Ramadhan 2019: Wakenya 'waanza' Ramadhan mbele ya Tanzania

Muumini wa dini ya Kiislam akisali Haki miliki ya picha Getty Images

Waumini wa dini ya Kiislam nchini Kenya wameanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Hii ni baada ya Kadhi Mkuu Ahmed Muhdhar kutangaza mwandamo wa mwezi mjini Hola pwani ya Kenya.

Sheikh Muhdhar amesema mwandamo wa mwezi unaashiria mwanzo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

"Tulipokea taarifa za kuandama kwa mwezi kutoka kwa sheikh Said Jillo wa Tana River ndio tukatangaza mfugo unaanza (Jumatatu)," alisema Sheikh Muhdhar akiwa mjini Mombasa siku ya Jumapili.

Mataifa kama Saudia Arabia, Algeria, Qatar, Libya na Turkey pia yameanza mfungo wa mwezi wa Ramadhan siku ya Jumatatu.

Waislamu katika taifa jirani la Tanzania wataanza mfungo wa ramadhani mara baada ya kukamilika siku 30 za mwezi Shaaban.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Tende mara nyingi huliwa wakati wa iftar

"Tumekubaliana tumetimiza siku 30 za mwezi Shaaban, hivyo tutaanza kufunga siku ya Jumanne," Kadhi Mnyasia aliiambia televisheni ya Shirika la Utangazaji Tanzania.

Ramadhan ni mwezi wa tisa katika kalenda ya Kiislam, na unaaminiwa kuwa mwezi mtukufu zaidi na waumini wa dini ya Kiislam.

Kwa mujibu wa mafundisho ya Quran, waislamu wanatakiwa kuanza kufunga kula na kunywa baada ya kuuona mwezi

Ramadhan ni nini?

  • Ramadhan ni moja ya nguzo tano kuu katika dini ya Kiislamu.
  • Mwezi huo, Waislamu hujifunga kula na kunywa kuanzia macheo hadi machweo.
  • Kufunga wakati huu huwawezesha Waislamu kujitolea zaidi katika dini na kumkaribia Allah.
  • Kando na kufunga, ni wakati pia wa kutafakari kiroho, kuswali, kutenda matendo mema na kujumuika na familia na marafiki.
Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Iftar msikitini

Waislamu hufanya juhudi za kipekee kuungana na wengine katika jamii na kuwasaidia wale wanaohitaji usaidizi katika jamii.

Huwa ni kawaida kwa Waislamu kula chakula asubuhi kabla ya mawio, suhur, na jioni wakati wa kufungua baada ya jua kutua, ambacho hufahamika kama iftar.

Mwisho wa kufunga, baada ya machweo, familia na marafiki hujumuika pamoja kufungua.

Wengi pia huenda Msikitini kuswali.

Ramadhan imekuwa mwezi huu kwa sababu ndio wakati Koran tukufu ilipofichuliwa kwa mara ya kwanza kwa Mtume Muhammad.

Ramadhan huwa ni mwezi wa tisa katika kalenda ya Kiislamu, lakini tarehe hiyo hubadilika kila mwaka.

Hii ni kwa sababu dini ya Kiislamu hufuata kalenda inayotumia mzunguko wa mwezi, hivyo hubadilika tofauti na kalenda inayotumiwa na mataifa ya Magharibi inayofuata jua.

Ni kila mtu hufunga?

Si kila Mwislamu hufunga wakati wa Ramadhan.

Watoto, wanawake waja wazito, wazee na wagonjwa au wanaosafiri wameruhusiwa kutofunga wakati wa mwezi huu mtukufu.

Watoto hutakiwa kuanza kufunga punde wanapobalehe, ambapo kawaida huwa ni wakiwa na miaka 14.

Mtu mzima anaweza kufidia siki ambazo hakufungwa wakati wowote katika mwaka au kulipa fidyah, ambapo mtu hutoa msaada wa chakula au pesa kwa kipindi ambacho hakufunga.

Mwisho wa mwezi wa ramadhan, ambao mwaka huu utakuwa 14 Juni, au karibu na hapo, huwa kuna maadhimisho ya siku tatu ya sikukuu ya Eid al-Fitr.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii