Shambulio Sri Lanka: Mavazi yanayofunika uso marufuku baada ya mashambulio ya Pasaka

Sri Lankan Muslim women in Colombo, 2013 Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Marufuku imeidhinishwa, lakini hakuna ufafanuzi wa iwapo ni niqab au burka

Sri Lanka imepiga marufuku watu kujifunika uso hadharani kufuatia mashambulio ya kujitoa muhanga katika sikukuu ya Pasaka yaliosababisha vifo vya watu 250 na mamia wengine kujeruhiwa.

Rais Maithripala Sirisena amesema anatumia sheria ya dharura kuidhinisha marufuku hiyo kuanzia leo Jumatatu.

Kitambaa chochote kinachofunika "na kuzuia mtu kutambulika " kitapigwa marufuku kuhakikisha usalama, ofisi yake imeeleza. Viongozi wa dini ya kiislamu wameshutumu uamuzi huo.

Niqab na burka - mavazi yanayovaliwa na wanawake wa kiislamu - hayakutajwa kama ndiyo yaliodhamiriwa marufuku hiyo.

Hatahivyo, hatua hiyo inachukuliwa kupinga mavazi hayo.

Sri Lanka inasalia kuwa katika tahadhari kubwa siku nane baada ya mashambulio ya itikadi kali za dini ya kiislamu dhidi ya makanisa na hoteli nchini humo.

Baadhi ya washukiwa wamekamatwa, lakini maafisa nchini wanaonya kwamba wanamgambo zaidi wangali kukamtwa.

Tofauti kati ya vazi la niqab na burka

Image caption Niqab
Image caption Burka

Ni watu wangapia walioathirika?

Sri Lanka ina kiasi wastani cha waislamu walioishi nchini humo kwa karne kadhaa - kati ya watu milioni 21, ni chini ya 10% walio waislamu.

Ni kiwango kidogo cha waislamu wanaodhaniwa kuvaa mavazi hayo ya kufunika uso niqab, au burka.

Wiki iliyopita mbunge mmoja nchini humo alipendekeza marafuku ya vazi la burqa kwa wanawake akieleza kwamba linapaswa kupigwa marufuku kwa misingi ya usalama.

Muungano wa viongozi wa dini ya kiislamu Jamiyyathul Ulama, imeshutumu vikali uamuzi huo wa rais.

" Ni jambo la kipumbavu, siku tatu zilizopita tulitoa uamuzi wa hiari kuhusu hili. Jamiyyathul Ulema iliwaambia wanawake wa kiislamu wasifunike nyuso zao kwa masuala ya usalama. Na iwapo wanataka kufanya hivyo, basi waliambiwa wasitoke nje," anaeleza Hilmy Ahmed, makamu wa rais wa kundi hilo.

Mwishoni mwa juma maelfu ya wanajeshi wa Sri Lanka walisimama wima mitaani wakilinda makanisa na misikiti.

Misa nyingi za kanisa hazikufanyika, lakini waumini walikusanyika na kusali nje ya eneo tukufu la St Anthony lililoharibika vibaya baada ya mashambulio hayo.

Siku ya Ijumaa baba na kaka zake mtuhumiwa anayedhaniwa kuratibu mashambulio hayo, Zahran Hashim, waliuawa katika operesheni ya vikosi vya usalama.

Hashim, aliyejilipua katika hoteli moja huko Colombo, alilianzisha kundi lenye itikadi kali za dini ya kiislamu, NTJ, ambalo maafisa wanasema limehusika na mashambulio haya.

Haki miliki ya picha Getty Images

Ni mataifa gani mengine yaliopiga marufuku Niqab na Burka?

Sheria za kupiga marufuku mavazi ya kiislamu kama burka na Niqab zimeidhinishwa katika baadhi ya mataifa duniani.

Katika eneo la Afrika mashariki, wanawake waislamu nchini Rwanda, wamepigwa marufuku wasijifunike nyuso zao.

Hatua hii ilichukuliwa na jumuiya ya waislamu nchini humo mnamo 2016 iliyofikia uamuzi wa kuipiga marufuku Niqab inayovaliwa na wanawake.

Jumuiya hiyo ilisema marufuku hiyo inatokana na sababu za kiusalama kwa waislamu na vilevile waRwanda.

Jamuhuri ya Congo- Brazaville ilipiga marufuku vazi la Niqab mnamo 2015 katika maeneo ya umma katika inachoeleza kuwa ni kukabiliana na ugaidi.

Mnamo 2017 Serikali ya Austria iliidhinisha sheria ambayo inaeleza kwamba ni lazima uso uonekane katika kulinda tamaduni za Austria.

Ufaransa na Ubelgiji zilipiga marufuku vazi la burka mwaka 2011 na hatua kama hiyo, au mapendekezo ya sheria yamewahi kujadiliwa katika nchi nyinginezo duniani.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii