Sokwe mtu wawili wapiga picha ya 'selfie' na askari wanyama pori nchini DRC

Gorillas posing for selfie in Virunga National Park, DR Congo

Chanzo cha picha, Ranger Mathieu Shamavu

Maelezo ya picha,

Hawavumi lakini wamo!

Sokwe mtu wawili wameshangaza wengi kwa kuweza kuiga mkao wa binaadamu waliponaswa kwenye picha iliyopigwa kwa kutumia kamera ya mbele ya simu ya mkononi, maarufu kwa lugha ya mtandaoni kama selfie.

Sokwe hao wamepiga selfie hiyo na askari wa wanyamapori ambao waliwaokowa kutoka kwenye makucha ya majangili walipokuwa wadogo.

Picha hiyo imepigwa katika makao ya sokwe yatima kwenye Hifadhi ya Taifa ya Virunga nchini DR Congo, ambapo sokwe hao wamekuwa wakilelewa toka wazazi wao kuuawa na majangili.

Naibu mkurugenzi wa hifadhi hiyo Innocent Mburanumwe ameiambia BBC kuwa sokwe hao walijifunza kuiga tabia za binaadamu wanaowatunza toka walipokuwa wadogo.

Sokwe hao, kwa mujibu wa Mburanumwe wanadhani askari hao ni wazazi wao.

Mburanumwe pia ameiambia BBC kuwa mama wa sokwe hao waliuawa Julai 2017.

Sokwe hao waliokolewa wakiwa na umri kati ya miezi miwili na minne.

Muda mfupi baada ya wazazi wao kuuawa, sokwe hao waliokolewa na askari na kutunzwa kwenye makazi maalumu ndani ya hifadhi ya Virunga mpaka hii leo.

Kwakuwa wamekuwa wakiwa na askari waliowaokoa, Mburanumwe anasema, "wanaigiza tabia za binaadamu" - na kusimama kwa miguu miwili ndio namna yao ya "kujifunza kuwa binaadamu".

Hata hivyo "haitokei kila wakati", amesema Mburanumwe.

"Nilipigwa na mshangao nilipoiona picha hiyo .... ni picha ichekeshayo. Ni jambo la kushangaza kuona namna gani sokwe wanaweza kuiga mwanadamu na kusimama."

Kuwa askari wa wanyama pori kwenye eneo hilo hata hivyo si kazi nyepesi au ya raha tele - ni kazi ngumu sana.

Askari wanyama pori watano mwaka jana waliuwa na watu wanaodhaniwa kuwa waasi katika shambulio la kushtukiza kwenye hifadhi ya Virunga.

Kwa ujumla, toka mwaka 1996, askari wanyamapori 130 wameuawa Virunga toka mwaka 1996.

Hifadhi ya Virunga ipo Mashariki mwa DRC eneo ambalo limetawalia na vita baina ya serikali na makundi kadhaa ya waasi.

Baadhi ya makundi hayo yamekita kambi ndani ya hifadhi hiyo, na wamekuwa wakishiriki biashara haramu ya ujangili.