Afrika Kusini: Pengo kati ya maskini na matajiri linazidi kuongezeka?

A man walks past an ANC election poster in Johannesburg

Raia Afrika Kusini wanapojiandaa kupiga kura 8 Mei kuwachagua viongozi wapya, pengo kati ya maskini na matajiri limesalia kuwa suala kuu kwenye kampeni.

Ndilo taifa lililoendelea zaidi kiviwanda barani Afrika - lakini pia ni moja ya mataifa yasiyo na usawa zaidi duniani.

Vyama vya upinzani vinasema hali imekuwa baya zaidi chini ya utawala wa chama cha ANC ambacho kimeongoza taifa hilo kwa robo karne sasa.

Je, kuna ukweli wowote katika madai hayo? BBC Reality Check imedadisi hilo.

Utapimaje ukosefu wa usawa?

Kipimo kinachotumiwa zaidi na wachumi katika kukadiria kiwango cha ukosefu wa usawa katika jamii hufahamika kama kipimo cha Gini. Ni kipimo kinachoangazia mapato ya mtu, na huwa kati ya 0 na 1, ambapo 1 ndiyo hali ambayo hakuna usawa kabisa. Wakati mwingine asilimia hutumiwa, ambapo jamii isiyo na usawa kabisa itakuwa na kipimo cha asilimia 100.

Kipimo hiki huwa hakiwezi kuonyesha uhalisia kabisa lakini ni kiashiria ambacho kinaweza kutumiwa kukadiria hali ilivyo Afrika Kusini na katika mataifa mengine.

Kiwango cha ukosefu wa usawa Afrika Kusini kiko juu

Kiwango cha Gini

Takwimu za 2014 bila Namibia (2015) na US (2013)
Chanzo: takwimu za Benki ya Dunia

Kwa kutumia kipimo hiki na takwimu za Benki ya Dunia, Afrika Kusini ndilo taifa lenye kiwango cha juu zaidi cha ukosefu wa usawa duniani. Kipimo cha Afrika Kusini ni zaidi ya asilimia 60.

Ndiyo nchi pekee pamoja na Haiti iliyopitisha asilimia 60 kwenye kipimo hicho.

Nchi jirani Namibia na Msumbiji zinaifuata karibu. Brazil ni taifa jingine pia lililonawiri kiviwanda lakini lililo na kiwango cha juu cha ukosefu wa usawa.

Ukichunguza hali tangu ANC ilipoingia mamlakani mwaka 1994, kiwango cha ukosefu wa usawa kilipanda kwa miaka kadha na kufikia kiwango cha juu zaidi mwaka 2005.

Baadaye haya hivyo, hali haijabadilika sana.

Kiwango cha ukosefu wa usawa hakijabadilika sana

Kiwango cha Gini

Chanzo: Takwimu za Benki ya Dunia

Kwa hivyo, kwa kutumia takwimu za Gini, wakosoaji wa serikali ya ANC wako sahihi kusema kwamba kiwango cha ukosefu wa usawa Afrika Kusini kimesalia kuwa juu sana.

Lakini hawako sahihi kusema kwamba hali inaendelea kuwa baya zaidi, ukitumia takwimu kutoka kwa mwongo mmoja uliopita.

Kupungua kwa ukuaji wa uchumi

Kwa miaka kadha baada ya ANC kuingilia madarakani, Afrika Kusini ilipiga hatua katika kupunguza umaskini na kutoa huduma za msingi kwa raia.

Juhudi hizi zilisaidiwa na ukuaji wa kuridhisha wa uchumi wa nchi hiyo, lakini katika miaka ya karibuni kasi ya ukuaji wa uchumi imepungua.

Matokeo yake ni kwamba kwa jumla mapato ya raia wengi Afrika Kusini yamekuwa yakipungua tangu 2010.

Kiwango cha ukosefu wa ajira kimeanza kupanda

Chanzo: Benki ya Dunia

Kiwango cha ukosefu wa ajira pia kimepanda katika kipindi hicho.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Democratic Alliance, Mmusi Maimane, anasema pengo kati ya "walio ndani ya mfumo wa uchumi na walio nje" limeongezeka.

"Hakuna dalili kwamba pengo hili litapungua. Ni taifa lililogawanyika kuwili," anasema.

Na Nkosazana Dlamini-Zuma, ambaye ni waziri serikalini Afrika Kusini anasema kiwango cha ukosefu wa usawa Afrika Kusini kimesalia kuwa juu mno.

Umaskini umeongezeka?

Kwa kutumia kipimo cha serikali ya Afrika Kusini kuhusu umaskini - ambacho kwa kawaida maskini huchukuliwa kuwa anayepata chini ya $55 (£42) kwa mwezi - takwimu rasmi zinaonyesha kwamba kati ya 2006 na 2011 kiwango cha walio maskini kilishuka kutoka 51% hadi 36.4%.

Lakini kufikia 2015, kiwango hicho kilikuwa kimepanda tena na kufikia 40%.

"Kwa jumla, maskini hawajafaidika sana kutokana na ukuaji wa kiuchumi," anasema Carlene van der Westhuizen, mchumi wa Afrika Kusini ambaye ameandika ripoti iliyochapishwa na taasisi ya Brookings Institution kutoka Marekani.

Haki miliki ya picha AFP

Tofauti kutokana na ajira zilichangia zaidi ukosefu wa usawa Afrika Kusini kati ya 2006 na 2015 kwa mujibu wa ripoti ya pamoja ya Benki ya Dunia na serikali ya Afrika Kusini.

"Kupata kiwango cha juu cha elimu na kuwa nafasi ya kazi ni vitu viwili muhimu vinavyohusika kuamua iwapo familia itakuwa thabiti kiuchumi," ripoti hiyo inasema.

Serikali imekuwa na mfumo wa kusaidia maskini ambapo maskini hupokea pesa za kujikimu kutoka kwa serikalini.

Ripoti hiyo inasema mpango huo umesaidia sana kupunguza idadi ya maskini wa kupindukia, lakini kuna wasiwasi kwamba huenda serikali isipate pesa za kutosha za kuendeleza mpango huo kwa kipindi kirefu.

Ni nani walioathirika zaidi?

Idadi kubwa ya watu weusi Afrika Kusini wamekuwa wakiishi katika umaskini ukilinganisha na watu wa asili ya Asia na Wazungu.

Na kati ya mwaka 2011 na 2015, kiwango cha watu weusi na watu wa asili mchanganyiko ambao wanaishi katika umaskini kimeongezeka, kwa mujibu wa takwimu za serikali.

Umasiki na asili Afrika Kusini

Asilimia ya wanaoishi katika umaskini

Chanzo: Idara ta takwimu Afrika Kusini

Raia Wazungu wanaoweza kufanya kazi ni asilimia 10 - lakini huwa kwa pamoja wanalipwa karibu mara tatu zaidi ya pesa wanazolipwa watu weusi Afrika Kusini ambao ni karibu robo tatu ya wafanyakazi nchini humo.

Ingawa mishahara kwa watu wa asili zote imeongezeka, wanaopata mapato ya wastani wamekosa kufaidi zaidi baada ya kuondolewa kwa utawala wa ubaguzi wa rangi.

Mishahara ya watu wanaolipwa mishahara ya juu zaidi imeongezeka kwa kasi mara dufu ya kasi ambayo mishahara ya watu wa kipato cha chini zaidi inaongezeka nayo kwa mujibu wa Benki ya Dunia.

Na kiwango cha mapato ambacho watu asilimia 1 matajiri zaidi wanapata Afrika Kusini kiliongezeka mara dufu katika miaka 20 baada ya mwaka 1994, na kufikia kiwango cha mishahara wanacholipwa watu matajiri zaidi Marekani.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii