Uchunguzi dhidi ya Trump: Mwanasheria Mkuu wa Marekani 'athibitisha' rais wa nchi hiyo hana hatia

William Barr

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

William Barr amekuwa akishutumiwa kufanya mkutano na wana habari kabla ya kutolewa ripoti

Mwanasheria Mkuu wa Marekani amemtetea rais wa taifa hilo Donald Trump dhidi ya tuhuma za kuzuia uchunguzi dhidi yake, na kusisitiza kuwa hakuna ushahidi uliodhihiri kuwa alikula njama mamlaka za Urusi.

Bwana William Barr amekutana na wanahabari jijini Washington hii leo muda mfupi kabla ya ripoti ya uchunguzi wa sakata hilo kuachiwa.

Barr pia amesema kulichunguzwa visa 10 kumhusu Trump iwapo alizuia ama aliingilia uchunguzi dhidi yake.

Hata hivyo, Barr anakabiliwa na upinzani mkali akisemwa kuwa nampendelea Trump.

Wanasiasa waandamizi kutoka chama cha Democrats wanamshutumu mwanasheria huyo, ambaye ni mteule wa Trump, kwa 'kuchakachua' ripoti hiyo.

Ripoti hiyo, maarufu kama ripoti ya Muller imetolewa rasmi leo japo kuna maeneo ambayo yamefichwa kwa sababu za kiusalama.

Barr amejitetea akidai "nimejitoa kuhakikisha kuwa kuna uwazi wa hali ya juu" kwa uchapishaji wa ripoti hiyo, na kusema sehemu zilizofichwa ni "chache".

Muda mfupi baada ya Barr kuongea na waandishi, Trump alituma ujumbe wa dhihaka akisema "mchezo umekwisha" kwa wale "wanaonichukia na wanachama wa Democrats wenye msimamo mkali."

Kabla ya hapo, Trump alichapisha mlolongo wa wa ujumbe kwenye ukurasa wa kijamii wa Twitter akisema uchunguzi huo dhidi yake akisema "ni habari kubwa zaidi ya kughushi kuwahi kutokea" na "udhalilishaji wa mamlaka ya rais".

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Rais wa Marekani Donald Trump

Ripoti ya Mueller ni kitu gani?

Ripoti ya Muller ni uchunguzi wa miezi 22 juu ya uwezekano wa kula njama baina ya timu ya kampeni ya uchaguzi ya Trump mwaka 2016 na Urusi.

Uchunguzi huo uliongozwa na Mueller, ambaye aliteuliwa kuongoza kazi hiyo mwaka 2017 baada ya vyombo vya kiintelinjesnia vya Marekani kubaini kuwa Urusi walijaribu kushawishi Trump ashinde uchaguzi.

Mueller pia alichunguza iwapo Trump aliingilia uchunguzi pale alipoamuru uchunguzi dhidi ya mshauri wake wa usalama wa taifa Michael Flynn usitishwe, na baadae kumfuta kazi Mkuu wa FBI James Comey.

Flynn amekiri kuwa aliwadanganya FBI juu ya mahusiano yake na Urusi.

Hili ni swali la msingi: upi unatakiwa kuwa ukomo wa tabia ya Rais wa Marekani?

Rais huyu wa 45 amekua akifurahia kuvunja kanuni na sheria-wengine wamedai kuwa mashambulizi yake mara kwa mara dhidi ya Mueller kulikosababisha kuingiliwa na kutishiwa.

Anasema kuwa Rais amefedheheka na kughadhabishwa kutokana na imani kuwa uchunguzi ulikua ukidhoofisha kiti chake.Lakini Mwanasheria maalum Rober Mueller amebainisha mazingira 10 wakati Rais alipokiuka sheria-moja kati ya uhalifu mkubwa kutekelezwa kama inavyoeleza katiba ya Marekani ambapo madhara yake yanaweza kuwa kuondolewa madarakani.

Mwanasheria Mkuu amesema kuwa hawavuki kizingiti hali itakayosababisha kushtakiwa.Bwana Mueller hata hivyo anasema kitu kingine tofauti:''Wakati ripoti hii haihitimishi kuwa Rais ametenda kosa, pia haina maana kuwa halaumiwi.''

Lakini ni sawa? Unaweza kufanya unachokipenda kwa vile si makosa kisheria? Mwisho wa mchakato huu kwa kweli tunaweza kusema kuwa Rais Donald Trump amebaudilisha urais lakini urais haujambadilisha.