya raia wa Sudan.

AU inachukua msimamo mkali dhidi ya mapinduzi na iliipiga marufuku Misri, na jamhuri ya Afrika ya kati CAR mwaka 2013 kufuatia mapinduzi katika mataifa yote mawili.

Hatahivyo uanachama wa mataifa yote mawili umerejeshwa.

Mkutano na waziri mkuu wa Ethiopia

Makataa hayo yanajiri muda mchache baada ya waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kuwa kiongozi wa kwanza wa kigeni kukutana na wanachama wa baraza hilo la kijeshi la Sudan.

Jenerali Galaledin Alsheikh aliongoza ujumbe wake hadi mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa siku ya Jumatatu ili kumjuza bwana Abiy kuhusu hatua zilizopigwa nchini Sudan kufuatia kupinduliwa kwa rais Omar al-Bashir, kulingana na ofisi hiyo ya waziri mkuu.

Haki miliki ya picha EPA

Watawala hao wa kijeshi waliitaka Ethiopia kuendelea kuiunga mkono Sudan huku bwana Abiey akiwataka kuangazia malalamishi na wasiwasi wakati ambapo Sudan inatarajiwa kuwa na kipindi cha amani cha mpito, ofisi hiyo ya waziri mkuu iliongezea katika taarifa iliochapishwa katika mtandao wa facebook.

Wakati huohuo Mwenyekiti wa umoja huo amewataka wale wote wanaohusika katika swala hilo kuwa watulivu, kuheshimu haki za raia, zile za raia wa kigeni na mali ya kibinafsi kwa niaba ya taifa hilo na raia wake.

Vilevile Umoja huo umewataka washikadau kuanzisha mazungumzo yatakayoshirikisha watu wote ili kuleta hali ambayo itawezesha kuafikia mahitaji ya kidemokrasi ya raia wa Sudan, utawala bora mbali na kuheshimiwa kwa katiba mara moja.

Baraza hilo tayari limewakamata baadhi ya waliokuwa maafisa wa serikali ya Bashir na kuahidi kutowatawanya waandamanaji.

Haki miliki ya picha AFP/getty

Msemaji mmoja pia ameuomba upinzani kumchagua waziri mkuu mpya na kuahidi kumuidhinisha watakayemchagua.

Waandamanaji wameapa kusalia mitaani hadi itakapoundwa serikali ya kiraia

Raia wanaendelea kuandamana na wamekita kambi nje ya makao makuu ya wizara ya ulinzi katika mji mkuu Khartoum.

Je baraza la kijeshi limesema nini?

Katika mkutano na waandishi habari siku ya Jumapili, msemaji Meja Jenerali Shams Ad-din Shanto ameeleza kwamba baraza la kijeshi lipo "tayari kuidhinisha" serikali yoyote ya kiraia itakayoidhinishwa na vyama vya upinzani.

"Hatutomteua waziri mkuu. Watamchagua," alisema akimaanisha upinzani na makundi yanayoandamana.

Ameeleza pia kwamba jeshi halitowaondoa waaandamanaji kwa lazima lakini ametoa wito kwa waandamanaji hao "kuruhusu maisha yaendelee kama kawaida" na waache kuweka vizuzi kinyume cha sheria.

"Kushika silaha hakutoruhusiwa," aliongeza

Maamuzi ya baraza la Kijeshi

  • Viongozi wapya wa jeshi na polisi
  • Mkuu mpya wa kitengo cha ujasusi (NISS)
  • Kamati za kupambana na rushwa na kuchunguza chama tawala kilichoondoka
  • Kuondolewa kwa marufuku zote na kubanwa kwa vyombo vya habari
  • Kuachiwa kwa maafisa wa polisi na jeshi waliozuiwa kwa kuungamkono waandamanaji.
  • Ukaguzi wa wajumbe wa kidiplomasia, na hatua ya kutimuliwa kwa balozi wa Sudan nchini Marekani na Uswizi.

Maandamano ya kupinga kupanda gharama ya maisha yalianza Desemba mwaka jana lakini punde tu yakageuka kuwa wito mkubwa wa kumpinga rais Bashir na utawala wake.

Aliyeongoza mapinduzi hayo, waziri wa ulinzi Awad Ibn Auf, alitangaza kwamba jeshi litasimamia serikali ya mpito kwa kipindi cha miaka miwili kitakachofuatwa kwa uchaguzi na akaidhinisha miezi mitatu ya hali ya dharura.

Lakini wandamanji waliapa kusalia mitaani hata baada ya hatua hiyo, wakitaka maguezi na kuidhinishwa kwa serikali ya kiraia mara moja.

Ibn Auf alijiuzuliu siku ya pili , kama alivyojiuzulu mkuu wa usalama anayeogopwa na wengi Jenerali Salah Gosh.

Luteni Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman Burhan baada ya hapo alitajwa kuwa kiongozi wa baraza la mpito la kijeshi, kuwa kiongozi wa tatu kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha siku nyingi.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii