Taarifa feki

Mwandishi wa habari wa BBC Roncliffe Odit akimpatia maziwa mzee Lomoni
Image caption Mwandishi wa habari wa BBC Roncliffe Odit akimpatia maziwa mzee Lomoni

Ni picha ya mzee Lomoni kutoka Kaunti ya Turkana nchini Kenya ambayo imekuwa ikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwa madai kwamba ni kanali wa Jeshi nchini Sudan ambaye alikuwa amefungwa na Rais aliyeondolewa madarakani Omar Bashir.

Kwenye Uvumi huo ulioanzishwa na mitandao ya kijamii kutoka Sudan, picha ya aneyedaiwa kuwa kanali Ibrahim Chamsadine ilichapishwa kando ya mzee Lomoni Liwani na ujumbe kwamba ni Kanali huyo akiwa gerezani alikofungiwa mwaka wa 1995 na rais.

Ujumbe huo pia uliongeza kuwa kanali huyo alipatikana katika jela chini ya msikiti mmoja nchini Sudan ilhali alikuwa ametangazwa kufariki tarehe 11 Juni 2008.

Ukweli ni kwamba picha hiyo ni ya Mzee Lomoni iliyopigwa na waandishi wa BBC mwezi Machi wakati wa ukame katika kaunti ya Turkana.

Waandishi wa BBC walimkuta mzee Lomoni akiwa amelala kwenye sakafu ndani ya nyumba yake ijulikanayo kama Manyatta. Mzee Lomoni alikuwa amejifunga shuka kiunoni na kkuegeza kichwa chake kwenye kiti ambacho hukaliwa na wazee wa jamii hiyo ijulikanayo kama Ekicholong' .

Alipoarifiwa kwamba alikuwa na wageni wanahabari kutoka BBC, mzee huyo aliamka kuwaamkua wanahabari na baada ya kuwasiliana, mzee huyo aliwaruhusu waandishi hao kumpiga picha ili kuangazia baa la njaa ilivyowaathiri wakaazi wa eneo hilo.

Hapo ndipo waandishi wa BBC walivyopata nafasi ya kupiga picha hiyo na zingine kadhaa.

"Nilipoona picha ya mzee huyu ikisambazwa, nilipigwa na butwaa kwa sababu mimi na mpiga picha wangu tunafahamu huyu mzee. Tulikutana naye mwezi wa Machi tukiangazia tatizo la baa la njaa katika kaunti ya Turkana nchini Kenyana mpiga picha wangu Faith Sudi, tuliumizwa sana na hali ambayo tulimkuta. Tulizungumza na jamaa zake kuhusiana na hali yake. Kwa hivyo inachukiza sana kuona watu kwenye mitandao ya kijamii wakieneza habari gushi kuhusu mzee huyu" Roncliff Odit mwanahabari wa BBC anaelezea.

Image caption Mzee Lomoni akiwa amelala ndani ya nyumba yake

Habari hiyo gushi ilisambaa sana kwenye mitandao ya vyombo vya habari na pia watu wenye ushawishi kwenye mitandao ya kijamii.

Hata hivyo ilizua migawanyiko kwani watu wengine kwenye mitandao ya kijamii waliamini na wengine kutoamini na kudai kwamba wanafahamu picha hiyo.

Robert Esekon ambaye ni jirani yake mzee Lomoni na ambaye pia ni afisa wa afya katika kliniki ya Louwae ameelezea hisia zake kuhusiana na uvumi huo.

"Nilipoona picha yake kwenye mitandao ya kijamii kwamba anadaiwa kuwa kanali wa kijeshi nchini sudan, nilikasirisha sana kwa sababu hiyo ni kupotosha hadhira kwa ukweli kwamba mzee huyo alikuwa muathiriwa wa baa la njaa"

Robert anasema kwamba hali ya mzee Lomoni imeimarika pakubwa tangu walipopokea misaada ya chakula.

"Tumemweka mzee katika matibabu ya utapia mlo na hali yakke ya afya inaendelea kuimarika."

Kulingana na mwakilishi wa wadi ya Kerio ambayo mzee Lomoni anatoka mheshimiwa Peter Ikaru, mzee huyo ni mkaazi wa wadi yake na anaifahamu familia yake vizuri.

"Ujumbe unaoenezwa ni uvumi, ni uongo mtupu. Picha hiyo ni ya Lomoni Liwanambaye ni mkaazi wa wilaya ya Nakurio kijiji cha Lotukumo. Ni mzee ambaye ninamtambua vizuri kwa sababu tunatoka kijiji kimoja"

Image caption Mwakilishi wa Wadi ya Kerio, Peter Ikaru

Hata hivyo mwakilishi huyo aliwasuta wale ambao wanaeneza uvumi kwamba ni kanali wa kijeshi nchini Sudan.

"Huyu ni mturkana. Huyu ni mkenya ambaye tunajua hali yake na tunajua nyumbani kwake. Hajatembelea nchi jirani, hajaenda kokote halafu mtu anakuja kusema kwamba ni raia wa Sudan…"

Kulingana na mheshimiwa huyo,uvumi huo umeathiri jamii yake .

"sisi kama jamii tumekerwa, tumegadhabishwa na tumekasirishwa na uvumi huo kwa sababu kama wewe ni Mkenya alafu uhusishwe na nchi nyingine utajihisi namna gani, hautajihisi huru, na utaishi kama mtumwa katika nchi yako. Hiyo ni taarifa ya kuharibia watu jina"

Hata hivyo ameiomba serikali kuwachukulia hatua walioanzisha uvumi huo

"Sisi tuko tayari kuonyesha ulimwengu mahali huyo mzee yuko , hata leo hii, hata sasa hivi ili kuthibitisha na kueleza ukweli kwamba huyo mzee ni wetu. Ikiwa kuna sheria ambayo itamruhusu mtu kutetea habari yoyote ambayo hajadhihirisha ukweli wake, basi tuelezwa lakini kama watu hao walitumia uvumi huo kujinufaisha basi mkono wa sheria ichukue mkondo wake "

Uvumi huo ulionukuliwa na washawishi kadhaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba ulichapishwa na Tchad One kwenye mtandao wa Facebook,bado mwanzo wake haujabainishwa baada ya Tchad One kuandika kwamba haikuhusika katika kuchapisha uvumi huo.

Kufikia sasa, kuwepo kwa kanali huyo haijulikani.

Mzee Lomoni si muathiriwa wa kwanza wa habari ghushi, watu wengi wakiwemo wanamuziki, wanasiasa na wanahabari mara nyingi hujikuta katika hali kama hii. Wengi wao wameuliwa kabla ya siku zao kuwadia.

Mwaka uliopita shirika la BBC lilizindua utafiti wa uenezaji wa habari gushi barani Afrika ambapo iliandaa kongamano lililojumuisha wanahabari, watu wenye ushawishi katika mitandao ya kijamii na washikadau wengine ili kutathmini vyanzo vya habari gushi na athari zake.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii