Papa Francis awataka wahudumu wa saluni kuacha udaku

Papa Francis Haki miliki ya picha Reuters

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis hii leo amekutana na wasusi, wanamitindo na wataalam wa mitindo ya ulimbwende mjini Vatican, lakini akawaonya dhidi ya kuwa na udaku ama umbea wakati wakiwa wanaendesha shughuli zao za kikazi.

Papa Francis amewataka wahudumu hao wa saluni kufanya kazi zao kwa njia ya Kikristo na kuwatendea wateja wao kwa heshima na upole.

"Kila wakati ongeeni na wateja wenu kwa unyenyekevu na muwape matumaini katika maisha," amesema Papa na kuongeza; "mjitahidi kujizuia na vishawishi vya kuanziasha maongezi ya udaku ambayo ni rahisi kufanyika katika mazingira ya kazi yenu."

Papa amewataka wahudumu hao kuiga tabia njema za mtakatifu na mlezi wa waumini wa kanisa hilo wanaojihusisha na masuala ya urembo, Martino de Porres, aliyeishi Peru katika karne ya 16.

De Pores aliishi jijini Lima na alikuwa kinyozi shughuli ambayo kwa kipindi hicho ilihusisha pia kufanya upasuaji wa kukata viungo.

Mtakatifu huyo anatajwa kufanya miuziza kadhaa ikiwemo kutibu kwa haraka, kuongea na wanyama, kuwa sehemu mbili kwa wakati mmoja na kunyanyua watu juu bila ya kuwashika.

"Kila mmoja wnu, akiwa kazini anaweza kufanya majukumu yake kwa weledi na kutoa mchango chanya kwa maendeleo ya jamii," amesema Papa.

Haki miliki ya picha Getty Images

Mara nyingi wahudumu wa saluni wamekuwa wakikashifiwa kwa kutumia muda mrefu kusengenya pamoja na wateja wao, na kupiga domo tu.

Lakini je hilo lina ukweli? mwandishi wa BBC Lizzy Masinga amemuuliza swali hilo Asnath Mwalukunga, anayemiliki Asnath Salon jijini Dar es Salaam na kusema: "kuna ukweli kiasi chake katika hilo lakini si kweli kuwa wahudumu wote ni wambea. Mimi huwakataza wafanyakazi wangu kuanzisha mada za udaku na kusengenya watu. Lakini nashindwa kufanya hivyo kwa wateja wangu. Naheshimu wateja, sitaki kuwapoteza."

Bi Mwalukunga, amedai kuwa watu huwa wanatumia muda mwingi kupata huduma saluni na ndio maana kunakuwa na uwezekano wa mazungumzo mbalimabli kushamiri.

"Huwezi kukaa kimya kwa saa tatu huku unamhudumia mteja. Lakini si lazima kuanzisha gumzo la umbe ana udaku," amesema.

Mada zinazohusiana