Reginadl Abraham Mengi: Mwili wa bilionea wa Tanzania kuzikwa leo

Jeneza lililoubeba mwili wa Dkt. Reginald Mengi likiingizwa katika ukumbi wa Karimjee

Siku mbili baada ya mwili wa bilionea wa Tanzania marehemu Reginald Abraham Mengi kuwasili mjini Dar es Salaam mwili wa mwanzilishi huyo wa makampuni ya IPP umewasili mjini Kilimanjaro tayari kwa mazishi yake.

Mamia ya marafiki na watu wa familia walikongamana katika uwanja a ndege wa Kilimajaro kuupokea mwili wa mfanyibiashara huyo na msomi aliyefariki akiwa na umri wa miaka 75.

Kulingana na mtandao wa The Citizen nchini Tanzania Baadaye msafara wake unatarajiwa kuelekea nyumba kwa marehemu katika eneo la machame wilaya ya hai ambapo waombolezaji watamuombea.

Kulingana na vyanzo vya familia mwili huo unatarajiwa kupelekwa hadi Moshi mjini mapema Alhamisi alfajiri ambapo wakaazi wa eneo hilo watatoa heshima zao za mwisho kwa mtu aliyekuwa maarufu kwa kuwasaidia wengi.

Kamanda wa jimbo la Kilimajaro Anna Mwira alisema kuwa hatua ya kuusafirisha mwili huo hadi Moshi ilitokana na ombi la watu wengi ili kuwqaruhusu watu wa Moshi kutoa heshima zao za mwisho.

Haki miliki ya picha IPP

Tulikuwa tumejiandaa kufanya kila kitu katika eneo la Machame lakini kukatokea ombi kutoka kwa wakaazi waliofanya kazi kwa karibu na kumjua marehemu kutoa heshima yao ya mwisho, alisema kamishan huyo wa eneo la Kilimajaro.

Mazishi yake kulingana na msemaji wa familia Michael Ngalo yatafanyika hapo kesho baada ya misa ya wafu.

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli, ameongoza mamilioni ya Watanzania kutuma salamu za rambirambi kufuatia msiba huo.

Kupitia ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Twitter Magufuli amesema ataendelea kumkumbuka Mzee Mengi kwa mchango wake katika maendeleo ya taifa lake.

Historia ya Reginald Mengi

Mengi alizaliwa wilayani Machame, Kilimanjaro, Tanzania mwaka 1942, akiwa mmoja wa watoto saba wa Bw Abhraham Mengi na Bi Ndeekyo Mengi.

"Familia yetu ilikuwa masikini sana, kila siku ilikuwa ni vita ya kupambana na umasikini. Tulimiliki sio zaidi ya ekari moja tukiishi kwenye vibanda vya udongo tukichanganyika na ng'ombe wachache na kuku. Ninaporudisha fikra na kutazama nyuma ni vigumu napatwa na ugumu wa kufikiri namna tulivyoweza kuishi katika hali ile," alipata kusema kwenye uhai wake.

Alianza safari yake kielimu shule katika shule ya msingi Kisereny Village Bush School, kisha akajiunga Nkuu District School, kisha Siha Middle School, na baadaye Old Moshi Secondary School. Kwa ufadhili wa Chama cha Ushirika kilichokuwa na nguvu ya kifedha ushawishi KNCU Mengi alisomeshwa masomo yake ya shahada ya kwanza ya uhasibu nchini Uingereza.

Baada ya masomo ughaibuni, Mengi alirudi Tanzania 1971 na kuajiriwa na kampuni ya Cooper and Lybrand Tanzania ( sasa Prince water house Cooper) mpaka mwaka 1989 alipoamua kujikita kwenye ujasiriamali.

Baada ya kuachana na ajira, Mengi aliiboresha kampuni yake ya Industrial Projects Promotion Limited na baadae kufahamika zaidi kama IPP Limited.

Kupitia IPP Limited Mengi alaianzinza kampuni mbalimbali na kufanya biashara kadha wa kadha kuanzia uzalishaji wa sabuni, soda, maji ya kunywa, madini, mafuta, gesi asilia na kilimo.

Hata hivyo, umaarufu mkubwa wa Mengi ni kutokana na kumiliki vyombo vya habari, kuanzia magazeti, vituo vya runinga na redio. Runinga yake ya ITV pamoja na kituo cha Redio One ni moja ya vituo vikubwa vya utangazaji huku magazeti yake ya Guardian na Nipashe yakiwa miongoni mwa magazeti makubwa zaidi Tanzania.

Mpaka umauti unamfika, Mengi alikuwa mwenyekiti wa Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo Vya Habari Tanzania.

Haki miliki ya picha Jacqueline Mengi/facebook

Mengi pia amekuwa akijitoa katika kusaidia wasionacho na wenye uhitaji kwenye jamii ikiwemo walemavu wa ngozi na kugharamia matibabu ya watoto wnye matatizo ya moyo nchini India.

Mjane wa Mzee ni Jacqueline Ntuyabaliwe ambaye alipata kuwa Miss Tanzania mwishoni ma miaka ya 90.

Mwaka 2014, jarida maarufu la masuala ya fedha Forbes lilikadiria utajiri wa Mengi kuwa unafikia dola milioni 560.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii