Uhuru wa vyombo vya habari: Waandishi wangapi waliouawa mwaka jana duniani?

An injured journalist is helped by others during a street protest in Venezuela
Image caption Mwandishi aliyejeruhiwa asaidiwa na wengine wakati wa maandamano Venezuela

Takriban waandishi habari 95 wameuawa mwaka jana wakiwa kazini, kwa mujibu wa shirikisho la waandishi habari wa kimataifa (IFJ).

Idadi hiyo ipo juu zaidi ya ilivyoshuhudiwa 2017, lakini haipo juu sana kama viwango vilivyoshuhudiwa katika miaka ya nyuma wakati mzozo katika mataifa ya Iraq na Syria yalikuwa yakitokota.

Kiwango kikubwa cha vifo vya waandishi habari kilichowahi kunukuliwa ni waandishi 155 mnamo mwaka 2006.

Takwimu hizi zinajumuisha yoyote anaefanya kazi katika kiwango chochote katika shirika la habari.

Vifo vya waandishi habari

Chanzo: International Federation of Journalists

Kifo cha mwandishi kilichoigusa dunia mnamo 2018 kilikuwa cha mwandishi habari wa Saudia Jamal Khashoggi.

Aliuawa Oktoba baada ya kwenda katika ubalozi wa Saudia nchini Uturuki.

Haki miliki ya picha Getty Images

Mkasa huo ulizusha mzozo wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili na shutuma kali za kimataifa.

Na mwandishi wa habari za upelelezi nchini Ghana aliyepigwa risasi hadi kufa wakati akiendesha gari kwenda nyumbani, baada ya mwanasiasa kuitisha adhabu dhidi yake.

Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kuwa watu wasiojulikana wakiwa katika pikipiki walimpiga risasi Ahmed Hussein-Suale mara tatu katika mji mkuu wa Accra.

Alikuwa ni miongoni mwa wahusika wa shirika binafsi la upelelezi Tiger Eye na alipepeleza rushwa katika ligi ya mpira wa miguu Ghana.

Ni sehemu gani ilio hatari zaidi?

Afghanistan inasalia kuwa nchi ilio hatari zaidi kuishi kama mwandishi habari, kukishuhudiwa vifo vya waandishi 16 mwaka jana.

Waandishi 9 walifariki kwa wakati mmoja nchini Afghanistan katika mji mkuu Kabul, baada ya kufika katika eneo la shambulio la bomu kuripoti kuhusu kilichotokea.

Kumelipuliwa bomu la pili na mlipuaji aliyesemekana kujifanya kuwa mwandishi habari.

Na katika eneo la mashariki mwa Afghanistan, mwandishi wa BBC Ahmad Shah aliuawa katika mojawpao ya mashambulio hayo katika jimbo la Khost.

Waandishi habari walifariki Marekani pia mwaka jana.

Watano walipigwa risasi katika shambulio dhidi ya ofisi za gazeti la Capital Gazette huko Maryland, lililotekelezwa na mwanamume anayearifiwa alijaribu kulishtaki gazeti hilo miaka kadhaa nyuma.

Kutoweza kuvumilia taarifa za habari zinazo chapishwa, umaarufu, pamoja na rushwa na uhalifu ni vigezo muhimu sasa linasema IFJ.

Wanachangia "mazingira ambapo kuna waandishi zaidi wa habari wanauawa kwa kuangazia masaibu kwa jamii zao, mijini na hata mataifa, kuliko kuripoti matukio katika maeneo yanayokumbwa na mizozo".

Waandishi waliofungwa duniani

Chanzo: Committee to Protect Journalists

Kamati ya kuwalinda waandishi habari (CPJ) huwapiga picha waandishi wa habari waliofungwa gerezani mwanzo wa mwezi Desemba kila mwaka.

Takwimu hizi hujumuisha yoyote anayefanya kazi kama mwandishi habari, aliyefungwa kwa shughuli zinazohusiana na kazi yake.

Mataifa yenye idadi kubwa ya waandishi waliofungwa mnamo 2018 ni pamoja na:

  • Uturuki 68
  • China 47
  • Misri 25
  • Saudi Arabia na Eritrea 16 kila moja

Uandishi habari na demokrasia

Umoja wa mataifa mwaka huu unaangazia jukumu kuu la uandishi huru wa habari kwa demokrasia hususan wakati wa uchaguzi.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres anasema katika taarifa yake kwamba "hakuna demokrasia iliokamilika pasi kuwepo habari za wazi na za kuaminika."

Haki miliki ya picha Getty Images

Courtney Radsch, kutoka kamati ya kuwalinda waandishi habari CPJ, anasema kauli za kupinga uandishi habari zimeongezeka katika nchi nyingi akitaja zaidi Ufilipino na Marekani.

Anaamini mitandao ya kijamii na intaneti kwa jumla zimechangia katika masaibu yanayowakabili waandishi habari.

Katika faharasha yake ya mwaka huu - katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari , kundi la waandishi wasio na mipaka (RSF) wanaitaja hali Marekani kuwa ni 'tatizo'.

Marekani imeshuka kwenye orodha ya RSF katika uhuru wa waandishi habari mwaka huu na ni kama ilivyo kwa India na Brazil.

Lakini wanaongeza kwamba mataifa yalioshuhudia kiwango kibaya cha uhuru wa vyombo vya habari - kama Venezuela, Urusi na China - zimezidi kudidimia chini mwaka huu.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii