Mzozo Khartoum unaacha wapi mustakabali wa amani Sudan kusini?

Kiir Khartoum

Chanzo cha picha, AKUOT CHOL

Rais Salva Kiir wa Sudan kusini amejitolea kuwa mpatanishi katika kuidhinisha mageuzi ya kisiasa nchini Sudan baada ya kupinduliwa kwa kiongozi aliyekuwepo Omar al-Bashir, Reuters linaripoti.

Hatua hii inajiri miezi saba baada ya Bashir kusaidia katika upatanishi na kufikiwa makubaliano ya amani kati ya Rais Kiir na kundi kuu la waasi wa upinzani Sudan kusini , uliosaidia kupata uhuru wa taifa hilo changa barani Afrika baada ya mapigano ya miongo kadhaa.

"Rais amejitolea kuwa mpatanishi katika majadiliano ya makundi tofauti nchini Sudan kwa matumaini kwamba mageuzi mapya yataidhinisha siku mpya Sudan...," Reuters limenukuu taarifa ya ofisi ya rais.

Mzozo wa kisiasa na wa kiaraia nchini Sudan umegubika majadaliano, lakini hali inayojiri nchini humo inatazamwa vipi kutoka Sudan Kusini?

Swali kubwa ni vipi taifa hilo litakavyofanikiwa katika pendekezo hili sasa?

Inafahamika kwamba Bashir alikuwa na jukumu kubwa katika kufikiwa makubaliano ya amani Sudan Kusini.

Chanzo cha picha, ASHRAF SHAZLY

Maelezo ya picha,

Makubaliano yaliosainiwa Khartoum mnamo Juni 2018 kati ya rais Omar al-Bashir, Rais Salva Kiir Mayardit, na Riek Machar, ya kusitisha mapigano Sudan kusini

Historia ya Sudan mbili

Mataifa hayo mawili yana historia ndefu na huenda ndio sababu Sudan Kusini inaona ina wajibu wa kuhusika katika yanayoshuhudiwa hivi sasa Sudan.

Sudan kusini ilijitenga na Sudan mnamo 2011 na miaka miwili baada ya hatua hiyo kubwa, taifa hilo changa lilitumbukia katika vita vya kiraia.

Takriban watu 400,000 wameuawa na karibu thuluthi ya idadi jumla nchini imeachwa bila ya makaazi.

Rais Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake Riek Machar wametia saini makubaliano ya amani hivi karibuni kumaliza mzozo huo wa miaka mitano.

Ni makubaliano yaliofikiwa kwa usaidizi wa Sudan, lakini jana Riek Machar alisema hayuko tayari kurudi Juba na anataka mipango ya kuunda serikali ya muungano iahirishwe mpaka masuala ya usalama yatakapo tatuliwa nchini.

Siku chache zilizopita rais Salva Kiir pia amesema haoni uwezekano wa kuundwa serikali ya muungano mwezi ujayo na kuongeza kwamba masuala ya usalama hayajatatuliwa.

Wanaharakati mjini Juba wana wasi wasi mwingi kuhusu uwezekano wa kufikia makubaliano katika mzozo ambao kiini chake ni masuala ya usalama.

'Wasiwasi wa usalama utabaini amani ya kudumu Sudan kusini na tunavyozungumza muungano wa vikosi haujaidhinishwa na mpango huo bado upo katika kiwango cha awali na muda umesogea, kwahivyo hili linawatia wasiwasi wengi' anasema Sarah Nyanath, afisa katika jukwa la mashirika ya kiraia Sudan kusini.

Chanzo cha picha, ASHRAF SHAZLY

Hali Khartoum inaacha wapi mustakabali wa amani Sudan kusini?

Akizungumzana BBC Bi Nyanath ameeleza kwamba hali nchini Sudan ina athari kubwa kwa mustakabali wa amani Sudan kusini.

'Ilituchukua miezi mingi katika majadiliano huko mjini Addis Ababa Ethiopia, na kilichochangia kujivuta kwa mazungumzo hayo ilikuwa ni suala la usalama. Lakini wakati mazungumzo yalipohamishwa Sudan, Na kutokana na uzoefu na uelewa wa Bashir kuhusu taifa la Sudan kusini, alisaidia sana kusukuma mazungumzo hayo na kufika mahali tulipofika.

Na sasa vile kunashuhudiwa mabadiliko katika utawala wa Khartoum, hatujui ni nani anayeingia kushikilia usukani'.

Nyanath anasema raia Sudan kusini wana wasiwasi zaidi kutokana na kwamba waandamanaji Khartoum wanaonekana hawana ajenda ya pamoja.

'Kwa kuangalia sababu ya kufanyika maandamano hayo ambayo awali yalikuwa ni ya kulalamikia gharama kubwa ya maisha, yakawa ya kushinikiza mageuzi ya utawala na sasa mambo mengine yanaibuka katikati ya maandamano hayo, ikiwemo baadhi wanaoshinikiza muungano wa Sudan itakayojumuisha Sudan yetu (ya kusini) ambayo tayari imejitangazia uhuru'.

'Ina tia wasiwasi, wakati waandamanaji wanaendelea kushinikiza huenda idara mbali mbali zikagawanyika au zikakataa kusikiza matakwa ya raia, na haya ni wakati tuna idadi kubwa ya wakimbizi nchini humo, na zaidi ya hayo Khartoum ikiwa ni mdhamini mkuu katika makubaliano ya amani, ikiwemo jitihada za kuundwa serikali ya muungano ambayo kufikia sasa hata haijaundwa' anaeleza Bi Nyanath.

Chanzo cha picha, STEFANIE GLINSKI

Maelezo ya picha,

Raia katika maandamano ya amani katika siku za nyuma Sudan kusini wameelezea hasira yao na mateso yanayowakabili wanawake na watoto Juba

Ameongeza kwamba haya yote yanachangia wasiwasi na maswali mengi kuhojiwa kwa sasa.

Inaarifiwa kwamba serikali ya Sudan kusini imetuma ujumbe mjini, Khartoum, kwa miongini mwa mengine, kuahidi kuwajibikia uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.

"Mheshimiwa rais amehakikisha kuunga mkono mageuzi ya amani yatakayo idhinisha siku mpya Sudan ambako amani, umoja na heshima ya mipaka na uhuru wa watu wa Sudan utahakikishwa." Linaripoti gazeti la South Sudan News Now kwa kunukuu ujumbe wa kutoka ikulu ya rais.

Raia Khartoum wanasema watasalia katika maandamano mitaani mpaka wakati ambapo viongozi wa kijeshi ambao wanashikilia madaraka hivi sasa, watakabidhi uongozi wa nchi kwa utawala wa kiraia.