Sudan: Waandamaji waapa kutangaza baraza la utawala wa nchi Jumapili

Umati mkubwa wa waandamanaji ulikusanyika tena nje ya makao makuu ya jeshi Ijumaa , huku ukishangilia: "Uhuru, amani na haki".

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Umati mkubwa wa waandamanaji ulikusanyika tena nje ya makao makuu ya jeshi Ijumaa , huku ukishangilia: "Uhuru, amani na haki".

Kiongozi wa vuguvugu la maandamano anasema kuwa watawataja wajumbe wa uongozi wa mpito Jumapili , watakaochukua nafasi ya utawala wa sasa wa jeshi la junta.

Baada ya miezi ya maandamano , jeshi lilimg'oa madarakanikiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir wiki iliyopita.

Lakini waandamanaji wanataka jeshi lirejeshe mamlaka ya uongozi kwa raia.

Kuunga mkono madai yao , umati mkubwa wa watu ulikusanyika tena nje ya makao makuu ya jeshi Ijumaa , huku ukishangilia: "Uhuru, amani na haki".

Maelfu ya watu walikusanyika katikati mwa mji mkuu Khartoum,baada ya sala ya Ijumaa katika maandamano makubwa kuwahi kushuhudiwa tangu Bwana Bashir aondolewa madarakani kwa nguvu , limeripoti shirika la habari la Reuters.

Jeshi limekubali baadhi ya madai ya waandamanaji yakiwemo kusema kuwa wanaweza kumteua waziri Mkuu na kumuhamishia Bwana Bashir katika gereza kuu lenye usalama mkali.

Hata hivyo jeshi limekataa kuachia madaraka na Wasudani wengi wanahofu kwamba maafisa wawe wale wa kijeshi ndio wanaoendelea kuongoza.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Maandamano dhidi ya Bashir yakasambaa ghafla kote nchini Sudan huku waandamanaji wakidai abaye alinyakua mamlaka kwa mapinduzi mwaka 1989 aondoke madarakani

"kama tusipokaa , itakuwa ni kama hatujafanya lolote, tutaendelea kukaa hadi tutakapoung'oa utawala wa kijeshi ," Muandamanaji Rania Ahmed mwenye umri wa miaka 26 katika mahojiano na Reuters.

Baraza la wasomi nchini Sudan, ambalo limekuwa likiongoza maandamano, limesema kuwa litawataja wjumbe wake wa baraza la mpito katika mkutano wa waandishi wa habari Jumapili saa kumi na moja jioni kwa saa za Sudan nje ya makao makuu ya jeshi.

Maelezo ya video,

Picha hii inaashiria nafasi ya wanawake katika maandamano dhidi ya serikalai ya Sudan.

" Tunadai kwamba baraza hili la kiraia, ambalo litakuwa na wawakilishi wa jeshi, lichukue nafasi ya baraza la jeshi ," Ahmed al-Rabia,kiongozi wa shirikisho la muungano wa madaktari, wahandishi na waalimu , aliliambia shirika la habari la AFP.

Wakati huo huo Marekani inamtuma naibu waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Makila James, ambaye anahusika na maswala ya Afrika mashariki aende Khartoum mwishoni mwa juma kufuatilia hali ya mambo nchini humo.

"Utashi wa watu wa Sudan ni wazi: ni wakati wa kusonga mbele kuelekea serikali ua mpito ambayo itakuwa ni shirikishi na yenye kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria," anasema msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Morgan Ortagus.

Maandamano yalianza miezi minne iliyopita, baada ya ongezeko la bei ya mkate na mafuta.

Lakini ghafla maandamano yakasambaa kote nchini Sudan huku waandamanaji wakidai Bwana Bashir, mabaye alinyakua mamlaka kwa mapinduzi mwaka 1989 aondoke madarakani.