Vyama vya kisiasa Tanzania: Serikali yapelekwa katika mahakama ya Afrika Mashariki EACJ

Viongozi wa vyama vya upinzani Tanzania Haki miliki ya picha CHADEMA

Vyama vinne vya upinzani nchini Tanzania vimeishtaki serikali katika mahakama ya Afrika mashariki kuhusu haki EACJ kufuatia mabadiliko ya hivi majuzi ya sheria ya vyama vya kisiasa.

Sheria hiyo ambayo ilitiwa saini na rais John Pombe Magufuli mwezi Februari na kuchapishwa katika gazeti la serikali siku 10 baadaye imezua mjadala mkubwa nchini humo.

Akizungumza jijini Dar es salaam kwa niaba ya vyama vinne vya kisiasa, mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo{Chadema} Freeman Mbowe amesema kuwa malalamishi hayo yamesajiliwa na mahakama ya EACJ.

Matamshi yake yanajiri siku chache tu baada waziri kivuli wa mambo ya kigeni nchini Uingereza Liz Mclinnes kuelezea kusikitishwa kwake na kupitishwa kwa sheria ya vyama vya kisiasa nchini Tanzania ambayo anadai inaminya vyama vya upinzani.

Liz McInnes ambaye ni mbunge kupitia chama cha upinzani cha Labour amekaririwa na mtandao wa chama chake akisema wapinzani inabidi waachiwe uhuru wao.

Mwanasiasa huyo ametahadharisha kuwa matendo ya serikali ya Tanzania yana athari mbaya kwa uchumi wa taifa hilo.

Malengo ya kesi hiyo

Lengo la kesi hiyo kulingana na Mbowe ni kwamba sheria hiyo mpya iliiwekwa kupitia kubadili na kuongeza baadhi ya vifungu ambavyo vinakiuka lengo la kuanzisha ushirikiano wa jumuiya ya Afrika mashariki.

''Kwanza tunapinga sheria yote mpya na tunaisihi EACJ kusitisha uidhinishwaji wa sheria hii hadi kesi hii itakaposikizwa'', alisema Mbowe.

Alisema kuwa sheria hiyo inakandamiza demokrasia nchini Tanzania swala ambalo ni kinyume na itifaki ya uanzishaji wa Jumuiya ya Afrika mashariki na kwamba ilipitishwa kimabavu licha ya malalmishi kutoka kwa washikadau wa kisiasa.

''Mbali na kukiuka haki za kibinaadamu, sheria hiyo pia ni kinyume na katiba ya Tanzania ya 1977 mbali na maadili ya uongozi na azimio la kimataifa ambalo Tanzania ni mwanachama'', alisema.

Ameongezea kwamba wameamua kuanzisha kesi hiyo katika mahakama ya EACJ kutokana na muda mchache uliopo kuianzisha katika mahakama za nchini lakini akaongezea kwamba baada ya kesi hiyo watafungua nyengine katika mahakama ya nchini.

Malalamishi ya vyama vya kisiasa

Sheria mpya ya Vyama vya kisiasa imekumbana na upinzani mkali toka muswada wake ulipowasilishwa kwa mara ya kwanza Bungeni.

Vyama vya upinzani na asasi za kirai vimekuwa vikilalamikia sheria hiyo wakidai inafanya shughuli za siasa kuwa kosa la jinai.

Haki miliki ya picha Getty Images

Bunge lilipitisha muswada huo mwezi Januari na hatimaye kusainiwa kuwa sheria na rais Magufuli.

Wakati wa kupitishwa kwake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama alilieleza Bunge kuwa muswada huo ni kiboko.

"Lengo ni kuhakikisha chama cha siasa kinakuwa na sifa za usajili muda wote wa uhai wake na kueleza bayana mamlaka ya msajili wa vyama vya siasa kuhakiki muda wowote utekelezaji wa sheria ya vyama vya siasa ili kuhakikisha chama cha siasa kinazingatia na kutekeleza masharti ya usajili," amenukuliwa na Mwananchi akisema.

Toka kuingia madarakani rais John Magufuli amekuwa akilaumiwa kwa kuminya demokrasia nchini Tanzania. Pia analaumiwa kwa kuminya uhuru wa habari na kujieleza.

Baadhi ya yale yanayolalamikiwa kwenye sheria hiyo ni pamoja na msajili wa vyama vya siasa kupewa mamlaka ya kuingilia mfumo wa uchaguzi ndani ya vyama.

Haki miliki ya picha BUNGE

Malalamiko mengine ya uonevu kwa mujibu wa upinzani ni masharti ya namna ya utoaji wa elimu ya uraia kwa kuzuia vyama rafiki kutoka nje kushiriki.

Moja ya kifungu kinachopingwa ni cha Kifungu cha 19 ambacho kinasema msajili anaweza kukisimamisha usajili wa chama kwa sababu atakazozitaja na kwa muda atakaouweka mpaka ili chama hicho kiweze kujirekebisha.

Chama ambacho kimesimamishiwa usajili hakitaweza kufanya shughuli zote za kisiasa.

Na iwapo msajili ataona chama hicho hakijajirekebisha anaweza kukifutia usajili.

Kifungu hiki, wapinzani wanadai kinaweza kutumika kuzuia vyama kushiriki uchaguzi kwa jusimamishiwa usajili kabla yay a uchaguzi na kurudishiwa usajili baada ya uchaguzi kupita.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii