Mahakama ya Upeo ya Uganda 'yamsafishia njia' Museveni kugombea tena Urais

Yoweri Museveni

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Rais wa Uganda Yoweri Museveni

Mahakama ya Upeo nchini Uganda imethibitisha uamuzi wa mahakama ya katiba ya nchi hiyo kuidhinisha mabadiliko ya katiba yaliondoa ukomo wa umri wa kugombea urais.

Kesi hiyo ilifunguliwa katika mahakama hiyo na wapinzania wa rais wa nchi hiyo Yoweri Musevenia mabo wanataka kumzuia kugombea uraisi kwa awamu ya sita.

Hata hivyo, majaji wanne walipinga hoja za rufaa hiyo huku wanne wakikubaliana nayo.

Jaji Mkuu wa Uganda Bart Katureebe alitangaza kuwa "rufaa hii imeshindwa" kutokana na zaidi ya nusu ya majaji wa mahakama hiyo kuipinga.

Mwezi Julai mwaka 2018, Majaji wanne kati ya watano wa jopo la majaji ya Katiba ya nchi hiyo waliamua kuwa mabadiliko hayo ya katiba ni halali.

Awali umri wa mwisho kwa kugombea ulikuwa ni miaka 75.

Bunge la Uganda ambalo wajumbe wake wengi ni kutoka chama tawala cha NRM mwaka 2017 walibadili katiba na kuondoa ukomo wa umri wa kugombea urais.

Mabadiliko hayo hata hivyo yalipita kwa ugumu, huku upinzani na maafisa usalama wakirushiana makonde ndani ya ukumbi wa bunge.

Museveni kashateuliwa kugombea 2021

Hii inamaana ya kuwa, kiongozi huyo mwenye miaka 74, na aliyeingia madarakani kwa mtutu wa bunduki mwaka 1986, atagombea urais kwa muhula wa sita.

Maelezo ya picha,

Luteni Jenerali Kainerugaba Muhoozi anadaiwa kupikwa ili amrithi baba yake Yoweri Museveni uraisi wa Uganda

"Chama cha National Resistance Movement (NRM) kimekubali, katika kikao kilichoongozwa na Museveni kuwa " (Museveni) aendelee kuongoza harakati na taifa mwaka 2021 na kuendelea ili kuondosha vikwazo vya mabadiliko na maendeleo," ilisema taarifa ya chama hicho.

Miaka ya nyuma, Museveni aliwahi kusema kuwa, viongozi "wanaodumu" madarakani ndio chanzo cha matatizo barani Afrika.

Hata hivyo, wakati akigombea muhula wa tano wa madaraka mwaka 2016, alisema kuwa huo haukuwa muda muafaka kwake kuondoka madarakani kwani bado alikuwa na kazi ya kufanya.

Museveni amekuwa akituhumiwa kumuandaa mtoto wake Luteni Jenerali Muhozi Kainerugaba kuja kumrithi pindi atakapoondoka madarakani.

Hata hivyo, Kainerugaba amekanusha vikali madai hayo.