Man City yatungua Man United, Arsenal nao wabutuliwa na Wolves

ushindi

Chanzo cha picha, Reuters

Manchester City wamerejea kileleni mwa ligi ya England baada ya ushindi wa goli 2-0 dhidi ya mahasimu wao Manchester United.

Ushindi huo wa City umewafanya kukaa kileleni mwa ligi wakiwa na alama 89, wakiwazidi Liverpool kwa alama moja huku wakilinga idadi ya michezo wote wakiwa wamecheza jumla ya michezo 35.

Man City walipata magoli yao kupitia kwa Bernardo Silva aliyefunga goli la kwanza katika dakika ya 54 ya mchezo kisha winga Leroy Sane, aliyetokea benchi aliongeza goli la pili kwenye dakika ya 66.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Bernardo Silva aliyefunga goli la kwanza katika dakika ya 54

Licha ya kucheza Ugenini Manchester City waliutawala mchezo kwa asilimia kubwa huku wenyeji Man United wakiwa ndio wanahangaika bila kupata chochote..

Chanzo cha picha, Reuters

Nao washika mitutu wa London Arsenal wakicheza ugenini kwenye dimba la Molineux, walikubali kichapo kitakatifu cha goli 3-1 toka kwa Wolverhampton Wanderers.

Wolves wamejikita katika nafasi ya saba baada ya ushindi huo kwa kufikisha jumla ua alama 51 na wakisaliwa na michezo mitatu kabla ya ligi kumalizika.

Kiungo wa Kireno Ruben Neves ndie aliyeanza kuifungia timu yake goli la kuongoza kisha Matt Doherty akaongeza goli la pili, nae Diogo Jota akifunga goli la tatu.

Goli pekee la Arsenal liliwekwa kambani na mlinzi wake Sokratis Papastathopoulos, na licha ya kufungwa washika mitutu hao wanasalia katika nafasi ya wakiwa na alama 66.