Je ni nini chanzo cha rushwa ya 'ngono' katika vyuo vikuu Afrika Mashariki?

Mwanafunzi Haki miliki ya picha Getty Images

Madai ya rushwa na ngono yamekuwa yakigusa vyuo vikuu mbalimbali katika nchi za Afrika Mashariki.

Kumekuwa na tuhuma kuwa baadhi ya wanachuo wa kike wanalazimika kutoa rushwa ya ngono ili waweze kufaulu masomo yao.

''Vishawishi tunapata kwa wahadhiri wenyewe'' anasema Nasra Swai mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha USIU jijini Nairobi.

Lakini swali ni je ni nini hasa chanzo cha rushwa hii ya ngono vyuoni?

Wahadhiri wamekuwa wakilaumiwa kwa kuwanyanyasa kijinsia wanafunzi wa kike kwa kuwaomba rushwa ya ngono au kuwajengea mazingira ya kuwataka kimapenzi kwa nguvu.

Lakini Paul Mabuga, ambaye ni Mhadhiri wa wa zamani, Mwandishi wa Habari na mkereketwa anayefuatilia kwa karibu masuala ya Elimu anapinga hoja hayo.

''Hili ni suala la ugavi na utashi, kwamba kuna mmoja ana bidhaa inahitajika sokoni alafu kuna mwingine anauhitaji wa hiyo bidhaa. Kwa hivyo wakati mwingine inafikia hali fulani ambapo watu hawa wanakutana kwenye pointi moja ya kwamba huyu anahitaji alama darasani ili kusudi awe na ufaulu mzuri na ajenge maisha yake na mtu mwingine ni mtoaji wa hizo alama'' anasema Bw. Mabuga.

Haki miliki ya picha Getty Images

Anaongezea kuwa hiyo ndio sababu wakati fulani mkataba huo haramu unafanyika na wakati mwingine inakuwa vigumu sana kufahamu namana gani mkataba huo unavyotekelezwa kwasababu mtoaji ana maslahi fulani na mpokeaji nae ana maslahi fulani.

Pia anasema hilo ni tatizo ambalo ni vigumu sana kuthibitishwa kama yalivyo makosa mengine.

Kwa upande mwingine,wanafunzi wa kike vyuoni nao wanalaumiwa kwa kutumia jinsia yao kama kishawishi cha kuwatega wahadhiri wa kiume kwa lengo la kupata alama bora.

''Mbona utafute alama za bure, kwanini usisome vizuri na ukubali matokeo ambayo utapata?'' anauliza Mwanasikolojia Grace Destiny.

Anasisitiza kuwa wanafunzi wasipojiuliza maswali hayo watasalia kupoteza hadhi yao na ndio maana baadhi yao wanajipata wakiendekeza tabia hiyo, na kwasababu ya kutojiheshimu,wanajiuliza maswali ya kupotosha kama vile ''Nitapoteza nini nikilala na mwalimu huyu''.

Haki miliki ya picha Getty Images

Bi Grace anasema kuwa suala la kutojipenda, kutojiamini na kutojiheshimu ndio mambo yanachangia rushwa ya ngono kwa wanafunzi wa kike.

Kwa upande wa wahadhiri wanaowajengea mazingira ya kuwataka kimapenzi wanafunzi wa kike Bi Grace anawashauri kuwachukulia kama baba zao wasichana hao.

Bi Grace anaelewa kuwa mazingira ya sasa yamezorota kimaadili lakini ni vyema kuzingatia mambo kama vile mtu alikotoka na kule alikozaliwa.

''Msichana aliliyelelewa bila baba huwa amekosa mapenzi ya baba na anapokuja kwako wewe mhadhiri anatarajia usaidizi wa kisaikolojia zaidi na wala haji kwako wa ajili ya mapenzi'' alisema.

''Nawaomba wa waadhiri wasichukue nafasi hiyo kuwanyanyasa kingono wasichana hao'' Grace alitilia mkazo hoja yake.

Haki miliki ya picha Getty Images

Lakini mmoja wa wanajopo waliyochangia mjadala wa Amka na BBC anasema ni rahisi sana kwao kushawishika kwa sababu mhadhiri akiwangalia na jicho la matamanio anakua vigumu kumkatalia.

''Wewe Hata kama umelelewa katika maadili mwalimu akikuangalia na jicho la matamanio umkatae atakufelisha alafu hasara itakuwa kwa nani?''anauliza Nasra Swai mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha USIU jijini Nairobi.

Wanajopo wote watatu wamekubaliana kuwa ipo haja ya wasichana kupaza sauti wanapojipata katika hali ya kunyanyasika kimapenzi.

Japo taasisi nyingi za elimu ya juu katika Kanda ya Afrika Mashariki zimechukua hatua ya kuzuia ukiukwaji huu wa maadili, ikiwamo kuanzisha kanuni za maadili ya wafanyakazi, kutunga sheria ndogondogo za wanachuo na kuwa na sera ya jinsia,Kama sehemu mojawapo ya kupambana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia bado hali hii bado inaendelea kushuhudiwa.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii