Ajali DR Congo: Watu 150 hawajulikani waliko baada ya boti kuzama Ziwa Kivu

Watu wanaoabiri boti

Takriban watu 150 wametoweka baada ya boti waliokuwa wakiabiri kuzama katika ziwa moja mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

''Nimehuzunishwa na kuzama kwa boti hiyo tarehe 15 mwezi Aprili katika ziwa Kivu. Hadi kufikia sasa idadi ya watu ambao hawajulikani waliko ni 150'' , alisema rais wa taifa hilo Felix Tshisekedi katika akaunti yake ya Twitter.

Kulingana na mwanaharakati mmoja katika eneo la Kivu kusini ambaye alikuwa akizungumza na shirika la habari la Reuters, boti hilo ambalo lilikuwa limetoka katika mkoa jirani wa Kivu kaskazini lilizama katika ziwa hilo karibu na eneo la Kalehe.

Alisema kuwa miili mitatu iliopolewa , watu 33 wakaokolewa huku abiria wengine 150 wakiwa hawajulikani waliko kufuatia ajali hiyo.

Tshisekedi amesema kuwa anaifuatilia kwa karibu hali hiyo ili kuwatambua na kuwachukulia hatua wale waliohusika.

Mikasa mibaya ya ajali ya maboti ni swala la kawaida nchini DR Congo, taifa lenye msitu mkubwa na ambalo lina barabara chache nje ya miji mikuu ambapo boti hubeba watu wengi kupitia kiasi.

Ajali za maboti DR Congo

Kulingana na Reuters mwaka uliopita , boti moja lilipinduka katika mto kaskazini mwa DR Congo , na kusababisha watu 49 kufa maji huku idadi kama hiyo ya watu wakiokolewa.

Richard Mboyo Liuka, naibu gavana wa mkoa wa mashambani wa Tshupa, kaskazini mwa Congo aliambia radio Top Congo kwamba boti hilo lilizama na abiria wote jioni siku ya jumatano.

Mwaka wa 2015, zaidi ya watu 100 walitoweka baada ya maboti mawili kugongana katika mto Congo nchini DR Congo kulingana na shirika la afya duniani WHO.

Eugene kabambi , msemaji wa WHO katika mji mkuu wa Kinshasa, alisema kuwa boti hilo lilipinduka karibu na mji wa Kwamouth wakati boti lililokuwa limejaa kupitia kiasi lililokuwa likielekea eneo la Inongo lilipogongana na boti moja lililokuwa likiwabeba watu 150.

Mnamo mwezi Julai 2011, zaidi ya watu 100 walifariki baada ya boti mbili kugongana katika mto katika eneo la mkoa wa Equateur la DR Congo.

Miezi miwili awali, aliyekuwa rais wa taifa hilo Joseph Kabila alikua amemfuta kazi waziri wake wa uchukuzi kufuatia visa vya msururu wa ajali za maboti ambavyo viliwaua zaidi ya watu 100.