Victor Wanyama na Divock Origi: Shauku kubwa kwa Wakenya Liverpool na Tottenham kufuzu fainali ya Champions League

Victor Wanyama of Tottenham Hotspur celebrates Haki miliki ya picha Julian Finney
Image caption Mkenya Victor Wanyama wa Tottenham Hotspur

Mashabiki wa soka katika mitandao ya kijamii wamekuwa wakijadili ushindi wa timu ya Liverpool na Tottenham zinazotarajiwa kuminyamana katika fainali ya ligi ya mabingwa katika mji wa Madrid Uhispania.

Kuna shauku kubwa miongoni mwa Wakenya huku baadhi wakihoji kwamba fainali hiyo ni kama Derby ya 'Mashemeji'.

Na hilo ni kwasababau wachezaji nyota wawili wa Kenya wanazichezea timu zitakazokutana katika fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya Juni mosi.

Divock Origi, mchezaji mwenye asili ya Kenya aliyezaliwa Ubelgiji, alichangia ufanisi wa Liverpool kwa mabao mawili dhidi ya Barcelona siku ya Jumanne.

Tottenham Hotspur imeishinda Ajax hapo jana Jumatano, na kumkatia tiketi mchezaji wa kiungo cha kati wa Kenya Victor Wanyama kucheza dhidi ya Liverpool katika fainali ya ligi hiyo ya mabingwa Ulaya.

Kakake Wanyama, McDonald Mariga, alishinda Champions League akiichezea Inter Milan mnamo 2010 na alikuwa Mkenya wa kwanza kucheza soka ya juu Italia na Uhispania.

Origi na Wanyama watakutana Madrid Juni mosi kwa mtanange huo.

'Meshemeji Derby' kwa Wakenya

Fainali hiyo ya ligi ya mabingwa inatazamiwa pakubwa na kwa shauku kubwa na mashabiki nchini Kenya ambao baadhi wameitazama kama mechi maarufu nchini inayofahamika kama 'Mashemeji derby'

Huwa ni mechi kati ya timu mbili kuu za soka Nairobi A.F.C. Leopards na Gor Mahia. Ni mechi yenye uhasama wa jadi na yenye historia kubwa kati ya mashabiki wa timu ya Gor Mahia - wengi walio kutoka kabila la WaLuo, na AFC leopards wengi wa kutoka kabila la WaLuhya, ndiposa kuitwa 'mashemeji'- licha ya kujumuisha pia mashabiki kutoka jamii nyingine nchini.

Klabu hizo mbili zimekuwa mahasimu wa jadi tangu kwanza kuingia uwanjani kushindana inaarifiwa mnamo 1968.

Sifa kedekede zimemiminika kutoka akiwemo naibu rais nchini Kenya William Ruto aliyewapongeza wachezaji hao wawili wenye asili ya Kenya kwa kung'aa katika mechi zao katika ligi hiyo ya mabingwa Ulaya.

Baadhi ya raia nchini Kenya wakachukua fursa kuangazia sifa ya kuwa na nyota kama Wanyama na Origi na jitihada inayoweza kufanywa na serikali katika kuimarisha vipaji au talanta miongoni mwa vijana nchini.

Haki miliki ya picha TF-Images
Image caption Divock Origi, mchezaji mwenye asili ya Kenya aliyezaliwa Ubelgiji, anayeichezea FC Liverpool

Suala tete la mishahara duni kwa wachezaji na miundo msingi likigusiwa katika majadiliano ya baadhi ya mashabiki kwenye mitandao ya kijamii.

Utafiti mkubwa kuhusu masuala ya soka duniani unaonyesha kuwa maisha miongoni mwa baadhi ya wanasoka wa Afrika, yana tofauti kubwa na maisha ya wale walio na bahati ya kusakata soka kwenye vilabu vikubwa duniani.

Mnamo 2016, chama cha wacheza soka wa kulipwa cha kimataifa (Fifpro), kilifanya utafiti wa dunia nzima kwa karibu wanasoka 14,000 kwenye nchi 54, na kubaini kwamba: mishahara duni, ukosefu wa mikataba, dhulma au unyanyasaji wa kimwili, na upangaji wa matokeo, ni baadhi ya matatizo yanayowakabili wachezaji katika mataifa ya Afrika.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii