India: Ajikata kidole baada ya kupigia kura Chama kimakosa

Pawan Kumar

Chanzo cha picha, Yogesh Kumar Singh

Maelezo ya picha,

Bwana Kumar anasema alikipigia kura chama ambacho hakukikusudia

Mpiga kura mmoja nchini India amesema amekikata kidole chake baada ya kugundua kuwa alikipigia kura Chama cha siasa ambacho hakukidhamiria.

Pawan Kumar amesema kwa bahati mbaya aliishia kupigia kura chama tawala Bharatiya Janata (BJP), alieleza kwenye video iliyosambaa mitandaoni.

Alitaka kukipigia chama kingine lakini alichanganya alama nyingi zilizokuwa kwenye mashine ya kupigia kura.

Kila mpiga kura kidole chake cha shahada huwekwa alama kwa wino baada ya kupiga kura.

Alipiga kura yake siku ya Alhamisi katika eneo la Bulandshahr jimbo la kaskazini la Uttar Pradesh.

''Nilitaka kupiga kura kwenye alama ya Tembo, lakini nikapiga kwenye alama ya Ua kimakosa,'' Bwana Kumar alisikika kwenye video. Alielezea alama za vyama zilizokua kwenye mashine sambamba na jina la kila mgombea.

Chanzo cha picha, @Benarasiyaa/Twitter

Maelezo ya picha,

Pawan Kumar

Uchaguzi huu unapitia awamu saba, huku kura zikitarajiwa kuhesabiwa ifikapo tarehe 23 mwezi Mei. Nchini India kuna wapigakura 900, wanaofanya uchaguzi wa India kuwa mkubwa kuwahi kushuhudiwa duniani.

Wakati BJP alama yake ni Ua, Tembo ni alama ya chama cha Bahujan Samaj (BSP), Chama kilichoungana na vyama vingine viwili kupamban na chama tawala.

Alama za vyama zina nafasi kazi kubwa kwenye uchaguzi wa India kwa kuwa ni rahisi kutambulika kwenye nchi yeyote ambayo ina watu wengi wasio na elimu.

Kuna vyama mbalimbali na muungano wa vyama ambavyo huwachanganya wapiga kura.