Je, unaweza kufa kwa kuacha kupata kifungua kinywa?

Eggs on toast Haki miliki ya picha Getty Images

Mlo wa asubuhi ama kifungua au kiamsha kinywa wataalamu huuita "mlo wa muhimu zaidi wa siku".

Kwa mujibu wa tafiti iliyochapishwa nchini Marekani, mwezi Aprili, mlo wa asubuhi unaweza pia ukaokoa maisha yako.

Kutokupata kifungua kinywa kunahusishwa na hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa moyo na hatimaye kupelekea kifo.

Matokeo ya utafiti huo ulisimamiwa na jopo la madaktari kutoka vyuo vikuu mbali mbali nchini Marekani. Walichakata matokeo kutoka kwa watu 6,550 kati ya umri wa miaka 45 na 70 ambao walifanyiwa utafiti kati ya mwaka 1988 na 1994.

Watu hao walikuwa wakiripoti ni mara ngapi hawapati kifungua kinywa.

Haki miliki ya picha Getty Images

Kwa jumla, 5% ya washiriki waliripoti kuwa hawali kabisa mlo wa asubuhi, 11% hula mara chache na 25% walisema hula bila kukosa.

Watafiti baada ya hapo wakatathmini rekodi ya vifo vya washiriki mpaka mwaka 2011.

Washirirki 2,318 walikuwa wameshafariki kufikia mwaka huo, na watafiti wakaangazia uhusiano baina ya vifo na kifungua kinywa.

Baada ya kutoa sababu nyengine kama kuvuta sigara na unene, wataalamu wakabaini kuwa watu ambao walikuwa hawali mlo wa asubuhi walikuwa na hatari ya asilimia 19 kufa kwa magonjwa megine na asilimia 87 ya kufa kwa magonjwa ya moyo.

Angalizo

Tafiti za kitabibu tayari zimeshathibitisha kuwa kuacha kifungua kinywa kuna athari kwa afya, lakini wanasayansi bado wanaendelea kufanya tafiti kwenye eneo hilo.

Mamlaka ya Afya Uingereza (NHS) imesema utafiti huo bado "hauwezi kuthibitisha kwa yakini kuwa kuacha mlo wa asubuhi kunapelekea kifo kutokana na ugonjwa wa moyo."

Haki miliki ya picha Getty Images

"Watu ambao walikuwa hawapati kufungua kinywa (kwenye tafiti) inawezekana walikuwa wavuta sigara, walevi wa kiwango cha juu, wavivu, hawakuwa na lishe bora na ufinyu wa kipato kuliko wale ambao walikuwa wanapata kifungua kinywa," chapisho la NHS limeeleza.

"Tafiti imeangalia kipengele cha kifungua kinywa kwa wakati mfupi, hali ambayo yawezekana si tabia ya mtu kwa wakati wote wa maisha yake. Pia haiwezi kutubainisha kifungua kinywa kina maana gani kwa watu tofauti."

"Mfano, watu wengi hupata kifungua kinywa, lakini hutofautiana sana katika vile wanavyokula. Kuna ambao wanapata mlo kamili saa 2 asubuhi na wengine huonja tu kipande cha nyama au sharubati kwenye saa nne au tano asubuhi."

Hata hivyo, Dkt. Wei Bao, ambaye ni profesa msaidizi katika chuo kikuu cha Iowa na mwandishi mkuu wa matokeo ya utafiti huo ametetea kazi yao.

Haki miliki ya picha Getty Images

"Tafiti nyingi zimebainisha kuwa kuacha kupata kifungua kinywa kuna hatarisha kupata kisukari, shinikizo la damu na kolestro," Bao amesema.

"Utafiti wetu mwishowe unashauri kuwa, kupata kifungua kinywa ni njia nyepesi ya kutatua matatizo ya ugonjwa wa moyo."

Magonjwa ya moyo pamoja na kiharusi ni chanzo kikubwa cha vifo duniani. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) watu milioni 15.2 walipoteza maisha kutokana na matatizo hayo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii