Je ni kweli Tanzania kumezinduliwa kiwanda cha kutengeneza 'viungo nyeti' bandia?

NGONO

Chanzo cha picha, KAREN CHARMAINE CHANAKIRA

Kuna picha inasambaa mitandaoni nchini Tanzania, ikimuonesha Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela akiwa ameshika mfano wa uume huku akitabasamu.

Maelezo ya jumla yanayoambatana na picha hiyo ni kuwa kiongozi huyo amezindua kiwanda cha utengenezaji 'nyeti bandia.'

Picha hiyo imekuwa ikitapakaa kwenye makundi ya WhatsApp kama moto wa nyika, na imezua mjadala mkali mitandaoni kwa ujumla.

Je kiwanda kipo ama uzushi ?

Picha ni halisi, kweli Bw Kasesela alishika viungo hivyo bandia na kupigwa piacha.

Ila ni uzushi kuwa tukio lilikuwa ni la kuzindua kiwanda cha utengenezaji wa viungo hivyo bandia.

Kwa kutumia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Kasesela alilazimika kutolea maelezo picha hiyo. Inahusiana na elimu ya maambukizi ya ukimwi.

"Hii ndio Tanzania. Mngemuuliza aliye leta picha hizi maana lazima alikuwepo kwenye tukio ila kwa kuwa alikuwa na nia ovu na meamua kuchangia ili kutimiza matakwa yake," ameeleza Kasesera na kuongeza; "Iringa ina kasi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi ya asilimia 11. Kama kiongozi nashiriki kufundisha watu njia za kujikinga."

Baada ya maelezo hayo, wapo ambao walimpa pole Kasesela, "hapa kweli kabisa bwana kasesela raia wameamua kukuonea na unastahili kuombwa radhi," aliandika mtumiaji mmoja wa mtandao wa Twitter.

Baadae, aliyeanzisha mjadala huo mtandaoni, Kumbusho Dawson alisahihisha taarifa yake na kuomba radhi.

Magufuli na wanaume kuoa wake wengi

Mwaka jana Rais wa Tanzania John Magufuli alikuwa akihusishwa na taarifa mitandaoni kuwa amewataka wanaume wa nchi yake waoe mke zaidi ya mmoja.

"Wanawake wengi ambao hawajaolewa wanalizimika kushiriki uasherati na waume za watu kwa sababu kuna ukosefu wa wanaume wa kuwaoa," Magufuli alidaiwa kuseama maneno hayo na kunukuliwa na mtandao wa nipasheonline.com na kuongeza: "Siwalazimishi, lakini ninawashauri kuoa wake wawilia au zaidi ili kupunguza idadi ya wanawake wasio na waume."

Taarifa hiyo pia ilisambaa kwa kasi ndani na nje ya Tanzania, na mchungaji mmoja nchini Ghana alizinukuu kwenye moja ya mihadhara yake.

Hata hivyo, taarifa hiyo pia ilikuwa ghushi. Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu ya Tanzania Gerson Msigwa alilazimika kuikanusha taarifa hiyo kupiti mtandao wake wa Twitter.

Mitandao na kusambaa taarifa ghushi

Mitandao ya kijamii inasifiwa kwa kurahisisha mawasiliano na kufungua uwanja mpana wa mijadala duniani kote.

Mitandao hiyo imekuwa ikisifiwa kama nguzo muhimu ya kulinda demokrasia na uhuru wa kujieleza kwenye maeneo ama nchi ambazo dola imekuwa ikiminya uhuru wa watu.

Maelezo ya sauti,

Solomon Mugera: Hizi ndizo njia bora za kukabili habari feki mtandaoni

Lakini mitandao pia imekuwa ikilaumiwa vikali kuwa nyenzo ya kusambazwa kwa taarifa ghushi ama fake news, kwa lugha ya kingereza.

Pande zote mbili, chama tawala na upinzani zilikuwa zikitupiana lawama za kusambaza taarifa hizo mitandaoni kwa nia ovu ya kupaka matope upande wa pili.