Uhuru wa vyombo vya habari: Upi mustakabali Afrika Mashariki?

Vyombo vya habari

Leo ni siku ya kimataifa ya kusherehekea Uhuru wa Vyombo vya Habari, lakini kwa Afrika Mashariki bado kuna changamoto lukuki ambazo zinaitandazia giza siku hii.

Jumatano, Mei Mosi 2019, mamlaka nchini Uganda zilitoa mai ambayo bila shaka inaangazia ni kwa namna gani uhuru wa vyombo vya habari nchini humo na ukanda mzima wa Afrika Mashariki ulivyo mashakani.

Amri iliyotolewa na Tume ya Mawasiliano ya Uganda (UCC) imeagiza vituo 13 vya radio na Televisheni kuwafuta kazi ndani ya siku tatu waandishi waandamizi 39 kwa kutoa habari zilioitwa kuwa ni za ''kiupotoshaji' na kuchochea ghasia kwa kutangaza taarifa zilizo na "ujumbe wenye hisia kali".

Tume hiyo inasema kuwa vyombo hivyo vya habari vilikiuka kanuni ya kifungu cha 31 ibara ya 4 ya sheria ya mawasiliano ya Uganda ya mwaka 2013.

Japo kuwa haikufafanua jinsi sheria hiyo ilivyokiukwa katika agizo lake kwa vyombo hivyo vya habari ikiwa ni pamoja na - Vituo vya televisheni vya NBS TV, BBS TV, NTV, Bukedde TV, Kingdom TV na Salt TV. Vituo vya redio vilivyoangushiwa rungu hilo ni Akaboozi,Beat FM, Capital FM, Pearl FM, Sapientia FM and Redio Simba.

Inataka hatua dhidi ya wazalishaji vipindi, wahariri wa kuu na wasimamizi wa matangazo kusimamishwa kazi katika mda wa siku tatu.

"Hii ni kufuatia jinsi zinavyoshughulikia mada zinazopeperushwa hewani wakati wa matangazo ya moja kwa moja, Habari za hivi punde na Habari zingine kwa ujumla bila kuzingatia kanuni ," iliongeza Tume ya UCC.

Duru ndani ya Uganda zinaainisha kuwa huenda hatua hiyo imetokana na matangazo ya moja kwa moja ya kukamatwa na kushtakiwa kwa mbunge wa Kyadondo Mashariki, Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine.

Wakati huo huo mabalozi kutoka nchi wanachama wa Muungano wa Ulaya, Marekani na nchi nyingine 14 wamelaani hatua ya serikali ya uganda kubana uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa waaandamanaji baada ya kukamatwa kwa mwanamuziki maariufu aliyegeuka kuwa Mbunge Bobi Wine.

"Tunahofia sana msururu wa matukio ya hivi karibuni yanayozuwia uhuru w akujieleza na uhuru wa kukusanyika nchini Uganda," ilisema taarifa ya pamoja ya wanadiplomasia hao na kuongeza kuwa

"Tunawasiwasi na matumizi ya nguvu kupita kiasi zinazotumiwa na polisi na vya polisi na huduma za usalama dhidi ya waandamanaji na wanasiasa wa upinzani ,".

Kyagulanyi ameachiwa kwa dhamana na mahakama mjini Kampala japo kwa masharti makali.

Chama cha wanahabari nchini Uganda (UJA) kimeelezea kughadhabishwa na hatua hiyo.

''Wanahabari karibu 30 wanakabiliwa na tishio la kufutwa kazi na hili litakuwa na athari si kwa taaluma zao tu bali mamilioni ya waganda watakosa huduma ya kupashwa habari'' ilisema taarifa ya chama hicho.

UJA pia imeitaka serikali kupitia mashirika yake ya udhibiti wa mawasiliano inatakiwa kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari.

Yu wapi Azori Gwanda?

Image caption Februari 2018 zilitimia siku 100 toka kutoweka kwa Gwanda katika mazingira ya kutatanisha. Mpaka leo bado hajapatikana.

Nchini Tanzania changamoto za kuminywa kwa uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari bado zi lukuki.

Mwishoni mwa mwezi Machi, Mahakama ya ya Afrika Mashariki (EACJ) ilitoa hukumu kuwa baadhi ya vipengele katika Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 inakiuka uhuru wa kujieleza pia vinapingana na Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambao Tanzania imeuridhia.

Kesi hiyo ilifunguliwa mwaka 2017 na Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) wakilalamikia sheria hiyo kwa ukandamizaji wa uhuru wa habari.

Lakini, ni dhahiri kuwa itachukua muda na mapambano zaidi ya kisheria mpaka mabadiliko hayo yaliyopendekezwa na EACJ kufanyiwa kazi. Tayari serikali ya Tanzania imeweka wazi nia yake ya kukatia rufaa uamuzi huo katika mahakama hiyo ya EACJ.

Shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka (RSF), limetoa ripoti yake mpya mwezi Aprili ikionesha Tanzania imeporomoka kwa nafasi 25 katika orodha ya uhuru wa vyombo vya habari duniani.

Tanzania imeporomoka hadi nafasi ya 118 kwa mwaka 2019 kutoka 93 mwaka 2018 kati ya nchi 180 zilizofanyiwa tathmini.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo mamb yaliyochangia Tanzania kuporomoka kwa kiwango hicho ni, sheria kandamizi za habari, tukio la kuvamiwa kwa Clouds Media Group mwaka 2017 na kufungiwa kwa baadhi ya vyombo vya habari. Pia kutimuliwa nchini humo waandishi wawili wa Tume ya Kulinda Waandishi wa Habari (CPJ), Angela Quintal na Muthoki Mumo Novemba 2018 kumeitia dowa nchi hiyo.

Tukio jingine lililotikisa sekta ya habari ni kupotea katika mazingira ya kutatanisha kwa mwandishi wa kujitegemea, Azory Gwanda, zaidi ya siku 500 zilizopita.

Kuhusiana na mustakabali wa Azory Gwanda, Waziri wa Habari wa Tanzania hivi karibuni aliliambia Bunge la nchi hiyo kuwa: "Tunaongelea kesi ambayo ni dhaifu sana, mwandishi huyu amepotea eneo ambalo mamia ya Watanzania wengine wamepotea, hawauliziwi hao ila mmoja huyo ndiyo dhahabu."

"Halafu inaulizwa Serikali ambayo imeshughulikia kwa kiasi kikubwa na maofisa wa Serikali wengi wamekufa pale, najua mnawalisha Wazungu na wafadhili matangopori, hatujakosa chochote acha tushushwe madaraja, sisi tunaheshimu uhuru wetu kwanza," alisema.

Vyombo vya kimataifa marufuku Burundi

Image caption Serikali ya Burundi chini ya raisi Nkurunziza imeshutumiwa kwa kuzidisha uminywaji wa vyombo vya habari na wanahabari toka jaribio la mapinduzi mwaka 2015.

Mamlaka nchini Burundi mwezi Machi mwaka huu zimewapiga marufuku waandishi wa BBC na wale wa shirika la sauti ya Marekani VOA kutofanya kazi nchini humo.

Baraza la kitaifa la mawasiliano nchini humo lilisema kuwa halimruhusu mwandishi yeyote, awe raia wa Burundi ama yule wa kigeni kutoa habari yoyote kwa mashirika hayo ya habari.

Baraza hilo limeelezea kile kilichokiita 'uongo makala ya BBC mwaka uliopita kuhusu mauaji yaliotekelezwa na vikosi vya usalama katika nyumba za siri ndani ya mji mkuu wa Bujumbura'.

Mamalaka nchini Burundi zimesema kuwa makala hiyo ilikiuka sheria za habari nchini humo.

Lakini ukiachilia mbali kwa BBC na VOA hata vyombo vya ndani navyo vinapitia wakati mgumu.

Kwa mujimu wa ripoti ya Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka (RSF), hali mbaya nchini Burundi imeripotiwa toka jaribio lililofeli la mapinduzi mwezi Mei 2015.

"Redio nyingi binafsi bado zimefungwa. Makumi ya wanahabari bado hawawezi kurejea nyumbani kutoka uhamishoni, na wale ambao bado wapo Burundi, hawana uhuru wa kuripoti habari na imekuwa kawaida kwao kubughudhiwa na vyombo vya usalama," inasema sehemu ya ripoti hiyo na kuongeza: "Hakuna mwandishi yeyote aliyeripotiwa kuuawa ama kufungwa mwaka 2018, lakini vyombo vingi vya habari na wanahabari ametawaliwa na woga wa kupindukia."

Kwa upande wa Rwanda RSF inasema kuwa japo visa vya unyanywasaji a wanahabari vinapungua, lakini bado mkono wa serikali ni wa chuma kwa upande wa vyombo vya habari.

Kenya kwa mujibu wa RSF ndiyo nchi yenye unafuu, lakini nayo inashikilia nafasi ya 100 kwenye orodha yao ikiporomoka kutoka nafasi ya 96 kwa mwaka 2018.

RSF imetaja moja ya sababu ya kuporomoka kwa Kenya ni hatua ya kufungia kwa muda vituo vinne vya runinga mwanzoni mwa mwaka jana kwa kwa kukiuka marufuku ya mamlaka ya kurusha mbashara matangazo ya moja kwamoja ya hafla ya kujiapisha kwa Raila Odinga kuwa raisi wa wananchi.