Watu 13 wafariki baada ya Kanisa kubomoka wakati wa Ibada ya Pasaka

Ndani ya kanisa, uharibifu ulivyofanyika

Chanzo cha picha, KZN EMS/ Arrive Alive

Maelezo ya picha,

Waziri wa kazi alipanga kufika kwenye eneo la ibada ya Ijumaa Kuu kwenye eneo hilo

Takriban watu 13 wamepoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa baada ya ukuta kuanguka Afrika Kusini wakati wa kuanza ibada ya pasaka katika Kanisa la Pentekoste.

Mamlaka za huduma dharura zimesema watu 29 walikimbizwa hospitali baada ya ajali hiyo katika eneo la KwaZulu-Natal.

Maafisa mjini humo wamesema sababu ya ajali ni mvua nyingi iliyonyesha maeneo ya eMpangeni siku ya Alhamisi usiku.

Ripoti zinasema watu wengine walikua wamelala wakati ukuta ulipoanguka.

Siku ya Ijumaa, ibada maalum ilifanyika chini ya turubai kubwa mbele ya Kanisa televisheni ya eNCA iliripoti.

Rais Cyril Ramaphosa alitembelea kanisa mwaka jana na baadhi ya waumini waliripotiwa kuomba msaada ili waweze kujenga kanisa jipya.

Waziri wa kazi Midred Oliphant ni muumini wa kanisa hilo na alikua na mpango wa kuhudhuria ibada ya Ijumaa kuu katika kanisa hilo.

Aliwasili kwenye eneo la tukio na kusema: ''Hata wakati wa magumu, bado tunapaswa kuweka imani zetu kwa Mungu.''