Tanzania: Mwili wa Reginald Abraham Mengi kuwasili Jumatatu

Marehemu Reginald Haki miliki ya picha IPP

Mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi utawasili jumatatu mchana Mei 6, 2019 jijini Dar es salaam kutoka Dubai ambapo alifikwa na umauti jumatano usiku.

Mwanasheria wa familia, Michael Ngalo amesema mwili wa mfanyabiashara huyo maarufu nchini Tanzania utahifadhiwa katika hospitali ya jeshi ya Lugalo baada ya kuwasili.

Siku ya Jumanne, marehemu ataagwa katika viwanja vya Karimjee.

Siku ya Jumatano Mei 8, 2019 mwili utasafirishwa kwenda Machame mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya maziko yatakayofanyika siku ya Alhamisi Mei 9, 2019.

"Baada ya mwili kuwasili Machame ibada ya mazishi itafanyika katika Kanisa la Kilutheri la Kiinjili Tanzania la Kisereni,"

Mzee Mengi alizaliwa mwaka 1942 mkoani Kilimanjaro na umauti umemkuta akiwa mjini Dubai, Falme za Kiarabu baada ya kuugua kwa muda mfupi, kwa mujibu wa familia yake.

Umauti umemfika akiwa na umri wa miaka 77, huku akicha mke na watoo wanne.

Historia ya Reginald Mengi

Mengi alizaliwa wilayani Machame, Kilimanjaro, Tanzania mwaka 1942, akiwa mmoja wa watoto saba wa Bw Abhraham Mengi na Bi Ndeekyo Mengi.

"Familia yetu ilikuwa masikini sana, kila siku ilikuwa ni vita ya kupambana na umasikini. Tulimiliki sio zaidi ya ekari moja tukiishi kwenye vibanda vya udongo tukichanganyika na ng'ombe wachache na kuku. Ninaporudisha fikra na kutazama nyuma ni vigumu napatwa na ugumu wa kufikiri namna tulivyoweza kuishi katika hali ile," alipata kusema kwenye uhai wake.

Alianza safari yake kielimu shule katika shule ya msingi Kisereny Village Bush School, kisha akajiunga Nkuu District School, kisha Siha Middle School, na baadaye Old Moshi Secondary School. Kwa ufadhili wa Chama cha Ushirika kilichokuwa na nguvu ya kifedha ushawishi KNCU Mengi alisomeshwa masomo yake ya shahada ya kwanza ya uhasibu nchini Uingereza.

Baada ya masomo ughaibuni, Mengi alirudi Tanzania 1971 na kuajiriwa na kampuni ya Cooper and Lybrand Tanzania ( sasa Prince water house Cooper) mpaka mwaka 1989 alipoamua kujikita kwenye ujasiriamali.

Haki miliki ya picha IPP

Baada ya kuachana na ajira, Mengi aliiboresha kampuni yake ya Industrial Projects Promotion Limited na baadae kufahamika zaidi kama IPP Limited.

Kupitia IPP Limited Mengi alaianzinza kampuni mbalimbali na kufanya biashara kadha wa kadha kuanzia uzalishaji wa sabuni, soda, maji ya kunywa, madini, mafuta, gesi asilia na kilimo.

Hata hivyo, umaarufu mkubwa wa Mengi ni kutokana na kumiliki vyombo vya habari, kuanzia magazeti, vituo vya runinga na redio. Runinga yake ya ITV pamoja na kituo cha Redio One ni moja ya vituo vikubwa vya utangazaji huku magazeti yake ya Guardian na Nipashe yakiwa miongoni mwa magazeti makubwa zaidi Tanzania.

Mpaka umauti unamfika, Mengi alikuwa mwenyekiti wa Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo Vya Habari Tanzania.

Mengi pia amekuwa akijitoa katika kusaidia wasionacho na wenye uhitaji kwenye jamii ikiwemo walemavu wa ngozi na kugharamia matibabu ya watoto wnye matatizo ya moyo nchini India.

Mwaka 2014, jarida maarufu la masuala ya fedha Forbes lilikadiria utajiri wa Mengi kuwa unafikia dola milioni 560.

Haki miliki ya picha Jacqueline Ntuyabaliwe/Facebook

Mjane wa Mzee ni Jacqueline Ntuyabaliwe ambaye alipata kuwa Miss Tanzania mwishoni ma miaka ya 90.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii