Miaka 25 ya mauaji ya Kimbari Rwanda: Jean Claude aomba radhi baada ya kuua watu wengi

Jean Claude
Image caption Jean Claude Ntambara amekiri kuua idadi kubwa ya watu

Katika kumbukumbu ya miaka 25 ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda, serikali ya nchi hiyo imesema imelipa kipaumbele swala la umoja na maridhiano miongoni mwa wananchi wake ambapo waliotekeleza mauaji na kuomba msamaha waliachiwa huru.

Miongoni mwao ni Jean Claude Ntambara ambaye yeye binafsi amekiri kuua idadi kubwa ya watu. Aliachiwa huru na sasa anaomba msamaha kila mpita njia kwa kutojua alimkosea nani. Mwandishi wa BBC, Yves Bucyana alikutana naye na kumuelezea masaibu yake.

Ni katika kijiji cha Bugesera, si mbali na mpaka wa Burundi,ni miongoni mwa vijiji vilivyoshuhudia mauaji ya kupindukia dhidi ya watutsi mwaka 1994 nchini Rwanda.

Hapa ndipo nilimkuta Bwana Jean Claude Ntambara akiwa nyumbani kwake: ''Nakumbuka kwamba baada ya taarifa kwamba ndege ya aliyekuwa rais Habyarimana kuanguka wananchi wengi wa kabila la watutsi walikimbilia baadhi katika ofisi ya wilaya,wengine makanisani. Amri ilitolewa kutoka kwa wakubwa zetu tukazingira wananchi hao sehemu walikojificha na kuanza kufyatua risasi. Kwa kuwa walikuwa wengi tulitumia hata guruneti.Binafsi siwezi kujua niliuwa watu wangapi,bunduki niliyokuwa nayo ilikuwa ya risasi 10 lakini zikiisha nilikuwa naweza zingine, ukweli ni kwamba niliuwa watu wengi.''

Yeye alikuwa afisa wa polisi kabla na wakati wa mauaji ya kimbari, lakini anasema mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi yaliandaliwa mapema kiasi kwamba mwaka 92 eneo hilo kulitokea kile alichokitaja kama jaribio la mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waombolezaji wakiadhimisha kumbukumbu ya miaka 25 ya mauaji ya kimbari, kwenye uwanja wa Amahoro

''Tulianza kufundishwa chuki dhidi ya watutsi tangu zamani. Binafsi majirani zangu wote walikuwa watutsi na sikuwa na chuki dhidi yao,lakini viongozi wa wakati huo walianza kutufundisha kuchukiamajirani zetu. Nakumbuka kwamba mwaka 1992 hata kabla ya mauaji ya kimbari yenyewe tuliombwa kufanya majaribio. Watutsi wengi waliuawa ,nyumba zao zikachomwa moto. Wakati huo nilikuwa afisa wa polisi lakini mimi na viongozi wengine tulisimamia mauaji hayo ilihali tulikuwa na uwezo wa kuyazuia.''

Kutokana na idadi kubwa ya wahutu walioshiriki mauaji ya kimbari serikali ilianzisha mfumo wa mahakama za jadi maarufu Gacaca mwaka 2002 zilizowahukumu watu wengi. Lengo kubwa likiwa ni kusaka maridhiano kwa kutumia mkondo wa sheria. Utaratibu ulivyokuwa ni kwamba waliokiri na kusema ukweli kuhusu mauaji waliyofanya walisamehewa na adhabu zao kupunguzwa, Jean Claude Ntambara alikuwa miongoni mwao.

''Baada ya mauaji ya kimbari nilikimbilia Jamuhuri ya kidemokrasi ya Congo nikarejea nchini mwaka 2002. Nilikiri kwamba nilishiriki mauaji dhidi ya watutsi na kuomba msamaha. Nilipunguziwa adhabu nikahukumiwa kifungo cha miaka 14 lakini pia adhabu hiyo ilipunguzwa hadi miaka 7 nikifanyakazi zenye faida kwa taifa.Mambo niliyoyafanya hayawezi kusamehewa na mpaka sasa naendelea kuomba msamaha hasa sehemu zote zenye mikusanyiko ya watu na kila mpita njia kwani nilikosea watu wengi.''alieleza Ntambara.

Alipozindua juma la kumbukumbu ya miaka 25 ya mauaji ya kimbari, Rais Paul Kagame alipongeza manusura wa mauaji ya kimbari kuchangia pakubwa katika juhudi za serikali za maridhiano kwa kutoa msamaha wa dhati kwa wahusika wa mauaji ya kimbari.