Diamond Platinumz na Zari watupiana maneno kunani?

Daimond Platinumz

Nyota wa muziki nchini Tanzania Diamond Platinumz amedai kwamba mpenziwe wa zamani na mama ya watoto wake wawili Zari Hassan hakuwa mwaminifu kwenye uhusiano.

Nyota huyo wa wimbo 'Tetema' anadai kwamba mfanyibiashara huyo wa Uganda anayeishi nchini Afrika Kusini amedai kwamba alikuwa na uhusiano wa kando na msanii mmoja wa Nigeria.

Nyota huyo wa ''chibudi chibudee'' alitoa matamshi hayo katika kipindi cha radio ya Wasafi fm kwa jina 'Block 89'.

Hatahivyo Zari Hassan ambaye alikuwa na uhusiano na Diamond kwa kipindi cha miaka mitatu alijitokeza na kukana katu kwamba hakuwa mwaminifu.

Chanzo cha picha, Diamond/Instgram

Matamshi ya Diamond ni kinyume na sababu ambazo Zari alitoa kuhusiana na kuachana na Diamond Platinumz tarehe 14 mwezi Feb 2018.

Zari kwa upande wake wakati huo alimshutumu Diamond kwa kumuendea kinyume na wanawake tofauti akiwemo .

Diamond alikiri katika mahojiano hayo ya radio ya Wasafi kwamba madai hayo ya udanganyifu yalikuwa ya kweli , ijapokuwa anasema kwamba alilazimika kufanya hivyo kwa kuwa Zari alikuwa amekataa kuhamia Tanzania ili wawe pamoja.

''Kama kijana mdogo ambaye ni nyota na nina hisia nyingi , haiwezakani kwamba ningesubiri zaidi ya miezi mitatu bila kushiriki tendo la ngono.Nilikuwa tayari kumuanzishia Zari biashara nchini Tanzania , lakini akakataa kuondoka Afrika Kusini. Mulikuwa munatarajia nifanye nini'', aliuliza .

Mwanamuziki huyo vilevile alikiri kwamba alianza mahusiano na wanawake wengine kwa sababu alimtaka Zari aondoke katika maisha yake bila kumfukuza moja kwa moja.

Hatahivyo platinumz anakiri kwamba Zari alikuwa na tabia zote za ''mke mzuri'' na kunipenda zaidi ya alivyompenda.

Msanii huyo pia aliendelea kusema kuwa ni kweli madai aliyotoa Zari hapo awali kwamba miezi mengine hakutuma fedha za kuwalea watoto wake wawili kwa sababu Zari alimzuia kuwaona watoto wake.

''Alifunga kila njia ambazo ningetumia kuwasiliana na watoto. Na sasa ana mpenzi mwengine katika maisha yake; Siwezi kumpigia simu mara kwa mara nikimuomba kuwapatia wanangu simu nizungumze nao, mpenzi wake mpya atamfikiria vipi? Kwamba najaribu kumbembeleza arudi kitu ambacho sio kweli. Hiyo ndio sababu niliwacha kuwasiliana mara kwa mara na watoto. Hatahivyo nimemuandikia Zari nikimtaka aandike mahitaji yote ya kifedha ya watoto wangu na nitakuwa nikituma fedha moja kwa moja katika akaunti ya benki ya taasisi zote ambazo zinawapatia huduma'', alisema Diamond Platinumz.

Zari amekuwa akilalamika kwamba Diamond Platinumz ni baba asiyewaangalia wanawe ambaye hatoi usaidizi wowote kwa watoto wake.

Diamond hatahivyo anasema kuwa Zari anahisi uchungu baada ya kubaini kwamba amepiga hatua kimaisha na mwanadada wa Kenya Tanasha Oketch.