Yafahamu mambo ambayo rais John Magufuli anayatamani

Magufuli

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli ni mtu anayependa kutekeleza kile asemacho, ni mtu anayepambwa na sifa ya uthubutu.

Lakini, Magufuli pia ni mwanandamu mwenye matamanio, yapo ambayo kayasema hadharani na mengine yamo moyoni mwake hayajulikani.

Jumapili, Magufuli amefichua moja ya vitu ambavyo alikuwa akivitamani wakati akikua na kushindwa kuvifikia.

Akiwa katika ibada ya kusimikwa kwa askofu mpya wa Kanisa Katoliki mkoani Mbeya, askofu Gervas Nyaisonga Jumapili Aprili 28 Magufuli amesema alitamani kuwa padri au askofu.

"Nakumbuka nikiwa mdogo nilitamani sana kuwa padri au hata askofu, lakini kwa bahati mbaya sana sijui hata nini kilinitokea nikashindwa kuwa hata katekista. Nimeshindwa hata kuwa mwenyekiti wa jumuiya," amesema na kuongeza, "…nikawa najiuliza nimekosea wapi, yangekuwa masharti (ya kuwa padri) yanalegezwa, basi ningemuomba askofu Nyaisonga niwe padri nihubiri neno la Mungu."

Malaika kuzima mitandao

Septemba 28, 2016 rais Magufuli alionesha wazi kuwa anachukizwa na habari za uzushi mitandaoni na ugumu uliopo wa kuzidhibiti.

Akizungumza katika hafla ya kupokea ndege mbili za Bombardier kutoka Canada, alisema anatamani malaika washuke na kushughulikia mitandao hiyo.

Jambo liloonekana kumkera Magufuli ni juu ya bei ambayo ilikuwa ikisemwa mitandaoni serikali imetumia kununua ndege hizo.

"Mtu mwingine anasema ndege hizo tumezinunua kila ndege dola milioni 61 wakati mimi najua ndege moja haikufika hata nusu ya hiyo bei, na anapost (anachapisha) pale anaandika uongo, halafu hata akishajua ukweli wake baadaye wala hatubu," alisema na kuongeza, "Nilikuwa natamani siku moja malaika washuke waizime hii mitandao yote ili baada ya mwaka mzima itakapokuja kufunguka wakute sisi tumeshatengeza Tanzania yetu mpya, wanapost (wanachapisha) vitu vingine vya ovyo, wanasema no research no right to speak, (bila utafiti huna haki ya kuzungumza)."

Maelezo ya picha,

Magufuli akiongoza mapokezi ya ndege mbili za Bombardier Septemba 2016

Kuwa mkuu wa polisi

Si jambo la kawaida kumsikia mkuu wa nchi kufanya kazi fulani ambayo kimamlaka iko chini yake, lakini Magufuli ameshawahi kusema anatamani kuwa mkuu wa polisi.

Aliyasema hayo ikulu mwezi Februari 2017 akioneshwa kutoridhishwa kwake na utendaji wa jeshi la polisi nchini Tanzania.

Kipindi hicho kulikuwa na operesheni dhidi ya walanguzi wa dawa za kulevya iliyokuwa chini ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda.

Kati ya watu ambao waliitwa afisi kuu ya polisi jijini Dar es Salaam kuhusiana na sakata hilo alikuwa askofu Josephat Gwajima na aliyekuwa mwenyekiti wa klabu ya Yanga Yusuf Manji.

Wawili hao walisindikizwa na makundi ya wafuasi wao, mashabiki wa Yanga walilifuta gari la Manji huku wanakwaya wa Gwajima wakiimba nje ya kituo cha polisi.

Kufurika kwa wafuasi hao na polisi kutowatawanya kulimkera Magufuli.

" Mtu (Gwajima) anakwenda hapo (polisi) kwani mliambiwa manataka kuimbiwa mapambio? Unajuwa vyombo vyetu (vya usalama) saa nyengine vinakuwa…I wish I could be IGP (natamani ningelikuwa Mkuu wa Polisi)," alisema Magufuli.