Kimbunga Kenneth: Mamlaka za Hali ya Hewa Tanzania yathibitisha ujio wa upepo mkali

Kimbunga kilichotokea Australia

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania (TMA) imetangaza kuwa Kimbunga Kenneth kimeongezeka kasi na kinatarajiwa kufika pwani ya kusini ya Tanzania na kaskazini mwa Msumbiji kuanzia usiku wa Alhamisi wiki hii.

Kwa mujibu wa TMA, mpaka sasa (Jumatano mchana) kimbunga hicho kipo kilomita 450 kutoka pwani ya Mtwara na kina kasi ya kilomita 130 kwa saa.

Kufikia usiku wa leo, Aprili 24 kimpunga hicho kitakuwa kilomita 250 kutoka pwani ya Mtwara, kikiwa kinasafiri kwa kilomita 150 kwa saa.

Kimbunga hicho kinatarajiwa kuongeza nguvu zaidi Alhamisi mchana ambapo kitakuwa kinasafiri kwa kilomita 170 kwa saa na kitakuwa kilomita 150 kutoka pwani ya Mtwara.

Kwa mujibu wa TMA, eneo husika ambalo kimbunga hicho kitatua (landfall) litakuwa nchini Msumbiji, kikiwa na kasi ya kilomita 100 kwa saa. Eneo hilo litakuwa kilomita 200 kutoka pwani ya Mtwara.

Hata hivyo, mkoa wa Mtwara na maeneo jirani hususani mikoa ya Lindi na Ruvuma yataathirika pakubwa (athari zinategemewa kufikia umbali mpaka wa kilomita 500 kutoka Mtwara).

Maelezo ya video,

Usiku wa leo, kimpunga hicho kitakuwa kilomita 250 kutoka pwani ya Mtwara

TMA imetahadharisha kuwa kimbunga hicho kitaingia nchi kavu na nguvu kubwa (ya upepo na mvua) itakayopelekea madhara makubwa kwa maisha ya watu na mali zao.

"Madhara yanayotarajiwa ni pamoja na mtawanyiko mkubwa wa mafuriko, uharibufu wa mali na makazi, kuezuliwa mapaa kutokana na upepo mkali. Uharibifu wa mazao mashambani na miundombinu kutokana na mafuriko." Imeeleza taarifa iliyotolewa na TMA na kutaja madhara mengine kama: "Kuongezeka kwa kina cha maji ya Bahari katika kipindi kifupi (Storm surge). Kuathirika kwa shughuli za usafirishaji kwa njia ya anga, kwenye maji na nchi kavu."

Mtandao uliobobea kwenye masuala ya hali ya hewa wa AccuWeather wa nchini Marekani juzi ulikuwa wa kwanza kuripoti juu ya uwezekano wa kutokea kimbunga hicho. na kupiga maeneo ya kuanzia Lindi kusini mwa Tanzania mpaka Pemba kaskazini mwa Msumbiji.

Awali, Meneja wa Utabiri wa Hali ya Hewa wa Kimataifa wa AccuWeather, alitoa taarifa kuwa kimbunga Kenneth kinatarajiwa kuzikumba Tanzania na Msumbiji Alhamisi usiku ama mapema Ijumaa wiki hii.

Mamlaka za Msumbiji zatangaza tahadhari

Jana Jumanne, Aprili 23 mamlaka nchini Msumbiji ikiwa ni mwezi mmoja umepita tangu Msumbiji zilitangaza tahadhari ya uwezekano wa kutokea kimbunga hicho.

"Tutaendelea kufuatilia namna ambayo mfumo wa hali hiyo ya hewa unavyoendelea kuibuka na kujipanga kadri inavyotakiwa," Msemaji wa Taasisi ya Kupambana na Majanga wa nchi hiyo Paulo Tomás anaripotiwa kutoa kauli hiyo kwenye kikao kilichowashirikisha wataalamu kutoka idara za hali ya hewa, afya na ulinzi wa chakula za serikali ya Msumbiji.

Machi 14, baadhi ya maeneo ya Msumbiji, Malawi na Zimbabwe yalikumbwa na kimbunga Idai.

Kwa mujibu wa Kamati ya Dharura ya Majanga ya Uingereza watu 960 walipoteza maisha kutokana na athari za kimbunga hicho. Watu milioni tatu kwenye nchi hizo bado wanahitaji misaada ya kibinaadamu kama chakula, dawa, malazi na makazi.

Chanzo cha picha, TMA

Maelezo ya picha,

Ijumaa, Aprili 26 kunatarajiwa mvua kubwa, upepo mkali na mawimbi makubwa katika baadhi ya maeneo yenye mikoa ya Lindi na Mtwara.

Jumatatu Aprili 22, TMA ilitoa taarifa ya awali na kusema mgandamizo huo mdogo wa hewa katika eneo la kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar ulikuwa bado haujafikia hatua ya kimbunga.

Mamlaka hiyo pia ilitoa utabiri wa wiki nzima na kutahadharisha kuwa siku ya Ijumaa, Aprili 26 kunategemewa mvua kubwa, upepo mkali na mawimbi makubwa baharini katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Lindi na Mtwara.

"Tafadhali chukua hatua, uwezekano wa kutoke ni mkubwa na kiwango cha athari zinazoweza kutokea ni mkubwa," taarifa hiyo ya (TMA).