Kwanini biashara ya bangi ni ngumu Uruguay hata baada ya kuhalalishwa?

Shamba la bangi

Chanzo cha picha, IRCCA

Maelezo ya picha,

Uruguay ilihalisha matumizi ya bangi kwa starehe mwaka 2013

Uruguay ilikuwa ndiyo nchi ya kwanza duniani kuhalalisha matumizi ya bangi kwa starehe. Miaka mitano baada ya hatua hiyo, je biashara ya bangi inaendeleaje?

"Tuliuza bangi nyingi sana siku ya kwanza," anasema Esteban Riviera, ambaye anamiliki duka kubwa na la kisasa la dawa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Montevideo.

"Tuliuza pakiti 1,250 ndani ya saa sita. Kulikuwa na foleni ndefu sana ya wateja wa bangi."

Sheria ya kuhalalisha bangi ilipitishwa 2014 lakini uuzwaji rasmi ulichelewa mpaka mwezi Julai 2017.

"Iliwachukua muda mrefu,serikali ilisema kuwa inaleandea suala hilo kwa uangalifu mkubwa, hatua kwa hatua," anafafanua Guillermo Draper, mwandishi wa habari raia wa Uruguay ambaye ameandika kitabu juu ya mchakato wa nchi yake kuhalalisha bangi.

Maelezo ya picha,

Bangi nchini Uruguay inauzwa kwenye maduka ya dawa tu.

Licha ya kuwa waangalifu katika kutekeleza sheria ya bangi, bado kuna changamoto kubwa zinazoikabili sekta hiyo nchini Uruguay.

"Benki yangu iliniambia nichague kati ya kuuza bangi ama kufunga akaunti zangu," anaeleza Esteban Riviera. "Ilinilazimu kuacha kuuza bangi.

"Duka langu la dawa ndilo lilikuwa la kwanza kusajiliwa kuuza bangi za starehe kihalali," anaendelea huku akicheka kwa dhihaka, "lakini pia lilikuwa la kwanza kuacha kuuza bangi Uruguay."

Wafanyabiashara kama Esteban wanategemea mikopo kutoka kwenye mabenki ya Marekani uenye matawi ya kimataifa.

Ushirikiano huo wa kibiashara uliingia hatarini pale mabenki hayo yalipogundua washirika wao nchini Uruguay wanapokea pesa za bangi.

Japo Uruguay ni nchi huru, bado inaminywa na sheria za fedha za Marekani hususan kwenye bidhaa kama bangi ambayo ni haramu nchini Marekani.

Bangi ya starehe inaruhusiwa kuuzwa kihalali kwenye maduka ya dawa tu nchini Uruguay - na kutokana na vikwazo vya kibenki - kwa sasa kuna maduka 17 tu yanayotoa huduma hiyo kwenye nchi yenye watu milioni 3.5.

Ni miezi 18 tangu bangi ianze kuuzwa, japo shauku imeondoka lakini foleni za wanunuzi bado ni ndefu.

"Nimesimama kwenye foleni juani, naungua, ila nasubiri ifike saa nane mchana muda amao wanafungua mauzo," anaeleza mwanamke mmoja kwenye foleni nje ya duka ambalo bado linauza bangi jijini Montevideo.

Maelezo ya sauti,

Bangi yaaza kuunzwa madukani nchini Uingereza)

"Hili ni moja ya maduka ambayo yanauza kiwango kikubwa bila ya sharti la kuagiza awali mtandaoni. Kuna maduka mengi ambayo yanauza kiwango kidogo, hivyo watu wengi hupanga foleni nna kuambulia patupu. Inasikitisha sana."

Mfumo wa manunuzi unadhibitiwa vilivyo. Wateja lazima wajiandikishe kwenye rejesta ya serikali na kiwango cha juu kwa wiki ni gramu 10, sawa na misokoto 20.

Mamlaka pia zinachunguza makali ya bangi na kuhakikisha kuwa haipumbazi kupitiliza na wala haipandishi kwa kadi mapigo ya moyo ya mtumiaji.

Maelezo ya picha,

Wateja wa bangi wakipanga foleni nje ya duka la dawa

Katika maduka hayo ya dawa, kuna aina nne tu za bangi ambazo zinauzwa, hakuna hata moja ambayo ni kali kupitiliza. Bei ya gramu tano ni pauni 5, kima hicho pia kimewekwa na mamlaka.

Mmiliki wa duka linalouza bidhaa hiyo Gabriel Llano anasema yeye hupata faida ya asilimia 20 kwenye kila pakiti ya gramu tano. Hata hivyo faida kubwa ipo kwenye bidhaa zinazoambatana nayo kama karatasi za kufungashia na kuvutia.

Mauzo yanapoanza, wateja huingia mmoja baada ya mmoja na kuweka kidole gumba kwenye mashine maalumu inayotambua wanunuzi waliosajiliwa na kuhakiki iwapo hawajazidisha kiwango cha gramu tano.

Baada ya uhakiki, wanalipa kwa fedha taslimu, maana wakilipa kwa kadi benki zinaweza kufanya uchunguzi wa fedha zinazoingia, tena kwa kasi. Wakigundua tu ni pesa za bangi, kuna hatari ya kufungiwa akaunti hiyo.

Lengo kuu la kuhalaisha bisahara ya bangi Uruguay ilikuwa ni kufanya watu waache kununua kwa 'njia za panya' lakini foleni ndefu nje ya maduka ya dawa inadhihirisha kuwa mahitaji ni makubwa kuliko uwezo wa usambazaji.

Biashara ya Dunia

"Nchini Uruguay, hakuna hata mtu mmoja ambaye alishawahi kulima bangi kwa kiwango kikubwa," amesema Diego Olivera, katibu-mkuu wa Bodi ya Taifa ya Madawa ya nchi hiyo.

Amesema kwa sasa makampuni yameshapata uzoefu wa kutosha na yanatarajiwa kuanza uzalishaji wa kiwango cha juu hivi karibui.

Bodi hiyo ifahamikayo kama IRCCA pia inapanga kutoa leseni mpya kwa kampuni nyengine nne ama tano kulima bangi, kwa sasa kuna kampuni mbili tu.

Maelezo ya picha,

Meneja wa ubora wa bangi wa kampuni ya Fotmer ya Uruguay Elena Gonzalez Ramos

Soko nchini Uruguay ni kubwa na kampuni za ndani zimekuwa zikichangamkia fursa kwa nguvu. Kampuni ya maabara ya ICC ambayo ina leseni ya kuzalisha bangi ya starehe na dawa.

Uzalishaji wa bangi kama dawa una faida kubwa zaidi na masoko mengi ya nje.

Hivi karibuni, kampuni kubwa ya uzalishaji wa bangi nchini Canada - Aurora - hivi karibuni ilitoa dola milioni 220 ili kuinunua kampuni ya ICC. Aurora sasa inatazamiwa kuwa kampuni kubwa zaidi ya bangi kwenye Bara Amerika.

Mwezi Oktoba 2018, Canada ilikuwa nchi ya pili duniani kuhalalisha matumizi ya bangi kwa starehe. Mauzo ya bangi kama dawa yalihalalishwa mwaka 2001.

Soko la bangi ya starehe ni finyu zaidi lakini kama dawa, kampuni za Uruguay kama Fotmer, zina mawanda mapana ya kujitanua duniani.

"Masoko makubwa siku hizi yapo Australia, New Zealand, Canada, Ujerumani na baadhi ya mataifa ya Ulaya," amsema Helena Gonzalez Ramos ambaye ni meneja wa ubara wa kampuni ya Fotmer. "Uzuri ni kuwa kuna maoresho ya sheria kila uchao na tunatarajia bangi kutumika kama dawa itakubalika duniani kote siku si nyingi."