Pascal Haonga: Mbunge wa Mbozi akamatwa akitoka bunge Tanzania

Pascal Haonga Haki miliki ya picha Bunge

Mbunge wa chama cha upinzani nchini Tanzania Pascal Haonga amekamatwa nje ya majengo ya bunge.

Kiongozi huyo wa eneo bunge la Mbozi alikamatwa baada ya kikao cha bunge siku ya Jumatatu jioni kukamilika.

Kulingana na mwenzake wa eneo bunge la Momba David Silinde bado wanasubiri kujua kiini cha mwenzao kukamatwa.

Tayari inadaiwa kwamba maafisa wa polisi wamemuarifu kwamba makosa yake yamefunguliwa kesi mkoani Songwe.

"Ni kweli amekamatwa nje ya geti wakati akitoka bungeni leo jioni. Hajaambiwa kosa na wala sisi hatujui kosa. Tuko kwa RCO ( Mkuu wa Upelelezi) wanasema wanasubiri gari la kumpeleka Songwe," amesema mbunge hiyo alipokuwa akizungumza na gazeti la Mwananchini nchini humo.

Hatahivyo kamanda wa Polisi Mkoani Dodoma, Gilles Muroto amesema hana taarifa za kukamatwa kwa mbunge huyo.

"Niko Gairo sijapata taarifa zozote za kukamatwa kwa mbunge huyo," amesema Muroto.

Kumatwa kwake kunajiri baada ya maafisa wa polisi kudai hawana tarifa yoyote kuhusu kutoweka kwa mwanachama mwengine wa upinzani kijana Mdude Nyangali maarufu Mdude Chadema anayedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana siku ya jumamosi.

Tukio hilo limeendelea kuzua gumzo katika mitandao ya kijamii ndani na nje ya nchi hiyo huku wanaharakati wa kutetea haki wakianzisha kampeini ya kutaka kijana huyo aachiwe huru.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, George Kyando ameliambia gazeti la Mwananchi kuwa ''hajazipata'' taarifa ya kukamatwa kwa kijana huyo.

Kupitia hashtag ya #BringBackMdudeAlive katika mtando wa kijamii wa Twitter wanaharakati wa kutetea haki nchini Tanzania wameungana na wanaharakati wenzao nchini Kenya kushinikiza Mdude Chadema achiliwe huru na watekaji wake au wamrudishe akiwa salama.

Tayari chama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimelaani kitendo hicho na kutoa wito Mdude arudishwe au aachiliwe akiwa salama.

''Katika hatua ya sasa, CHADEMA kwa nguvu zote kinalaani vikali tukio hilo. Tunavitaka vyombo vya dola, hususan Jeshi la Polisi lenye wajibu wa kulinda raia na mali zao, kufuatilia taarifa za tukio hilo kama zilivyoripotiwa kwa polisi katika eneo husika na kuhakikisha Mdude anapatikana na wahalifu waliotenda tukio hilo wanajulikana, kukamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.'' alisema ilisema taarifa ya chama hicho iliyotolewa kwa vyombo vya habari.

Chama hicho pia kimevitaka vyombo vya dola, hususan Jeshi la Polisi lenye wajibu wa kulinda raia na mali zao, kufuatilia taarifa za tukio hilo kama zilivyoripotiwa kwa polisi katika eneo husika na kuhakikisha Mdude anapatikana na wahalifu waliotenda tukio hilo wanajulikana, kukamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.

''Baada ya kuendelea kupokea na kufanyia kazi taarifa mbalimbali, kuhusu tukio hilo la Mdude, Chama kitazungumza na vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa kuhusu suala hili, siku ya Jumatatu, Mei 6, mwaka huu, ili kupaza sauti kubwa dhidi ya tukio hili na mengine ya namna hiyo yanayohusu utekwaji na upotezwaji wa wananchi katika mazingira yenye utata unaoibua maswali yanayotakiwa kujibiwa na mamlaka au vyombo vilivyopewa dhamana ya Kikatiba na kisheria kuhakikisha uhai wa raia ni jukumu namba moja kwa Serikali yoyote iliyoko madarakani.''

Kwa upande wake Mwanaharakati wa Kenya Boniface Mwangi aliandika maneno haya katika mtando wake wa Twitter

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii