Ukosefu wa mvua wahofiwa kusababisha uhaba wa chakula na maji Tanzania na Kenya

Mkulima Consolata akikagua mavuno yake karibu na Kibiti wilayani Rufiji eneo la pwani Tanzania

Chanzo cha picha, Majority World

Maelezo ya picha,

Mkulima Consolata akikagua mavuno yake karibu na Kibiti wilayani Rufiji eneo la pwani Tanzania

Huenda Tanzania na Kenya zikaathirika na uhaba wa chakula na maji kutokana na kukosekana msimu wa mvua.

Mvua za masika ambazo kwa kawaida huanza kunyesha kati ya Machi na Mei hazikujiri kwa ukubwa na wakati kama ilivyotarajiwa idara ya hali ya hewa Kenya inasema.

Huenda Kenya ikazidi kuathirika na uhaba wa chakula na maji wakati mvua hiyo inazidi kuchelewa idara hiyo imeeleza siku ya Jumanne.

Kadhalika nchini Tanzania hali hiyo ya kutonyesha mvua kwa wakati muafaka, ina hofiwa kuisababisha nchi kuingia katika kipindi cha ukosefu wa chakula katika kipindi cha miezi sita ijayo, gazeti la Mwananchi limemnukuu Spika wa bunge nchini humo Job Ndugai akisema.

Katika mkutano kuhusu uwepo wa chakula cha kutosha uliowakutanisha wabunge kutoka nchi 10 za Afrika mashariki mjini Arusha, Ndugai ameeleza kwamba hali ya hewa inayoshuhudiwa sasa inayotokana na mabadiliko ya tabia nchi inatia wasiwasi kuhusu namna mataifa yatakavyoweza kuitikia na kukabiliana na changamoto hiyo, linaripoti Mwanachi.

Mvua ndefu hunyesha miezi ya Machi, Aprili na Mei, na nchini Kenya hushuhudiwa sana katika eneo la magharibi, na mkoa wa kati na ni muhimu sana katika sekta ya kilimo.

Chanzo cha picha, FACEBOOK/ KENYA METEOROLOGICAL DEPARTMENT

Idara ya hali ya hewa nchini sasa imewashauri wakulima kupanda mimea inayokuwa kwa haraka na ile isiotegemea maji kwa kuwa mvua hiyo huenda isinyeshe kwa muda mrefu iwapo itakuja.

"Kutokana na hali inayoshuhuidwa na hali ya hewa inayotabiriwa, kunatarajiwa kuwa na ukavu katika maeneo mengi nchini na kuchangia hali kuzidi kuwa mbaya katika kuwepo chakula cha kutosha na maji," Stella Aura, mkurugenzi wa idaraya utabiri wa hali ya hewa kenya amesema.

Awali idara ya hali ya hewa Kenya iliarifu kwamba mvua nchini Kenya imekwama Tanzania, kutokana na kwamba mifumo ya upepo iliopo kusini haijashikamana kuweza kusukuma mawingu hivyobasi mvua itachelewa.

Patrick Njoroge, Gavana wa benki kuu nchini amesema huenda benki hiyo ikashusha utabiri wa ukuwaji wa uchumi wake kwa mwaka huu hadi 5.3% kutoka asilimia 6.3 iwapo hali ya ukame itakithiri.

Benki kuu nchini Kenya imesema katika ujumbe kwenye mtandao wa Twitter ikinukuu mahojiano ya Gavana huyo na Televisheni ya Bloomberg Marekani.

Kwa upande wake Benki ya Dunia imepunguza utabiri wake wa ukuwaji wa uchumi Kenya kwa 0.1% kutokana na kukosekana na mvua nchini, linaripoti shirika la habari la Reuters.

Chanzo cha picha, SIMON MAINA

Ukulima wa mazao yanayosafirishwa nje ikiwemo wa chai, maua na kahawa unachangia karibu thuluhi ya pato la uchumi kwa mwaka nchini.

Wataalamu wa hali ya hewa walionya kwamba athari ya kimbunga Idai kilichoshuhudiwa Msumbiji na Zimbabwe mwezi uliopita wa Machi zitashuhudiwa katika baadhi ya maeneo ya Afrika mashariki.

Athari mojawapo kwa mujibu wa Benard Chanzu, naibu mkurugenzi katika idara ya utabiri wa hali ya hewa Kenya ni kwa msimu wa mvua kwenye eneo la Afrika mashariki.

Maelezo ya sauti,

Mafuriko yadaiwa kuhatarisha maisha ya wakazi nchini Kenya

'Wakati kimbunga kimeelekea kikaja mpaka kikatua Msumbiji, kilitunyanganya upepo wote kutoka sehemu ya Afrika mashariki, kwa hivyo inanyang'anya uwezekano wa kuwepo mvua katika sehemu hii yetu' Chanzu ameilezea BBC.

Idara ya kutoa tahadhari ya mapema ya baa la njaa inayofadhiliwa na shirika la misaada Marekani USAID pia linalaumu ukosefu huo wa mvua ndefu Kenya kutokana na athari za kimbunga hicho Idai ambacho inasema kilibadili mkondo wa mvuke kutoka enoe la Afrika mashariki.