Umoja wa mataifa unasema 'hali ni mbaya kuliko ilivyodhaniwa' nchini Msumbiji

Two people wade through rising floodwaters in Pemba, Mozambique after Cyclone Kenneth struck the African nation
Maelezo ya picha,

Takriban watu 700,000 wanahofiwa kuwa katika hatari

Hali kaskazini mwa Msumbiji ni mbaya kuliko ilivyodhaniwa, msemaji wa Umoja wa mataifa ameeleza, siku chache baada ya kimbunga Kenneth kutuwa nchini humo.

Kimbunga hicho kilituwa siku ya Alhamisi kwa upepo mkali wenye kasi ya 220km/h (140mph) kilichoviangamiza vijiji.

Takriban watu 700,000 sasa wanadhaniwa kuwa katika hatari katika eneo hilo wakati mvua kubwa ikiendelea kunyesha.

Pemba, mji mkubwa wa jimbo la Cabo Delgado kumeshuhudiwa mvua yenye kina cha mita mbili na mafuriko.

Msemaji katika ofisi ya uratibu wa masuala ya kibinaadamu (Ocha) Saviano Abreu ameeleza kwamba hali ni mbaya katika miji ya Macomia na Quissanga, akiongeza kwamba kuna wasiwasi pia kwa kisiwa kisichoweza kufikiwa cha Ibo.

Mawimbi ya hadi mita 4 yanatarajiwa, na mashirika ya misaada yanahofia kwamba mvua itazidi kunyesha.

"Tuna wasiwasi mkubwa kwasababu, kwa mujibu wa utabiri wa hali ya hewa, mvua nzito inatarajiwa kunyesha katika siku nne zijazo," Deborah Nguyen, msemaji wa shirika la mpango wa chakula la Umoja wa mataifa , alieliambia shirika la habari la AFP.

"Tunatarajia mvua iwe na ukubwa wa mara mbili zaidi ya ilioshuhudiwa wakati wa kimbunga Idai," ameongeza.

Kimbunga Idai kilisababisha vifo vya watu 900 katika nchi tatu mnamo Machi mwaka huu.

Maelezo ya video,

Hali ilivyo Mtwara baada ya Kimbunga Kenneth kuisha nguvu Msumbiji

Ni yapi yanayojiri?

Inadhaniwa kwamba watu 400,000 wanaishi Pemba , na mvua kubwa imesababisha watu wengi kuwa katika hatari.

Kuna wasiwasi unaotokana na maporomoko ya ardhi katika mtaa wa Mahate mjini humo, maafisa wa Ocha katika eneo hilo wanasema, na katika mtaa wa Natite, nyumba zimeanza kuporomoka.

Shirika la mpango wa chakula duniani linaarifiwa kuanza kutoa misaada kwa watu waliokwama, lakini barabara zilizoharibika zimesababisha shughuli zisitishwe katika maeneo yaliotengwa sana.

Takriban watu watano wamefariki kutokana na kimbunga hicho na takriban nyumba 35000 zimeharibika vibaya au kubomoka kabisa, maafisa wa kitaifa wanasema.

Maelezo ya picha,

Mafuriko yamesababisha uharibifu kwa miundo msingi na kutatiza juhudi za kuwasilisha misaada

Mashirika ya Umoja wa mataifa yanasaidia maafisa wa serikali na bwana Guterres ametoa wito wa "rasilmali za ziada" kutoka jumuiya ya kimataifa "kufadhili usaidizi wa sasa, wa siku zijazo na wa kipindi kirefu zaidi".

Eneo lililoathirika liko vipi?

Jimbo la Cabo Delgado halina watu wengi kama eneo lililoathirika na kimbunga Idai na inavyoonekana sehemu kubwa iko katika ardhi ya juu.

Hilo kwa pamoja na tahadhari za mapema kutoka kwa maafisa husika kabla ya kutokea kimbunga hicho huenda ikasaidia kuzuia hasara ikilinganishwa na wakati wa kimbunga Idai.

Lakini taarifa zinasema maelfu ya makaazi yameharibiwa kutokana na upepo mkali, na ene hilo limekabiliwa na mashambulio ya wanamgambo wenye itikadi kali za dini ya kiislamu katika miezi ya hivi karibuni, jambo ambalo linaonekana huenda likatatiza utoaji wa msaada.

Tayari maelfu ya watu walikuwa wametoroka makaazi yao kutokana na ghasia kutafuta hifadhi katika kambi za kuwahifadhi watu walioachwa bila ya makaazi.