'Amashyuza': Maji ya 'ajabu' yanayotibu maumivu ya mgongo , mishipa

Mama akikandwa miguu
Maelezo ya picha,

Maji haya ni ya moto hutumika kama sehemu ya matibabu

Mji wa Bugarama upo Rwanda karibu na mpaka wa nchi hiyo na DRC na Burundi. Kuna sehemu inaitwa 'Amashyuza' yaani maji moto.

Ni eneo maarufu sana kwa raia wa kigeni na wenyeji wanaolitembelea ili kutumia maji hayo kama tiba. Watumiaji wanasema maji hayo husaidia kupunguza uchovu wa mwili na maradhi ya mishipa na maumivu ya mgongo. Mwandishi wa BBC Yves Bucyana alitembelea sehemu hiyo.

Sehemu hiyo inaitwa 'amashyuza' yaani maji ya moto.kuna chemchemi ya maji moto.watu kutoka sehemu mbali mbali kufika eneo hilo kutumia maji hayo kama sehemu ya matibabu, wengine wanakuwa na magonjwa mbali mbali kama mgongo na maradhi ya mishipa.

Mama Cluadine anasema: ''nilikuwa na ugonjwa wa mishipa ya miguu.ilikuwa inaniumiza sana lakini wakati wanamaliza kunikanda sasa najisikia salama kabisa. Kwa kipindi kirefu nilikuwa sikanyagi sawa sawa lakini sasa naweza kukanyaga''.

Kuna dimbwi la maji na watu wanaogelea humo ndani.Maji haya Unapoyasogelea sawa sawa utasikia yakitokota. Yamekuwa kivutio kikubwa si tu kwa wenyeji bali pia kwa wageni.

Maelezo ya picha,

Mzee Gatwabuyenge Bernard huwasaidia wagonjwa wa mishipa na mgongo

Wengine wanataoka Tanzania kama Velas Charles:''mimi ninaishi Tanzania.Hapa kuna maji mazuri ya tiba. Kama unajisikia unaumwa mkono au mgongo unakuja unapata yale maji.Hivi nilikuwa ninajihisi nina tatizo la mgongo,nimeenda pale nimeogeshwa yale maji na kunyooshwanyooshwa kwenye maji nikaenda nikakaa kwenye jiwe,hivi nasikia mgongo hauumi. Haya maji ni mazuri sana natamani yangekuwa Tanzania."

Kando kando ya kidimbwi baadhi ya watu wamekaa kimya kimya kwenye sehemu za miinuko midogo au kwenye mawe ambako hutokea mvuke unaowasaidia kuongeza joto mwilini mfano wa sauna.Wenyeji hapa wanasema ni kuchaji betri za mwili.

Mashuhuda wamesema kwamba mzee huyu alipoletwa kwa mara ya kwanza miaka 5 iliyopita alikuwa na ugonjwa wa mishipa na mgongo huku akibebwa kwa machela,sasa anaweza kutembea mwenyewe.

Maelezo ya picha,

Mzee Kalimwabo alikua anaumwa mishipa na mgongo hivi sasa amepona

''Unapotoka kwenye hii sehemu tunayoita sauna unakuja hapa ndani ya maji.Hapa naanza kazi ya kukukanda kanda na kukunyoosha mishipa.hospitali nyingi zinawatuma wagonjwa hapa ili niwahudumie''

Huyo ni mzee Gatwabuyenge Bernard anayetoa huduma kwa kila mtu anayehitaji kukandwakandwa na kunyooshwa mishipa.Hakusomea taaluma hiyo lakini nimeelezwa kwamba alipewa mafunzo maalum na wasamalia wema walioamini kazi anayoifanya.

Wataalamu wa maswala ya geolojia wamekuwa wakifanya tafiti kuchunguza kama eneo hili kuna mvuke wa kutosha kuweza kuzalisha umeme au pengine kuwekeza zaidi ili pawe sehemu ya utalii unaoingiza fedha.