Kim Jong-un yuko nchini Urusi kukutana na rais Vladimir Putin

Shirika la kitaifa la habari, Korea Kaskazini ilimuoonesha Bw. Kim akiabiri treni yake ya kibinafsi

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Shirika la kitaifa la habari, Korea Kaskazini ilimuoonesha Bw. Kim akiabiri treni yake ya kibinafsi

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amewasili katika mji wa bandari wa Vladivostok nchini Urusi kwa mkutano wake wa kwanza kabisa na Rais Vladimir Putin.

Kremlin imesema kuwa viongozi hao watakutana mjinii Vladivostok siku ya Alhamisi na watazungumzia masuala ya usalama katika rasi ya Korea hasa "tatizo la nyuklia".

Kim anatafuta washirika wapya baada ya mazungumzo yake na rais wa Marekani Donald Trump kutibuka, wachambuzi wanasema.

Bw. Trump na Kim walikutana mjini Hanoi mapema mwaka huu kujadili mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini, lakini mkutano huo uliisha bila viongozi hao kukubaliana.

Tunafahamu nini kuhusiana na mkutano huo?

Vyombo vya habari vya Korea Kaskazini havijathibitisha wakati na mahali mkutano huo utakapofanyika.

Lakini bendera za Urusi na Korea Kaskazini tayari zinapepea sehemu fulani katika mji wa pwani wa Vladivostok nchini Urusi ambako mkutano huo unatarajiwa kufanyika.

Kiongozi wa Korea Kaskazini ameripotiwa kusafiri nchini Urusi siku ya Jumatano na kutoka ndani ya treni yake ya kibinafsi katika mji wa mpakani wa Khasan.

Alisalimiana na wanawake wa Urasi waliyokua wamevamilia nguo za kitamaduni kuashiria sherehe ya mapokezi yake.

Pande zote mbili zinataka nini?

Mkutano huu unachukuliwa na wengi kama fursa ya Korea Kaskazini kuonesha washirika wake wakuu baada ya mazungumzo yake ya nyuklia na Marekani kuvunjikamapema mwaka huu, anasema mwandishi wa BBC Laura Bicker.

Taifa hilo limemlaumu waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo kwa kuchangia kuvunjika kwa mkutano wa mwezi Februari mwaka huu.

Mapema mwezi huu Korea Kaskazini ilitaka Bw. Pompeo aondolewe katika mazungumzo ya nyulia baada ya kumlaumu kuwa "anazungumza upuzi" na kuomba mtu "makini zaidi" kuchukua nafasi yake.

Mkutano huo pia ni fursa kwa Pyongyang kuonesha hatma yake ya kiuchumi ya siku zijazo hategemei Marekani, mwandishi wetu aliongeza.

Bw. Kim huenda akaishinikiza Moscow kulegeza vikwazo dhidi ya taifa lake.

Chanzo cha picha, AFP/Getty

Maelezo ya picha,

Bendera za mataifa hayo mawili tayari zinapepe mjini Vladivostok

Wadadisi wanaamini mkutano huu utatoa fursa nzuri kwa Urusi kuonesha ushawishi wake katika rasi ya Korea.

Rais Putin amekuwa akisubiri kwa hamu kukutana na kiongozi wa Korea Kaskazini kwa muda mrefu.

Kremlin imeonekana kutengwa katika mikutano iliyopita ya Trump na Kim.

Urusi sawa na Marekani na Uchina inapinga wazo la Korea Kusini kuwa taifa lenye uwezo wa knuklia.

Maafisa wa ngazi ya juu wa Kremlin wanapania kuona hali ya taharuki inapunguzwa katika eneo la rasi ya Korea.

Mkuu wa sera sera za kigeni za Urusi Yuri Ushakov, amesema kuwa hali imetulia katika eneo hilo katika miezi ya hivi karibuni.

"Urusi ina mpango wa kusaidia kadiri ya uwezo wake kuimarisha uhusiano mzuri katika kanda hiyo," aliambia wanahabari siku ya Jumanne.

Urusi iliwahi kushirikishwa katika mazungumza ya mpango wa nuklia wa Korea Kaskazini.

Kiongozi wa zamani wa taifa hilo Kim Jong-il, alikutana na rais wa Urusi wa wakati huo Dmitry Medvedev mwaka 2011.

Kwa mujibu wa msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Korea Kusini ipo haja ya "kushauriana" kuhusu usalama wa rasi hiyo.

Korea Kaskazini imekuwa ikiendelea na shughuli zake za nyuklia.

Mapema mwezi Aprili taifa hilo lilidai kuwa limefanyia majaribio ''silaha yake mpya''- inayodhaniwa kuwa kombora la masafa mafupi.