Mdude Chadema: Watu wasiojulikana wamteka mwanachama wa upinzani Tanzania

Polisi Tanzania

Polisi katika eneo la Songwe nyanda za juu kusini mwa Tanzania imesema kwa haina taarifa kuhusu tukio la kukamatwa kwa kijana Mdude Nyangali maarufu Mdude Chadema anayedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana siku ya jumamosi.

Tukio hilo limeendelea kuzua gumzo katika mitandao ya kijamii ndani na nje ya nchi hiyo huku wanaharakati wa kutetea haki wakianzisha kampeini ya kutaka kijana huyo achiwe huru.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, George Kyando ameliambia gazeti la Mwananchi kuwa ''hajazipata'' taarifa ya kukamatwa kijana huyo.

Kupitia hashtag ya #BringBackMdudeAlive katika mtando wa kijamii wa Twitter wanaharakati wa kutetea haki nchini Tanzania wameungana na wanaharakati wenzao nchini Kenya kushinikiza Mdude Chadema achiliwe huru na watekaji wake au wamrudishe akiwa salama.

Tayari chama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimelaani kitendo hicho na kutoa wito Mdude arudishwe au aachiliwe akiwa salama.

''Katika hatua ya sasa, CHADEMA kwa nguvu zote kinalaani vikali tukio hilo. Tunavitaka vyombo vya dola, hususan Jeshi la Polisi lenye wajibu wa kulinda raia na mali zao, kufuatilia taarifa za tukio hilo kama zilivyoripotiwa kwa polisi katika eneo husika na kuhakikisha Mdude anapatikana na wahalifu waliotenda tukio hilo wanajulikana, kukamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.'' alisema ilisema taarifa ya chama hicho iliyotolewa kwa vyombo vya habari.

Chama hicho pia kimevitaka vyombo vya dola, hususan Jeshi la Polisi lenye wajibu wa kulinda raia na mali zao, kufuatilia taarifa za tukio hilo kama zilivyoripotiwa kwa polisi katika eneo husika na kuhakikisha Mdude anapatikana na wahalifu waliotenda tukio hilo wanajulikana, kukamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.

''Baada ya kuendelea kupokea na kufanyia kazi taarifa mbalimbali, kuhusu tukio hilo la Mdude, Chama kitazungumza na vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa kuhusu suala hili, siku ya Jumatatu, Mei 6, mwaka huu, ili kupaza sauti kubwa dhidi ya tukio hili na mengine ya namna hiyo yanayohusu utekwaji na upotezwaji wa wananchi katika mazingira yenye utata unaoibua maswali yanayotakiwa kujibiwa na mamlaka au vyombo vilivyopewa dhamana ya Kikatiba na kisheria kuhakikisha uhai wa raia ni jukumu namba moja kwa Serikali yoyote iliyoko madarakani.''

Kwa upande wake Mwanaharakati wa Kenya Boniface Mwangi aliandika maneno haya katika mtando wake wa Twitter

Taarifa za awali kutoka kwa watu waliyoshuhudia tukio hilo zimedai kuwa baada ya kusikika kwa purukushani na kelelekatika duka la Mdude Chadema, baadhi ya wananchi walijitokeza kutaka kujua kilichokuwa kikiendelea ili kutoa msaada, lakini ghafla watu waliokuwa wakimpiga Mdude walitoa silaha aina ya bastola na kuwatishia wananchi hao, kitendo kilichowaogofya wananchi na kukimbia kwa hofu.

Imedaiwa kuwa watu hao walimuingiza Mdude kwenye 'buti' ya mojawapo ya gari hizo, wakamuachia yule kijana mwingine kisha wakaondoka na Mdude kuelekea kusikojulikana.

Haki miliki ya picha Twiter
Image caption Mdude Chadema

Madai ambayo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, George Kyando amekanusha katika mahojiano yake na Gazeti la Mwananchi nchini Tanzania

"Mimi ni mkazi wa eneo linalodaiwa kuwa risasi zimepigwa lakini sijasikia na kama unavyojua mji wa Vwawa ni mdogo ambao zikipigwa risasi lazima utasikia," alisema.

Hata hivyo, Kamanda Kyando amesema ataendelea kufuatilia kwa kina zaidi juu ya taarifa hizo.

Kuna baadhi ya watu wanaohoji kampeni za kupigania haki kupitia miyandao ya kijamii.

Baada ya kutekwa kwa Bilionea Mohammed Dewji mweizi Oktoba mwaka jana Waziri wa mambo ya Ndani Tanzania Kangi Lugola alijitokeza na kusema kuwa kuna hofu kwa Watanzania juu ya matukio ya kutekwa na kuongeza kuwa hofu hiyo inabidi iondolewe.

Matukio ya watu kutekwa au kushambuliwa na watu wasiojulikana

  • Mauaji ya Kibiti mwaka 2017: Viongozi wa CCM, askari zaidi ya 10 na wananchi karibu 40 katika eneo la Kibiti walishambuliwa na kuuawa na watu wasiojulikana.
  • 11 Februari, 2018 Kiongozi wa Chadema Daniel John alitekwa na kisha aliuwawa kikatili wakati wa Kampeni za Uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni. Mwili wake ulipatikana mnamo 14 Februari.
  • Aprili 2017, Mwanamuziki Roma Mkatoliki na wenzie wawili watekwa na watu wasiojulikana na kuachiwa baada ya siku 3.
  • Mnamo 7 Septemba, 2017, Mnadhimu Mkuu wa upinzani bungeni, mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu alipigwa risasi na watu wasiojulikana katika eneo la Area D Mkoani Dodoma. Bw Lissu pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika.
  • 21 Novemba, 2017 Mwandishi wa habari wa Mwananchi Communications Limited Azory Gwanda alipotea katika mazingira ya kutatanisha na mpaka sasa hajapatikana.
  • Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema Ben Saanane alipotea katika mazingira ya kutatanisha.

Visa 21 vya watu kutekwa viliripotiwa mwaka 2018 na kati ya hivyo watu 17 walipatikana salama.

Hata hivyo kwa miaka ya karibuni nchini Tanzania kutekwa, kuchukuliwa ama kushambuliwa na watu wasiojulikana kumekuwa ni hali ya kutisha.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii