Tume ya mawasiliano Uganda yaamuru wanahabari wafutwe kwa kukiuka maadili

Rais wa Uganda Yoweri Museveni Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais wa Uganda Yoweri Museveni

Tume ya mawasiliano ya nchini Uganda imeagiza kufungwa kwa vituo 13 vya radio na Televisheni pamoja na kufutwa kazi baadhi ya wanahabari kwa ''kupotoshaji' na kuchochea ghasia kwa kutangaza taarifa zilizo na "ujumbe na hisia kali".

Tume hiyo inasema kuwa vyombo hivyo vya habari vilikiuka kanuni ya kifungo cha 31 ibara ya 4 ya sheria ya mawasiliano ya Uganda ya mwaka 2013.

Japo kuwa haikufafanua jinsi sheria hiyo ilivyokiukwa katika agizo lake kwa vyombo hivyo vya habari ikiwa ni pamoja na - Vituo vya televisheni vya NBS, Bukedde TV, NTV, CBS FM na Capital FM.

Inataka hatua dhidi ya wazalishaji vipindi, wahariri wa kuu na wasimamizi wa matangazo kusimamishwa kazi katika mda wa siku tatu.

"Hii ni kufuatia jinsi zinavyoshughulikia mada zinazopeperushwa hewani wakati wa matangazo ya moja kwa moja, Habari za hivi punde na Habari zingine kwa ujumla bila kuzingatia kanuni ," iliongeza Tume ya UCC.

Hatua hiyo imepokelewaje?

Chama cha wanahabari nchini Uganda (UJA) kimeelezea kughadhabishwa na hatua hiyo.

''Wanahabari karibu 30 wanakabiliwa na tishio la kufutwa kazi na hili litakuwa na athiri kwa taalumu zao tu bali mamilioniya waganda watakosa huduma ya kupashwa habari'' alisema taarifa ya chama hicho.

UJA pia iliongeza kuwa serikali kupitia mashirika yake ya udhibiti wa mawasiliano inatakiwa kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari.

Kuna madai kuwa huenda hiyo imetokana na mtangazo ya moja kwa moja ya kukamatwa na kushtakiwa kwa mbunge wa Kyadondo Mashariki, Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine.

Kyagulanyi kwa sasa anazuiliwa rumande na anatarajiwa kufikishwa tena mbele ya hakimu mkuu wa mahakama ya Buganda Road leo Alhamisi.

Haki miliki ya picha Getty Images

Baadhi ya watu pia wanasema hatua hiyo inaaleta taswira mbaya ya Uganda wakati Ulimwengu unapojiandaa kuadhimisha siku ya kimatifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.

Tume hiyo imedai kuwa iliwahi kutoa onyo kuhusiana na suala hilo lakini baadhi ya vyombo vya habari havikutilia maanani onyo hilo.

''Vituo vitakavyo puuza agizo letu vitachukuliwa hatua zaidi ya kinidhamu''

Pia imeongeza kuwa imeanzisha uchunguzi kuhusiana tuhuma iliyoibua dhidi ya vituo hivyo na baadhi ya wafanyikazi wake.

Mamlaka nchini Uganda imekuwa ikijaribu kuzima umaarufu wa mwanamuziki na mbunge wa upinzani kwa kuvilazimisha vyombo vya habari kutomuangazia.

Umaarufu wa Bobi Wine umemfanya kuonekana na waganda wengi kama tishio kwa utawala wa rais Yoweri Museveni ambaye huenda akagombea tena urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2021 - miaka 35 tangu aingia madarakani.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii