Peter Tabichi: Hivi ndivyo mwalimu bora duniani anavyofundisha

Peter Tabichi

Chanzo cha picha, VARKEY FOUNDATION

Maelezo ya picha,

Peter Tabichi amesifiwa kama "mwalimu wa kipekee" ambaye hugawa sehemu kubwa ya mshahara wake

Ni mwezi mmoja tu umemalizika tangu mwalimu wa sayansi kutoka Kenya aliposhinda tuzo ya mwalimu bora duniani kutokana na kazi yake.

Peter Tabichi alituzwa dola milioni moja kwa kulea akili ya vizazi vijavyo na kukabiliana na tatizo la masomo duniani. Wiki hii, ameteuliwa kama ''bingwa wa watoto walio katika mazingira ya vita na migogoro' duniani.

Mwandishi wa BBC Victor Kenani alifunga safari hadi katika eneo la nakuru lililopo kwenye bonde la ufa, na hii simulizi yake:

Kiu yangu ilikuwa ni kufahamu ni kipi kinachomfanya mwalimu Tabichi kung'ara.

Nilipofika shuleni kwake nilipokewa na shamrashamra zilizopamba moto kwa nyimbo, ngoma na kelele za shangwe bingwa nyumbani - Peter Mokaya Tabichi alikuwa anapokelewa. ''Thabiti!! Thabiti!! ..." walisikika waalimu na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Keriko wakimshangilia shujaa wao.

Hii ni mara ya kwanza kwa mtawa huyu wa shirika la kikatoliki la Mtakatifu Fransisco wa kapuchini kurejea katika shule ya kutwa mseto ya Keriko ambapo anafundisha, baada ya kutunukiwa tuzo ya mwalimu bora duniani mjini Dubai.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Tabichi amepokelewa kama shujaa katika shule ambayo amekuwa akifunza

Amerudi kufanya kazi anayoifahamu vizuri nayo niya ualimu. Na mara baada ya mapokezi hayo alianza kufanya kile anachokipenda.

Hakujali jua kali...anaongoza wanafunzi wake jinsi ya kuwasilisha miradi waliyobuni kwenye mashindano ya kitaifa ya sayansi.

Tabichi, aliyesomea ualimu nchini Kenya, mfumo wa elimu wa nchi hii ambao aghalabu hugubikwa na migomo, ambayo huathiri masomo, anakiri kuwa mafunzo kwa njia ya kawaida hayana tija na alilazimika kubuni mbinu ambazo zingewahamasisha kupenda masomo.

''Natumia zana za kufundishia zinazopatikana hapa hapa. Njia nyingine ya kuhakikisha wanafunzi wanafurahia masomo ni kwa kujumuisha teknolojia. Zaidi ya asilimia themanini ya masomo, najumuisha teknolojia na kupitia hilo unapata kwamba wanafunzi wanafurahia masomo'', ananieleza Tabichi.

Tabichi amekuwa mwalimu kwa miaka kumi na hutoa sehemu kubwa ya mshahara wake kuwasaidia wanafunzi maskini kulipa karo za shule. Kujitolea kwake huku kumesaidia wanafunzi wengi kujiunga na chuo kikuu idadi hiyo ikiongezeka kutoka wanafunzi 16 mwaka 2017 na kufikia hadi hadi 26 mwaka jana.

Wanafunzi wake wanamwagia sifa tele kwa mbinu zake za kutoa mafunzo, wakisema amebadilisha namna wanavyokabiliana na masomo ya Fizikia na Hisabati anayoyafundisha: ''Ana hicho kipaji, anaweza kutambua wanafunzi ambao hawafanyi vizuri katika somo fulani na kuwasaidia. Pia anajenga uhusiano mwema miongoni mwa wanafunzi ili wale wanaofanya vizuri waweze kuwasaidia wale ambao ufahamu wao ni mdogo na kusaidiana katika masomo mengine''., ananieleza mmoja wa wanafunzi wake, Teresiah Kanini.

Maelezo ya video,

Mwalimu wa Sayansi nchini Kenya ashinda tuzo ya dunia ya mwalimu bora zaidi.

Watawa wenzake wa shirika la Mtakatibu Fransisco wanaoishi nae pia wanasema Kaka Tabichi ni mtu mwenye bidii na mbunifu: ''Brother Peter ana kipaji. Ni mbunifu sana. Ameweza kuleta mbinu tofauti kwenye kundi letu na pia anaweza kuchonga vizuri vitu tofauti kutoka kutokana na mawe.'', anaeleza brothe Albanus Kioko, mmoja wa marafiki zake katika shirika hilo.

Lakini mafunzo yake hayaishii kwenye darasa tu. Katika jamii anayoishi,Peter Tabichi huwafunza wanakijiji kuhusu kilimo endelevu ili waweze kujitosheleza kwa chakula kwa kupanda mimea inayoweza kustahimili ukame.

Anaamini kuwa imani yake imechangia sana katika kazi zake ndani na nje ya darasa.

"Mimi mtawa wa shirika la Mtakatifu Fransisco na tunaamini kuwa tunapaswa kuwa wanyenyekevu na kuchukulia mambo kwa urahisi . Kwa hiyo kila kitu ninachokifanya kinakuwa na msingi wa imani hiyo na lazima nihakikishe kwamba ninakuwa mnyenyekevu sana na mtu asiyependa makuu'' anasema Tabichi.

Chanzo cha picha, Getty Images

Tabichi sasa anajianda kuanza safatri za kutembelea maeneo mbali mbali ya dunia yaliyoathiriwa zaidi na migogoro iliyowaathiri watoto. Amepangiwa pia kushiriki katika mazungumzo ya Umoja wa Mataifa katika Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 2019 na matukio mengine makubwa.

Inatarajiwa kuwa hadithi yake ya mafunzo na sauti yake yenye nguvu itasaidia kuelezea dunia haja ya dharura kuwekeza katika watoto wanaoishi katika maeneo yenye mizozo.

Atajiunga na wachezaji filamu kama Will Smith na Rachel Brosnahan ambao wanaendesha kampeni ya -Elimu haiwezi kusubiri.