Serikali ya Tanzania yasema ipo kwenye majadiliano na IMF kuhusu ripoti ya hali ya uchumi wa nchi hiyo

Sarafu ya Tanzania

Chanzo cha picha, Getty Images

Serikali ya Tanzania imevunja ukimya juu ya madai ya kuzuia uchapishaji wa ripoti ya tathmini ya ukuaji wa uchumi wake iliyoandaliwa na Shirika la Fedha Duniani (IMF).

Wiki iliyopita, IMF ilitoa taarifa kuwa imenyimwa ridhaa na Tanzania kuchapisha ripoti baada ya wataalamu wake kukamilisha tathmini yao nchini humo.

Matokeo ya ripoti hiyo hata hivyo yamevuja na kuripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa kama Reuters na Bloomberg.

Ripoti hiyo inaonesha ukuwaji wa kiwango cha chini cha asililimia 4 cha uchumi mwaka huu kutoka asilimia 6.6 mwaka 2018.

Mapema Bungeni hii leo, Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania, Dkt Philip Mpango amesema serikali haijazuia kuchapishwa kwa ripoti hiyo bali inaendelea na mazungumzo na IMF.

Mpango amedai kuwa kuna hoja za upande wa Tanzania ambazo hazikutiliwa maanani na wataalamu wa IMF.

Waziri huyo ameyasema hayo alipokuwa akijibu hoja iliyoibuliwa na Mbunge wa Tunduma kupitia chama cha upinzani Chadema, Frank Mwakajoka.

Toka suala hilo lilipoibuka, kumekuwa na shinikizo kubwa kutoka kwa viongozi wa upinzani nchini humo ambao wamekuwa wakishinikiza serikali ivunje ukimya.

Jana Chedema ilitoa taarifa kwa umma kuzitaka mamlaka zitoe kauli juu ya hoja ya IMF kunyimwa ridhaa.

Kiongozi wa chama cha upinzani ACT-Wazalendo Zitto Kabwe aliahidi kuchapisha ripoti hiyo mtandaoni baada ya Pasaka amefanya hivyo hii leo kwa kuichapisha kupitia mtandao wa Jamii Forums.

"Kuna juhudi kubwa kwenye suala la Ripoti ya IMF Kuhusu Hali ya Uchumi wa Tanzania. Jana wenzetu @ChademaMedia wameitaka Serikali iseme kitu, leo Waziri wa Fedha 'kasema kitu' Bungeni na kuna baadhi ya wanasiasa wanaongea na Press sasa hivi. Niliahidi kuweka Ripoti wazi LEO," amesema Zitto mtandaoni.

Hata hivyo wamekataa kuzungumzia vilivyomo ndani ya ripoti wakisema hawaongelei ripoti zilizovuja.

Utaratibu wa IMF kuchapisha ripoti

Kupitia kifungu cha nne cha makubaliano, IMF inaruhusiwa kuchunguza uchumi , hali ya kifedha na sera ya ubadilishanaji wa fedha ya wanachama wake ili kuhakikisha kuwa mfumo wake wa kifedha unatekelezwa bila matatizo yoyote.

Hatua hiyo inashirikisha ziara ya maafisa wa IMF ya kila mwaka katika taifa hilo ili kuangazia data mbali na kufanya vikao na serikali pamoja na maafisa wa benki kuu.

Baadaye wanatoa ripoti kwa bodi kuu, ambayo hutoa maoni yake kwa serikali na kuchapisha ripoti hiyo katika tovuti yake baada ya kupata ruhusa kutoka kwa taifa hilo.