Jeshi limemuweka Bobi Wine katika kifungo cha nyumbani

Bobi Wineamewekwa katika kizuwizi cha nyumbani katika kile ambacho polisi wanasema ni hatua ya kumzuwia kufanya mikutano kinyume cha sheria

Chanzo cha picha, Getty Images

Polisi na jeshi nchini Uganda jana jioni walizingira nyumba ya Mbunge wa Kyadondo mashariki Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, saa kadhaa baAda ya kutangaza mpango wake wa kutembea hadi polisi katika maandamano ya umma kupinga ukatili dhidi ya tamasha zake za muziki na wanasiasa wa upinzani.

Aliwataka waganda wote wenye hasira kuungana nae katika mapambano dhidi ya ukosefu wa haki.

Bobi Wine aliwekwa katika kizuizi cha nyumbani katika kile ambacho polisi walisema ilikwa ni hatua ya kumzuwia mwanasiasa huyo wa upinzani kufanya mikutano iliyo kinyume cha sheria.

"Hizo zilikuwa ni hatua zilizochukuliwa chini ya sera ya kuzuwia ili kulinda sheria na utulivu wa umma. Wakati bado anatishia kufanya mikutano kinyume cha sheria ,maafisa wetu wa ujasusi watatusaidia kumpata na tutaweza kuona ni nini kitakachofuatia. Hata hivyo hadi sasa tutaendelea pale majeshi yetu kwasababu hili limekuwa ni suala la usalama wa taifa ," amesema Msemaji wa polisi Bwana Fred Enanga.

Saa kadhaa awali , Bobi Wine alikuwa ametangaza mpango wa kufanya maandamano ya umma kote nchini kupinga hatua ya polisi kuendelea kuweka vikwazo dhidi ya tamasha zake za mziki na ukatili dhidi ya wanasiasa wa upinzani.

Alitangaza hatua yake alipokuwa nyumbani kwake Magere, Kasangati katika wilaya ya Wakiso mchana muda mfupi baada ya polisi kumzuwia asubuhi kufika katika makazi yake ya ufukweni ya One Love Beach yaliyopo eneo la Busabala na kumuingiza katika gari la polisi na kumbwaga nyumbani kwake.

Chanzo cha picha, Getty Images

Bwana Kyagulanyi alikuwa akielekea kwenye makaazi yake ya ufukweni kuvitangazia vyombo vya habari nia yake baada ya polisi kuzuwia tamasha lake la Kyarenga Extra alilotarajia kulifanya katika siku ya Jumatatu ya Pasaka.

"Nilitaka kuiambia dunia kile kinachofuatia na hicho ndicho polisi hawakutaka kukisikia.

Tumetumia njia zote za kisheria polisi wasitusimamishe kuzuwia maonyesho yangu na kuwatesa wapinzani lakini wameshindwa kuelewa. Ninatoa wito wa kuwepo kwa mbinu nyingine za kisheria ambazo ni kupinga ," Bobi Wine alivieleza vyombo vya habari kwenye makazi yake ya Kasangati.

Hali ya wasi wasi ilitanda katika eneo la Busabala jana baada ya polisi kumzuwia Bobi Wine kuelekea kwenye ufukwe unaofahamika kama One Love Beach.

Chanzo cha picha, Getty Images

Bobi Wine alikamatwa na kutoroshwa katika basi dogo la polisi na baadae kutupwa katika nyumba yake iliyopo eneo la Magere.

Aliwaambia waandishi wa habari nyumbani kwake kwamba ataandika barua na kuipeleka binafsi kwa polisi kuwafahamisha juu ya mpango wake wa kufanya maandamano ya amani kote nchini.

" Nitaandikia polisi binafsi na kuipeleka barua kwa miguu. Nitatembea hadi pale na nisubiri majibu yangu kutoka kwao . Ninawatolea wito Waganda wote kuandika barua nyingi ziwezekanazo. Tunahitaji kupata nyingi na tuone ," alisisitiza Bwana Wine

Akijibu hayo, Bwana Enanga alisema atajibu baada ya Bobi Wine kuwaandikia barua.

"Kuna sheria juu ya mikutano , hotuba kwa umma na maandamano ya amani. Kama Bobi Wine anatuandikia na kutekeleza sheria ya POMA (Agizo la umma la udhibiti wa usalama na amani ya jamii ), basi tutamruhusu kwasababu wana haki yao," Bwana Enanga alisema.

Chanzo cha picha, Getty Images

Jumapili , polisi walimuandikia promota wa Bobi Wine kuashiria kuwa matamasha yake ya muziki katika miji ya Kampala, Lira, Gulu na Arua katika siku ya Jumatatu ya Pasaka na Mei 3, 4, na 5, hayafatanyika kwasababu waandaaji walishindwa kutimiza muongozo wa polisi na iwapo angeyafanya yangeweka maisha ya mashabiki wake hatarini.

Kuzuwiwa kwa tamasha zake

Bobi Wine jana alisema kuzuiwa kwa tamasha zake kunamaanisha kuwa tamasha zake za muziki 124 zimezuwiwa na polisi tangu mwaka 2017. Mnamo mwaka 2017, polisi walizuia matamasha ya Bobi Wine yaliyoitwa Kyarenga, wakisema ameshindwa kutenganisha taaluma yake ya muziki na siasa.

Walidai kwamba Bobi Wine mwanamuziki na Bwana Kyagulanyi, mwanasiasa, ni watu wawili tofauti na walimtaka kama mwanamuziki kwenye jukwaa, na sio mwanasiasa.

Bobi Wine alisema aliwashitaki polisi kwa kuzuia matamasha yake lakini kesi haijapangwa kusikilizwa mahakamani.