Mitandao ya kijamii yabadili muelekeo wa ushawishi

  • Esther Namuhisa
  • BBC Swahili
USHAWISHI

Chanzo cha picha, INSTAGRAM

Si lazima jina lako liwe maarufu ili uweze kujipatia kipatao kupitia kile utakachokiweka katika mitandao ya kijamii.

Kizazi kipya cha watu wenye ushawishi kinaongezeka kutoka kwa watu ambao sio wasanii, wabunifu au wanasiasa.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

James Charles akiwa na Kim Kardashian anajulikana kwa picha upambaji wa uso

Inawezekana ni wazi kabisa hujawahi kusikia jina la James Charles.

Lakini James alishangaza wengi huko nchini Uingereza pale alipokusanya maelfu ya mashabiki wake mwezi Januari kwa ajili ya kujuana tu.

Charles ni mmoja kati ya mifano ya washawishi wa mitandao ya kijamii ambao hawapo katika orodha ya watu maarufu kutokana na kazi yao, lakini wana ushawishi mkubwa wa kuweza kuwafanya watu wafanye jambo Fulani.

Chanzo cha picha, Instagram

Maelezo ya picha,

Mange Kimambi

Mfano mwingine wa karibu ni mtu kama Mange Kimambi ambaye ni raia wa Tanzania anayeishi Marekani. Mange amepata umaarufu mkubwa katika harakati zake za siasa kupitia mitandao ya kijamii na ilifikia watu wananukuu kuwa Mange ameandika jambo fulani.

Huda Kattan, amekuwa akitambuliwa kama kamas "the Bill Gates of beauty influencers" Huda aliamua kuacha ajira yake na kwa msaada wa mitandao ya kijamii ameweza kufungua kampuni yake ambayo ina thamani zaidi ya dola bilioni moja.

Je, mtu ambaye ana ushawishi katika jamii anapaswa kufahamika au kutambuliwa kwa vigezo gani?

Chanzo cha picha, Instagram

Maelezo ya picha,

Baadhi ya wajasiriamali wanaotumia mitandao ya kijamii Tanzania

Yawezekana kuwa ni mtu mwenye kipaji fulani na amefanikiwa kupata kipato kikubwa kutokana shughuli anayoifanya.

Mwanamitindo wa kimataifa , warembo, wabunifu wa mavazi , wapishi au kazi yeyote.

Natasha Ndlovu, ameweza kupata wafuasi 90,000 katika mtandao wa kijamii kutokana na picha za urembo na mitindo ya nguo ambayo amekuwa akiweka kwenye mtandao.

Watu kumuita mshawishi inawezekana kuwa ngumu kusema lakini ni uhalisia kutokana na namba ya watu wanaomfuata katika mitandao hiyo.

Inawezekana kila mtu anapenda kufanya kazi ya kile kitu anachokipenda... kuna watu wengi wameacha ajira zao ili waweze kupata kipato kwa kile kitu wanachokipenda kukifanya.

Huu ni mfano wa wazi ambapo wanawanake wengi barani Afrka wameamua kuwa wajasiriamali na kutumia mitandao ya kijamii ili kupata kipato chao.

Chanzo cha picha, Malkia wa viungo/ facebook

Maelezo ya picha,

Malkia wa viungo

Teddy Bernad ni mjasiliamali wa viungo vya chakula ambapo kutokana umahiri wa utengenezaji wa viungo hivyo, amepachikwa jina la Malkia wa viungo.

Yeye ni msomi wa saikolojia lakini sasa amejiajili na kujishughulisha na utengenezaji wa viungo vya chakula. Alianza kufanya biashara hii kutokana na shauku yake binafsi ya kupenda viungo.

"Nilikuwa na utundu tu wa kuchanganyachanganya viungo na kusoma kwenye mtandao na kuweka vyakula vyangu kwenye mitandao na maswali niliyokuwa napata ya namna nnavyotengeneza na nikiwaelekeza wanakuwa hawaelewi nikaona hapo kuna fursa na nikaamua kwenda kusomea masomo ya muda mfupi ya uzindikaji chakula ".

Aidha kwa kizazi ambacho kinakuwa kwa kusoma masomo ya yaliozoeleka shuleni inawezekana ikawa ni ngumu kubadili mtazamo.

Je, kuna ugumu kwa mtu kuitwa mshawishi ?

Mfanyabiashara wa Uganda na mpenzi wa zamani wa nyota wa muziki wa bongofleva nchini Tanzania Diamond Platinumz, Zari Hassan anayefahamika kama the boss lady ana wafuasi zaidi ya milioni tano.

Umaarufu huo umemuwezesha kupata fursa za kufanya matangazo mbalimbali ya biashara na kuwa na mashabiki wengi ambao hata wengine wanaotumia jina lake na kuvutiwa au kufuatilia kila anachokiandika katika mtandao wa kijamii.

Washawishi hawa katika mitandao ya kijamii wanatengeneza fedha kwa kuweka kile wanachokifanya au kukiweka katika mitandao ya kijamii.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Forbes ilimtaja Kylie Jenner mapema mwaka huu kama bilionea mdogo duniani, aliyejitengenezea utajiri mwenyewe

Jina la mtu linaweza kushawishi watu wa aina fulani kutamani kufika pale ambapo mtu huyo maarufu amepata umaarufu au mafanikio kupitia mitandao ya kijamii.

Watu wengi wanatumia mitandao ya kijamii ili kuwavutia na kuwahamasisha watu kufanya jambo fulani.

Mtandao wa kijamii umempa umaarufu na mafanikio katika biashara yake licha ya kwamba mtu anaweza kusema amewezaje na kwa nini mimi nisiweze.

Mitandao ya kijamii inawapa watu mwanya wa kusimamia kile ambacho wanakipenda , kama ni mitindo au urembo basi Instagram, snapchat au facebook ipo kuonyesha kile unachokiweza.

Kuna ugumu pia wa kuanza kufahamika katika mitandao hiyo ya kijamii ndio maana kuna hata wengine wanadiriki kununua akaunti ya mtu ambaye amekusanya watu wengi tayari ili biashara yake iweze kushamiri.

Msikilizaji mmoja wa radio aliiambia BBC kuwa kupitia umaarufu wake ameweza kuuza akaunti zake za mitandao ya kijamii na kujipataia kipato..

'Unawezaje kuwa mtu wa mfano kwa wengine'

Chanzo cha picha, Nancy

Maelezo ya picha,

Nancy Sumari

Anafahamika zaidi kama Miss Tanzania na Miss World Africa wa mwaka 2005, lakini leo hii mlimbwende huyu ni mjasiriamali na mwanaharakati wa kijami aliyeamua kuwainua vijana na wanawake zaidi katika nyanja mbalimbali za kijami.

Mwaka 2017, Sumari aliweza kupata tuzo la vijana 100 wenye ushawishi zaidi Afrika, lifahamikalo kama 'Africa Youth Awards'.

Washawishi wengi hawaweki kila kitu ambacho unatamani ukikute katika ukurasa wake au umewataka waweke.

Inawezekana ni namna ambavyo wanapenda kulinda kipaji chao na kikubwa ni kutotaka kuwa chini ya kiwango walichojiwekea.

Mara nyingi huwa wanaweka picha ambazo zinafanana na shughuli wanazozifanya.

Salim Kikeke ni mtangazaji wa idhaa ya kiswahili na kupitia mitandao ya kijamii, ameweza kuwashawishi wengi kuendelea kuangalia kipindi chake na hata wengine wakitaka kueleza ni BBC ipi wanazungumzia watasema ile ya Salim Kikeke.

Hata hivyo huwa haijalishi mtu una wafuasi 20 au 20,000, kuweza kuleta utofauti katika maisha ya watu . Kama unaweza kumsaidia mtu kwa kumshawishi kufanya jambo fulani basi wewe ni mshawishi.