Rose Marie Bentley: Mwanamke wa Marekani aliyeishi na viungo vya mwili katika sehemu zisizofaa

Rose Marie Bentley

Chanzo cha picha, Courtesy of the Bentley family

Maelezo ya picha,

Rose Marie Bentley aliishi na hali hiyo isiokuwa ya kawaida kwa miaka 99

Mwanamke mmoja nchini Marekani ameishi na viungo vya mwili katika sehemu zisizofaa hadi akafariki dunia akiwa na miaka 99.

Rose Marie Bentley, alifariki mwezi Oktoba mwaka 2017, lakini alikua amewapatia idhini watafiti wa Chuo Kikuu cha Oregon kufanyia uchunguzi mwili wake.

Wanafinzi wa sayansi ya viungo vya mwili mara ya kwanza waligundua ya kwamba viungo vyake vingi havikuwa mahali vilipostahili kuwa.

Licha ya kufanyiwa upasuaji mara kadhaa, hali yake haikufahamika.

Madaktari walishanga jinsi Bi Bentley alivyoweza kuishi maisha marefu bila matatizo ya kiafya licha ya hali ya viungo vyake.

Wataalamu wanasema alikua na hali inayofahamika kama ''situs inversus'', iliyomaanisha kuwa ini, utumbo na viungo vingine vya sehemu ya chini ya tumbo vilikuwa mahali pasipo stahili kuwa ima viungo hivyo vilikua upande wa kushoto au kulia.

Moyo wake hata hivyo ulikuwa upande wa kushoto wa mwili kama ilivyokawaida.

Chanzo cha picha, Lynn Kitagawa

Maelezo ya picha,

Picha inayoonesha viungo vya ndani vya mwili wa Bi Bentley vilivyokuwa katika sehemu zisizofaa

Hali hiyo si ya ''kawaida kabisa'', alisema Dkt Cam Walker, mmoja wa maprofesa waandamizi wa sayansi ya viungo katika chuo cha Oregon cha sayansi ya afya, ambaye aliwasaidia wanafunzi wake kubaini maajabu ya kimaumbile ya mwili wa Bentley.

Dkt Walker ameimbia BBC kuwa utafiti huo ulianza wakati wanafunzi wake walipokua wakifanyia upasuaji wa mshipa mkubwa wa kusafirisha damu mwilini lakini wakashindwa kufikia mshipa huo.

Ni hapo walipobaini kuwa mwili wa Bi Bentley ulikuwa tofauti na watu wengine.

Ni mtu mmoja kati ya watu 22,000 ambao huzaliwa na hali kama hiyo duniani.

Hali hiyo mara nyingi huhusishwa na maradhi hatari ya moyo au magonjwa mengine.

Dkt Walker anakadiria kuwa ni mtu mmoja kati ya watu milioni 50 wanaozaliwa nha hali ya viungo vya mwili kuwa katika sehemu zisizostahili ambao huishi hadi utu uzima.

Yeye na wenzake wanaamini kuwa Bentley ni mtu wa kwanza kuwahi kuishi na hali hiyo kwa miaka mingi.

Wanasayansi wametafiti matukio mawili ya wagonjwa walioishi na hali hiyo hadi miaka 70.

"Hakuna hata mmoja wa wafanyakazi wenzangu aliyewahi kuona mtu aliye na ''situs inversus'' japo wengi wao walikuwa wamefunza kuhusu hali hiyo kwa mika 30," Dkt Walker alisema.

"Sijawahi kuona kitu kama hiki."

"Wanafunzi, nadhani, hawatawahi kusahau," alisema

Chanzo cha picha, OHSU/Kristyna Wentz-Graff

Maelezo ya picha,

Dkt Cam Walker na Dkt Mark Hankin waliyofanyia uchunguzi mwili wa Bi Bentley

Louise Allee, mmoja wa watoto wa Bw na Bi Bentley, alikiambia chuo kikuu cha sayansi cha Oregon kuwa mama yake angelifurahia sana jinsi hali yake ilivyoangaziwa.

"Mama angelichukulia suala hili kuwa ni wazo zuri sana", Bi Allee alisema.

Watoto wa Bentley walikiambia chuo hicho kuwa mama yao aliishi maisha ya kawaida licha ya hali aliyopitia.

Alifanyiwa upasuaji mara tatu na wakati huo madaktari walitoa kongosho baada ya kubaini ilikua upande ambao haikustahili kuwa.